Dar es Salaam. Ni vizuri kutaka kuwa peke yako nyakati nyingine, lakini inapofikia kuwa hatua hiyo ndio mtindo wa maisha yako ya kila siku ni hatari. Kujihisi mpweke ni kitu kibaya kiafya kwani huchangia kushusha kinga za mwili.
Akieleza tafsiri ya upweke, Mkurugenzi wa kituo cha kushughulikia upweke katika Chuo Kikuu cha Sheffield Hallam huko Uingereza, Dk Andrea Wickfield anasema: “Upweke ni hali ya huzuni na hisia ya kutoridhika inayotokana na kujihisi uko peke yako kinyume na vile unavyohitaji.
Wataalamu wengi wanakubali kwamba upweke hutokea unapohisi hali ya uhusiano wako binafsi na watu wengine iko chini kuliko vile unavyotamani iwe.
Mtaalamu wa saikolojia tiba na afya ya akili kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Isaac Lema anasema upweke ni tatizo linalopaswa kuepukwa, japo anaongeza kuwa kuwa peke yako si tatizo.

Dk Lema anasema mtu mpweke hata ukimweka katikati ya Uwanja wa Benjamin Mkapa, bado atajiona yuko katika hali ya upweke kwa sababu amekosa mjumuiko na watu wengine hata kama kuna watu wanaomzunguka.
Anasema upweke ni zaidi ya kuzungukwa na watu, kwahiyo ni tatizo… “Hakuna mtu anatamani kuwa mpweke kila mtu ameumbwa ajaliwe, apendwe, lakini unapohisi kwamba hakuna anayekujali na umeumbwa katika hali ya upweke, ina maana tayari ni tatizo la kisaikolojia, lakini si dalili ya ugonjwa wa akili.”
Dk Lema anasema wenye upweke huwa wanapewa mbinu za kuwasaidia kutoka kwenye hali hiyo, katika kuyaangalia maisha yake, kwakuwa wengine ni kutokana na ule mtazamo alionao kuhusiana na watu wanaomzunguka.
Anasema wakati mwingine wanawashauri kujitofautisha na matatizo na kuwatofautisha wengine na matatizo ili ile hali ya upweke iweze kuondoka katika maisha yake.
Kwa mujibu wa Dk Lema, hali hiyo ikiendelea mara nyingi huwa inaleta sononeko, baada ya hapo mtu hukabiliwa na msongo, hali ambayo humfanya mhusika kuwa na changamoto ya kisaikolojia na sio ya afya ya akili.
“Inamuweka kwenye uhatarishi kwakuwa ikitokea hali ya msongo, atakuwa na changamoto ya kukabiliana na msongo kuliko yule ambaye hayupo kwenye hali ya upweke, sababu tunapopata usaidizi na tunapohisi tu miongoni mwa watu, thamani yetu inakua ni njia nzuri ya kuweza kukabiliana na upweke,” anasema Dk Lema.
Mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Ali Mzige anasema upweke unaharibu akili za watu na ndio maana watu wanaowekwa kizuizini na kutopewa mtu wa kuzungumza naye, mwishowe wanavurugikiwa akili.
Anasema upweke ni kitu ambacho hakistahili kuwepo… “Ukiwa mpweke unapoteza kinga zako kwa sababu mwili ukifanya kazi vizuri, unapata kinga nzuri. Mfano mwanaume kama hakufanya kazi inavyotakiwa ni rahisi kupata kiharusi.
“Kwa sababu ukiwa unafanya kazi ile homoni ya kiume ‘testosterone’ inakusaidia wewe kukuzia usipate kiharusi, ndiyo maana unaona wachezaji mpira wazuri, wakimbiaji na wengine hawawezi kupata kiharusi kwa sababu wanatengeneza ile homoni…” anafafanua Na kuongeza:
“Homoni za kiume zikiwa chache anaweza kupata kiharusi, sasa yule mwenye upweke atakuwa fikra zake si nzuri, atakosa mtu wa kuzungumza naye na mwingine anaweza hata kujiua na kama wewe mpweke hufanyi chochote umelala tu, umekaa tu unaweza kunenepa.”
Dk Mzige anasema upweke unaathiri ubongo, fikra sambamba na kudhuru kinga ya mwili.
