Wabunifu wa teknolojia duniani wameendelea kuvumbua njia mpya za kuua mbu, matibabu na chanjo, ikiwa ni njia ya kutokomeza ugonjwa wa malaria, ambao ni tishio kwa kusababisha vifo vya maelfu ya watu duniani.
Teknolojia mbalimbali, ikiwemo ya kubadilisha vinasaba (DNA) itambulikayo kwa jina la ‘Genetic biocontrol’ zina uwezo wa kuifanya malaria kuwa sehemu ya historia.
Teknolojia hii inahusisha kubadilisha vinasaba vya mbu, kwa kuongeza jeni ambazo hupunguza uwezo wao wa kuishi na kuzaana, na hivyo kupunguza idadi yao.
Hupunguza uwezo wa mbu kusambaza vimelea vya malaria, kwa kuzuia ukuaji wa vimelea hivyo ndani ya miili ya mbu. Udhibiti wa kijeni unaweza kufanywa kwa kuwazuia kuzaana, hali inayosababisha kupungua kwa idadi yao.
Aidha, mbu wanaweza kubadilishwa kijeni ili wasiweze kulea au kukuza vimelea vya malaria, jambo linalopunguza maambukizi.
Kwa kutumia mbinu hizi za kisasa, malaria inaweza kudhibitiwa kwa njia ya kudumu na endelevu, hasa inapojumuishwa na mikakati mingine ya kinga na tiba.
Pia inawezekana mbu kubadilishwa jeni kwa kupitia teknolojia ya Gene Drive inayosimamiwa na mradi wa Transmission Zero.
Katika mradi huo, ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Imperial London na taasisi kadhaa nchini Tanzania, umetengeneza mbu waliorekebishwa kijenetiki wasio na uwezo wa kueneza vimelea vya malaria.
Mradi huo unalenga kutokomeza malaria kwa kutumia udhibiti wa kijenetiki wa mbu, hasa makundi matatu ya mbu aina ya ‘anopheles’ wanaohusika na zaidi ya asilimia 85 ya maambukizi nchini Tanzania.
Timu ya watafiti kutoka Chuo cha Imperial London kwa kushirikiana na Taasisi ya Afya ya Ifakara na Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Tiba nchini Tanzania (Nimr), wametengeneza teknolojia ya vinasaba ambayo inamfanya mbu ashindwe kusambaza vimelea vya malaria.
Faida ya teknolojia hii inaweza kupunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa malaria katika nchi zenye viwango vya juu vya maambukizi. Inaokoa maisha ya maelfu ya watu kila mwaka, hasa watoto chini ya miaka mitano.
“Teknolojia yetu ni ya usawa, inaleta matumaini katika vita dhidi ya malaria na haina vizingiti vya kiuchumi au kijamii,” anasema Profesa George Christophides wa chuo hicho.
Tanzania sasa ina maabara ya usalama wa kiwango cha tatu (biosafety level 3) na kituo cha uzalishaji wa mbu waliobadilishwa kijeni.
Mbu wa kwanza waliobadilishwa kijeni wamezalishwa Afrika kwa mara ya kwanza na wanasayansi wa Kiafrika.
“Tulikubaliana tangu mwanzo kuwa ni lazima kuwajengea uwezo wanasayansi wa ndani na kuhakikisha ushirikiano wa Serikali na jamii,” anasema Dk Dickson Lwetoijera kutoka Taasisi ya Afya ya Ifakara.
Pia tayari kuna chanjo mpya za kisasa dhidi ya malaria zilizoidhinishwa na WHO ambazo ni RTS,S/AS01 na R21/Matrix-M. Chanjo hizi zimeonyesha mafanikio katika kupunguza wagonjwa na vifo miongoni mwa watoto katika maeneo yaliyo katika hatari kubwa.
Chanjo zote mbili zimeonyesha kuwa salama na zinafaa katika kuzuia malaria kwa watoto na zinatarajiwa kuwa na athari kubwa kwa afya ya umma.
RTS,S imeonyesha katika utekelezaji wa majaribio kupunguza kwa kiasi kikubwa ugonjwa wa malaria na vifo kwa watoto wadogo.
Kutokana na kufanana kwa chanjo hizi mbili za malaria, inawezekana kuwa R21 pia itakuwa na athari chanya.
Maelfu kwa maelfu ya maisha ya watoto wadogo yanaweza kuokolewa kila mwaka, kwa utekelezaji mpana wa chanjo hizi za malaria.
Chanjo zote mbili huzuia takriban asilimia 75 ya matukio ya malaria, ikiwa zitatolewa kwa msimu katika maeneo yenye maambukizi makubwa ambapo kinga ya malaria ya msimu hutolewa.
Hata hivyo, hakuna ushahidi hadi sasa unaoonyesha chanjo moja inafanya kazi vizuri zaidi kuliko nyingine.
Chanjo ya RTS,S ilipata ithibati ya ubora kutoka WHO Julai 2022, huku R21 ikipata ithibati Desemba 2023. Ithibati ya ubora kutoka WHO inahakikisha usalama na ubora wa chanjo.
Kinga mwili za Monoclonal
Kinga mwili hizi hutengenezwa maabara na kulengwa moja kwa moja dhidi ya vimelea vya malaria: mtu anapochomwa sindano yake, hutoa ulinzi wa muda mfupi lakini wenye nguvu.
Zinaweza kutumika kwa makundi maalumu kama wanawake wajawazito, watu waliopona magonjwa mengine, au wasafiri wa maeneo yenye malaria.
Pia katika teknolojia hizo kuna vyandarua vyenye mchanganyiko wa dawa zaidi ya moja, kukabiliana na usugu wa dawa za awali, pamoja na viua-viwavi vya kunyunyizia ukutani na mitego yenye sumu.
Wavumbuzi wa kampuni ya Sygenta wamezindua dawa mpya ya kuua wadudu ambayo inashughulikia mbu sugu zaidi, wasioathirika na matibabu.
Syngenta imetangaza kuwa dawa yake mpya ya kuua wadudu ya Sovrenta® imepokea ithibati ya ubora kutoka WHO na kufungua njia ya matumizi yake katika nchi zilizoathiriwa na malaria.
Sovrenta hufanya kazi kwa kulenga mfumo wa neva wa mbu, ikizuia misuli inayofanya wadudu kupumzika, kulemaza na hatimaye kufa.
Sovrenta inatokana na teknolojia ya kisasa ya PLINAZOLIN® ya Syngenta ambayo ina mfumo mpya wa utendaji, kuhakikisha udhibiti mzuri wa mbu hata pale ambapo idadi ya wadudu inazidi kuwa sugu kwa dawa za zamani za kuua wadudu.
Crédito: Link de origem