Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chaumma, Hashimu Rungwe amewataka wanachama wapya 3,000 waliopokelewa kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuheshimu itikadi ya chama hicho inayoamini katika demokrasia ya kijamii.
Amesema wanachama hao wanapoingia kwenye mapambano ya kusaka dola, wanapaswa kujenga hoja madhubuti za kukabiliana na chama tawala cha Mapinduzi (CCM).
Rungwe ambaye ni mwanasheria kitaaluma, ameyasema hayo leo Jumatano Mei 21, 2025 kwenye hafla ya kuwapokea wanachama hao waliokihama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa nyakati tofauti kuanzia Mei7, 2025, hafla iliyofanyika Ukumbi wa Ubungo Plaza Jijini Dar es Salaam.
“Nawakaribisha twendeni tukakijenge chama ambacho kitashindana na kukabiliana na CCM kwa hoja madhubuti, na hakika kwa umoja wetu tutawashinda katika uchaguzi ulio huru na haki,” amesema Rungwe.
Amesema Chaumma tangu kuanzishwa kwake, falsafa zake ni kuujenga umoja wa kitaifa, uwazi na ukweli, kujenga jamii yenye mshikamano na Demokrasaia iliyo huru na haki kila wakati.

“Katika kipindi chote cha miaka 13 tangu kuasisiwa na kusajiliwa kwa chama chetu, tumeiishi misingi hiyo kwa vitendo na ndio maana imetuwezesha leo kufikia katika hatua hii ambayo imevutia watanzania wengine kujiunga nasi kwa maelfu kama mnavyowaona hapa ukumbini, nina imani walioko nje ya ukumbi huu ni wengi maradufu kuliko walioko hapa ndani,” amesema na kuongeza;
“Nawakaribisha wanachama wapya tukapambane kwa hoja ili tuweze kupata mabadiliko ambayo yatalipelekea taifa letu kufikia na kuishi misingi ya kuundwa kwa chama chetu,” amesema.
Amesema chama hicho hakihitaji kuona Taifa ambalo halina lishe, kwa sababu halitaweza kuendelea na ndio maana sera yao wanaamini ili kujenga nchi madhubuti na yenye watu imara ni lazima wapate lishe.

“Tunataka lishe itolewe tangu wakiwa watoto, huwezi kujenga taifa imara kama watu wake wanakuwa na shida ya utapiamlo, ndiyo maana halisi ya kauli mbiu yetu ya ‘Ubwabwa kwa wote.’ Karibuni tukajenge taifa lililoshiba na lenye afya njema,” amesema mwenyekiti huyo.
Amesema watu walioshiba wataweza kupiga kura kwa utashi wao kwa sababu hawatasubiri kupewa rushwa ya chakula ili wauze utu wao, “twendeni tukajenge taifa la ndoto zetu.”
Amesema leo Chaumma inaandika historia mpya tangu kilipopata usajili wa kudumu mwaka 2012.
Amesema ni takribani miaka 13 sasa wameendelea na safari ya kujenga chama chao hatua kwa hatua huku wakipitia mapito mbalimbali na hatimaye wameifikia siku muhimu ya kuandika historia kwa Tanzania nan je ya mipaka yake.

Rungwe amesema bado chama hicho kinakumbuka dhamira ya waasisi wa Taifa la Tanzania waliokuwa na ndoto ya kutaka kuona jamii ambayo waliijenga ikiishi pamoja.
“Walikusudia kujenga jamii ambayo pamoja na tofauti, lakini yenye usawa katika mahitaji ya msingi na ya lazima. Walikusudia kujenga jamii ambayo watu watashindana katika ziada, lakini wote wanakuwa sawa katika kupata mahitaji ya msingi, heshima na utu wao,” amesema Rungwe.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Chaumma Bara, Devotha Minja amesema malengo dhabiti ya chama hicho katika kuwakomboa watanzania kupitia uchaguzi badala ya kususia ni sababu iliyomsukuma kujiunga nacho.
“Nilikotoka nilikutana na misukosuko na dhoruba nyingi, ilinipasa nitulie na kufikiria ni wapi naweza kwenda na kutuliza akili ya kuwatumikia watanzania, lakini naamini kujiunga kwangu na Chaumma ni jukwaa sahihi linaloweza kunipa utulivu,” amesema Devotha.
Amesema chama hicho kina mipango ya kuchukua dola katika uchaguzi ulio huru na haki na kujenga demokrasia nzuri kwa wote na kuinua maisha ya wanawake.
“Kujenga jamii isiyokuwa na ubaguzi wa rangi au kipato bila kujali hadhi zao utajiri au maskini, niko hapa nahitaji kujenga taifa kwa misingi hiyo kwa kuwa waliopo madarakani wameshindwa kuwanufaisha watanzani,” amesema.
Devotha amesema wakati anatafakari kujiunga na Chaumma alisoma Katiba na kubaini wanamtanguliza zaidi Mungu huku akiwataka wanachama hao kwenda kuwavuta wengine kujiunga nacho.

“Niwakaribishe wanawake wote kujiunga na chama hiki kilijichojidhatiti kupigania ndoto ya wanawake ndani ya uwanja, kwa sababu hatuwezi kuchukua kombe kama hatutapeleka timu uwanjani, twendeni katika uwanja wa mapambano,” amesema Devotha.
Kulingana na Devotha, Tanzania hakuna vita, jambo la msingi ni kuingia uwanjani kwenda kupambana kwa ajili ya uchaguzi ili kutimiza azma ya kuwatumikia watanzania.
Crédito: Link de origem