top-news-1350×250-leaderboard-1

Hivi ni Askofu Gwajima huyuhuyu ninayemfahamu au…

Namsikiliza Josephat Gwajima, mbunge wa Kawe na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima. Unatafakari hoja yake kuhusu vitendo vya utekaji.

Unamwelewa, unaona anayo hoja. Matukio ya kuchukuliwa na watu kupotea, ni mabaya, ni aibu kwa nchi.

Nataka kumpongeza, nakumbuka ni Gwajima huyohuyo aliyewapanga wananchi wa Kawe, kuwa endapo wangemchagua awe mbunge wao, angewapeleka Greater Birmingham, jimbo la Alabama, Marekani. Na wangeishi kwenye nchi hiyo.

Gwajima aliahidi kuwa wakazi wa Birmingham, wangehamia Kawe. Miaka mitano inakatika. Hakuna Mzungu anayeonekana Kawe Ukwamani wala Kawe Maringo, ambaye ametokea Birmingham. Hakuna mwana-Kawe aliyehamia Birmingham kwa mpango wa Gwajima.

Naikumbuka ahadi ya Gwajima, kushusha Kawe meli za uvuvi kutoka Japan. Eti, alikuwa na makubaliano na watu wa Japan.

Miaka mitano inakatika, hakuna meli, boti wala mtumbwi kutoka Japan. Hili pia Gwajima inawezekana bado wana-Kawe wanalisubiri litimie.

Ni Gwajima aliyeahidi kumrejesha akiwa hai aliyekuwa mbunge wa Viti Maalum (CCM), Amina Chifupa.

Gwajima huyohuyo akaahidi kumfufua Waziri Mkuu pekee aliyefariki dunia akiwa ofisini hadi sasa, Edward Sokoine. Inakaribia miongo miwili, hakuna ahadi iliyotimia.

Unakuja kwenye tafakuri; je, hoja ya Gwajima kuhusu watu wanaotekwa, ni mwanzo wa mbunge huyo kuyaona masuala na kuusema ukweli kama ulivyo, au ni gia mpya ambayo ameona aitumie kujenga uhusika wa kisiasa, kipindi hiki taifa linapojielekeza kwenye uchaguzi?

Uchaguzi una mambo mengi. Wanasiasa hujisahau wanapochaguliwa. Siku 365 ambazo ndizo hukamilisha mwaka, unaweza kuziona nyingi, lakini kama una madeni ya kulipa, ni chache. Mbunge ni mdaiwa wa wananchi jimboni kwake.

Yupo mbunge aliahidi pepo kwa wapigakura. Aliwaambia wananchi kuwa yeye akiwa mbunge, akina mama wajawazito wangepelekwa hospitali na helikopta, ambayo ingekuwa ambulance. Wanafunzi wa sayansi wangesoma elimu kwa vitendo (practical), Silicon Valley, California, Marekani. Aliahidi vipato vya moja kwa moja kwa wanaume ili wasishindwe kuhudumia familia zao.

Alipokuwa akitoa ahadi hizo, mawazoni alijua asingetekeleza, ila alijisemea: “Nawadanganya, wakinichagua, nakuwa mbunge kwa muhula mmoja, halafu naacha.” Kweli alichaguliwa. Akaongoza kiujanja-ujanja. Muhula ulipokaribia ukingoni, akagundua ubunge ni mtamu, kwa hiyo alitaka kuendelea.

Angefanya nini na hakutimiza ahadi yoyote? Zaidi, kila ahadi ilikuwa hadaa kwa sababu alijua fika hakuna ambayo angeitimiza. Sasa, ili kucheza na hisia za wapigakura, akaanza mchezo wa kupandisha majini na kuishika uchawi serikali kwamba inaliroga jimbo lake na kumroga yeye mwenyewe.

Swali linakuja kwa Gwajima, je, hoja yake ya kudai majibu ya upotevu wa watu na kuuawa, ni kukumbuka shuka wakati kumekucha, au ndiyo mwanzo wa kuamka kwake usingizini na kunena mambo ya msingi kuhusu nchi? Maana kadhia ya utekaji, mauaji na upotevu wa watu ni matendo yenye kutimiza muongo mzima na alikuwa kimya.

