Dar es Salaam. Ni bajeti ya kicheko na maumivu, hivi ndivyo inavyoweza kutafsiriwa kufuatia bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kuwa na pande mbili zinazowagusa wananchi.
Wapo ambao huenda wakapata nafuu kupitia bajeti hiyo baada ya kuwa na mapendekezo ya kuondolewa kwa kodi na tozo mbalimbali hali itakayosaidia kupunguza gharama na kuleta unafuu.
Akiwasilisha bajeti hiyo bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amependekeza kufanyika kwa maboresho ya mfumo wa kodi, ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya sheria mbalimbali pamoja na kuboresha taratibu za ukusanyaji na usimamizi wa mapato ya Serikali.
Amesema maboresho hayo yamefanyika kwa kuzingatia migogoro na vita vya kibiashara baina ya mataifa yaliyoendelea, kutokana na nchi ya Marekani kutangaza mabadiliko mbalimbali ya kisera kwa lengo la kuinua uchumi wake.
Eneo mojawapo ambalo linatarajiwa kuleta ahueni ni neema ya kuongezwa kwa pensheni ya wastaafu wanaolipwa na hazina kwa asilimia 150.
Dk Mwigulu Nchemba amesema hatua inatokana na Serikali kutambua umuhimu na mchango mkubwa wa wastaafu katika ujenzi wa Taifa.
“Kwa kuzingatia hilo, katika mwaka 2025/26, Serikali itaongeza kima cha chini cha pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu wanaolipwa na Hazina kutoka Sh100,125.9 hadi Sh250,125.9, sawa na ongezeko la asilimia 149.8 na utekelezaji wake utaanza katika pensheni ya Julai 2025,”.
Mapendekezo mengine ya kicheko ni kupunguzwa kwa kodi ya usajili wa pikipiki za kibiashara maarufu, bodaboda.
Katika eneo hilo alipendekeza kufanyiwa marekebisho kwenye Kanuni za Sheria ya Usalama Barabarani za mwaka 2024 ili kupunguza kodi hiyo kwa asilimia 50.
“Napendekeza kupunguza ada ya usajili wa pikipiki za biashara kutoka Sh340, 000 hadi Sh170,000 kwa miaka mitatu. Ada husika italipwa wakati wa usajili wa awali pekee. Pia kufuta kodi ya mapato kwa mwaka inayolipwa kwa utaratibu wa presumptive tax na kuanzisha ulipaji wa mara moja wa ada na presumptive tax kwa kiasi cha Sh120,000 badala ya Sh290,000. Ada na kodi hii italipwa wakati wa usajili,” amesema.
Unafuu kwenye sekta hiyo haukuishia hapo, Serikali imependekeza pia kupunguzwa kwa ada ya leseni ya uendeshaji wa pikipiki, bajaji na guta kutoka Sh70,000 hadi Sh30, 000.
Kicheko kingine kinaonekana kwenye sekta ya habari kufuatia pendekezo la msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye magazeti yanayozalishwa nchini.
Akizungumzia hilo, Dk Mwigulu amesema hatua hiyo inalenga kupunguza gharama za magazeti hayo na hivyo kuwezesha upatikanaji wa taarifa muhimu kwa wananchi.
“Hatua hii inalenga kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh1.27 bilioni”, amesema Dk Mwigulu.
Waziri huyo amependekeza pia Serikali kupunguzwa kwa kiwango cha ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vya kuongeza nguvu ‘energy drink’.
Ushuru wa bidhaa ya vinywaji hivyo vinavyozalishwa ndani ya nchi, imepungua kutoka Sh561 kwa kila lita hadi Sh134.2 kwa kila lita.
Mwigulu amesema lengo la hatua hiyo ni kuweka unafuu kwa wazalishaji wa ndani wanaozaliwa energy drink, kuongeza ushindani na kuchochea uwekezaji nchini.
Hata hivyo amesema hatua hiyo inatarajia kupunguza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh1.7 bilioni.
Waziri Mwigulu pia anapendekeza kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148 ili kusamehe kodi ya ongezeko la thamani kwenye viuatilifu vinavyotambulika kwa HS Codes 3808.61.00, 3808.62.00 na 3808.69.00.
Anasema hatua hiyo inalenga kuwapa unafuu wakulima ya kupata dawa za kuua wadudu mashambani na hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao nchini.
Upande wa pili wa bajeti hii ni maeneo ambayo yametakiwa kutozwa kodi ikihusisha baadhi ya bidhaa zinazotumiwa na watu wengi ikiwemo aisikrimu na soseji zinazozalishwa nchini.
Katika eneo hilo amesema Serikali inatarajia kutoza ushuru wa bidhaa kwa kiwango cha asilimia 5 kwenye aisikrimu zinazotengezwa nchini kwa kutumia kakao au malighafi nyingine, na asilimia 10 kwa zile zinazoingizwa kutoka nje ya nchi.