“Ndiyo maana mtu akifiwa wanakwenda kumpa pole, akiwa mpweke akifiwa na mume au mke upweke ule ukizidi, baadaye unamnyong’onyeza, ananyongea naye mwisho anapata matatizo ya kiafya, kisaikojiloa ya kutopata usingizi, kinga zinashuka, kitu ambacho si kizuri,” anasema.
Kwa mujibu wa Dk Mzige ni muhimu kwa watu ambao umri umeenda kutafuta watu wa kukaa nao pamoja kuondoa upweke.
“Watu wajaribu kukaa na makundi, ndugu, marafiki hasa watu wazima. Ndiyo maana wanaambiwa wajukuu wakija ucheke nao na ufurahi nao unajua kucheka nako kunaongeza maisha,” anaeleza.
Utafiti wa hivi karibuni wa Chuo Kikuu cha Cambridge umegundua, hisia za upweke zinahusishwa na hatari kubwa ya ugonjwa wa moyo. Pia huongeza hatari ya kiharusi na kisukari cha aina ya pili.
Dk Wigfield anasema wanasayansi wamepata ushahidi kwamba upweke husababisha shida ya akili, unyogovu na wasiwasi na huongeza hatari ya kifo.
Sababu hasa ya uhusiano huu bado haijulikani, lakini madaktari wanakisia upweke unaweza kusababisha msongo wa mawazo wa ndani. Upweke wa muda mrefu unaunyima ubongo vichocheo vinavyochochea michakato ya fikra na hilo linaweza kuzidisha matatizo ya afya ya akili.
Shirika la Afya Duniani (WHO) linasema mtu mmoja mzima kati ya watu wazima wanne ametengwa na jamii, na makadirio yanasema kati ya asilimia tano na 15 ya vijana hukumbwa na upweke.
Makundi fulani ya watu yako katika hatari zaidi ya kukumbwa na upweke, ikiwa ni pamoja na wahamiaji, jamii za wachache, wakimbizi, walezi na watu wenye magonjwa sugu.
Utafiti unasema, kujitolea kufanya shughuli za kijamii ni njia nzuri ya kuzuia upweke. Utafiti uliofanywa kwa watu 375 huko Hong Kong, uligundua kuwa kutumia muda wako wa ziada kufanya kazi za hisani, kunasaidia kupunguza hisia za upweke hasa miongoni mwa wazee.
Katika nchi za Australia na Uholanzi, serikali zinawekeza katika jumuiya za makazi ya kijamii, ambapo wazee na vijana wanahimizwa kujumuika na kushiriki katika shughuli za pamoja, kama vile katika vituo vya jumuiya au maeneo ya umma.
Madaktari nchini Uingereza wanaposhuku wagonjwa wao wanapitia upweke, huwaelekeza shughuli za kijamii ambazo zinaweza kuwasaidia kuwaunganisha watu.
Unaweza kuwa mpweke kidogo
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Reading nchini Uingereza, wamegundua kuwa kujitenga mara moja moja kuna athari chanya na hasi katika maisha ya watu.

Utafiti huo ulifuata watu wazima 178 kwa muda wa siku 21, ambao walijaza dodoso na kuweka kumbukumbu ili kupima viwango vyao vya msongo wa mawazo, kuridhika na maisha, hisia za uhuru na upweke.
Matokeo yalionyesha kuwa kadiri watu walivyokaa peke yao kwa muda mrefu, ndivyo walivyokuwa na msongo wa mawazo kidogo na walijisikia huru. Ni dalili za amani ya ndani inayotokana na kujitenga.
Hata hivyo, baadhi ya washiriki waliripoti kwamba siku walizokaa muda mrefu wakiwa peke yao, walihisi kukosa furaha na kutoridhika, na hizo ni dalili za upweke.
Utafiti mwingine unathibitisha kujitenga kunaweza kuwapa watu nafasi ya kudhibiti hisia zao, kujisikia huru na hali ya kujitegemea. Kujitenga ni njia muhimu ya kushughulika na viwango vya juu vya msongo wa mawazo au kushughulika na siku yenye shughuli nyingi.
Crédito: Link de origem