Nyakati watu wanahoji kupotea kwa kada wa Chadema, Ben Sanane, mwandishi wa habari, Azory Gwanda, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Simon Kanguye, kuuawa kwa Mkurugenzi wa Wizara ya Fedha, aliyekuwa anashughulikia miradi ya Umoja wa Ulaya (EU), Leopard Lwajwabe, mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini, Gwajima alikuwa wapi?

Zile nyakati za mnyororo wa vifo Mkuranga, Kibiti na Rufiji, maiti zikiokotwa mfululizo fukwe za Bahari ya Hindi, na kingo za Mto Ruvu, Gwajima alikuwa wapi hata kushindwa kuguswa na kutoa neno? Haina maana sasa hivi anakosea kuhoji, yupo sahihi, lakini je, sauti yake inatoka moyoni au anasukumwa na agenda tofauti? Mwangwi wa jimboni Kawe hauna ushawishi, ndiyo maana anaanza kushika watu uchawi?

Hizi ni nyakati zenye kuhitaji umakini mkubwa. Unaweza kuogelea agenda ya mtu kumbe mwenzako anatafuta uhusika wa kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025. Je, mbona Gwajima hakuwahi kuguswa popote na mashambulizi ya risasi aliyofanyiwa Tundu Lissu, mchana kweupe, Dodoma, Septemba 7, 2017?

Mwendelezo wa matukio ya utekaji na mauji, kutoka utawala mpaka utawala, unahitaji namna tofauti ya kufikiri. Nadharia kuu inahama kutoka kumnyooshea kidole mtu mmoja hadi wito wa mshikamano wa kitaifa kuhusu njia bora ya kulikabili tatizo.

Tangu kupotea kwa Saanane, Kanguye na Azory, hadi Deusdedith Soka, Jacob Mlay, Frank Mbise, Ali Kibao na Mdude Nyagali, sura ya dola imebadilika. Mkuu wa Jeshi la Polisi wakati Saanane anatekwa alikuwa Ernest Mangu.

Hata hivyo, matukio yaliendelea hata alipoingia ofisini Simon Sirro na sasa yupo Camillus Wambura. Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (DGIS), alikuwepo Modestus Kipilimba, akafuata Diwani Athuman, kisha Said Masoro, akaja Ali Siwa na sasa yupo Suleiman Mombo. Je, mbona matukio hayakomi?

Inahitaji fikra ambazo zinavuka kiwango cha kawaida cha kufikiri, na kutengeneza nadharia nyingi ili kuyafikia majibu halisi. Je, watekaji, wapoteza watu, wauaji na wapigaji wa risasi, ni kikundi ambacho kimeshindikana au kila baada ya muda vinazaliwa vikundi vipya vyenye kutekeleza uhalifu huo wa kibinadamu?

Je, mifumo ya kiusalama ya nchi inawatambua na kuwaacha waendelee, au ni watu wasioguswa? Vipi ikiwa hawajulikani kabisa? Kwa nini kusiwe na mshikamano wa kitaifa wa kuhakikisha kunakuwa na msako wa nguvu mpaka ufumbuzi upatikane na wahusika halisi wakamatwe?

Historia ya matukio ya utekaji, upotevu wa watu na mauaji, inakataza mashambulizi na kushutumiana. Haishauri kushikana uchawi na kunyoosheana vidole. Inataka ushirikiano. Hali ni mbaya. Na haitaisha kama utaendelea utaratibu uleule wa kumtazama mtu mmoja kama ndiye sababu, halafu huyohuyo awe suluhisho.

Alikuwepo Dk John Magufuli, sasa dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. Bila kukifikia kiini halisi, matukio yataendelea hata baada ya Dk Samia. Na kwa kasumba ileile, atalaumiwa rais atakayekuwa madarakani kipindi hicho.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.