“Lengo la hatua hii ni kupunguza athari za kiafya zinazotokana na matumizi ya bidhaa hizi, kuongeza mapato ya Serikali na kulinda wazalishaji wa ndani. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh119 bilioni,” anasema.
Anasema bidhaa hizo zinatambulika kwa HS Code 1601.00.00 na kwamba lengo la hatua hiyo ni kuongeza mapato ya Serikali, kuvutia uwekezaji nchini na kulinda wazalishaji wa ndani, hatua inayotarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha Sh2.4 bilioni.
Waziri huyo pia amependekeza kufanyika kwa marekebisho kwenye Sheria ya Bima, sura 394 ili kuanzisha bima ya usafiri kwa wageni wanaoingia hapa nchini kwa kiwango cha dola za Marekani 44 kama ilivyo kwa upande wa Zanzibar.
Oktoba 1, 2024 Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia ofisi ya Rais, Fedha na Mipango ilianzisha mpango wa bima za safari kwa wageni wote wanaoingia Zanzibar.
Bima hiyo iliibua mjadala mkubwa visiwani humo wengi wakiwa na hofu kuwa itadhoofisha hali ya utalii. Hata hivyo kufikia Machi 31, 2015 kiasi cha Dola za Marekani milioni 20.034 sawa na Sh53.270 bilioni zilikusanywa.
Amesema bima hiyo ni kwa ajili ya dharura za kiafya zinazohusiana na safari kwa wageni wanapokuwa hapa nchini, kupotea kwa mizigo ya wageni, kugharamia wageni wanapoondoshwa kwa lazima au ikitokea hatari yenye kulazimu uondoshwaji.
“Bima hii itakuwa na ukomo wa hadi siku 92 kwa mgeni ndani ya muda huo na haitahusisha raia wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).
Amesema utaratibu huo utakuwa wa ubia kati ya sekta binafsi na Serikali ikiwakilishwa na Shirika la Bima la Taifa, ambapo mgawanyo wa mapato utabainishwa ili kuweka ufanisi katika uendeshaji wake.
Akitahadharisha ongezeko la kodi kwa bidhaa kama petroli na dizeli, mchambuzi wa masuala ya bajeti, Felix Joseph amesema linaweza kusababisha mfumuko wa bei na hivyo kupunguza uwezo wa matumizi ya kaya.
“Mafuta haya yanaathiri karibu kila sekta kutoka usafirishaji hadi uzalishaji wa chakula. Athari zake zinaweza kuwa kubwa kwa wananchi wa kipato cha chini,” amesema Felix.
Mchambuzi wa masuala ya Serikali za mitaa, hasa bajeti za Halmashauri, Dk John Maleko ameonya, iwapo ongezeko la kodi halitazingatia hali ya soko, linaweza kuibua wimbi la magendo na biashara haramu ya bidhaa kama vile vileo na mafuta.
“Ushahidi wa nchi nyingi unaonyesha kuwa kodi kubwa isiyoendana na kipato huongeza uvujaji wa mapato badala ya kuyaongeza,” amesema Dk Maleko.
Akichambua vyanzo hivyo vipya vya mapato, Nicholaus Machunda amesisitiza kuwa fedha zitakazokusanywa lazima zisimamiwe kwa ufanisi na kwa uwazi mkubwa ili kuimarisha uaminifu kwa Serikali na wananchi.
Akizungumzia ongezeko la kodi kwenye bidhaa, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Mwanza, Patrick Masagati amesema hatua hiyo inaweza kuleta athari kwa wananchi wa kawaida ambao ni watumiaji wa bidhaa hizo na kusababisha matumizi yake kupungua na mzunguko wa fedha kuwa mdogo, hivyo malengo yaliyokusudiwa yasifikiwe.
Amesema Serikali imechukua hatua hiyo baada ya kudhani kwamba vinywaji kutoka ndani na nje ya nchi havina manufaa makubwa kwa wananchi kwakuwa mwananchi anaweza kuamua kuacha ama ukaendelea navyo.
“Katika maisha yetu ya kawaida pamoja na kazi tunazozifanya kutwa katika uzalishaji mali na kujenga Taifa lazima ukae mahali upumzike uburudike kwa namna moja au nyingine. Kuongeza hiyo kodi kunaweza kuongeza gharama za maisha kwa mwananchi wa kawaida,” amesema Masagati.
Amesema endapo wananchi watapunguza matumizi ya vinywaji hivyo fedha zilizokusudiwa kukusanywa katika sekta hiyo hazitopatikana.
“Kwa mfano tungekuwa na usimamizi mzuri katika rasilimali za Taifa kama migodi na madini kwa ujumla tusingewapandishia kodi wananchi. Wananchi waendelee kula starehe lakini wakati huo wakilipa kodi inayoendana na hali zetu za kiuchumi,” amesema Masagati
Nyongeza na Saada Amir, Samwel Mwanga na Damian Masyenene.
Crédito: Link de origem