Hayo hapo ni maneno yaliyozoeleka kusikika kuonyesha maudhi na kumuumiza mama ambaye hakujaliwa kuzaa.
Japo si jamii zote hufanya hivi, kuna ushahidi kuwa wanawake wagumba wanapata matatizo mengi kuliko wanaume, kutokana na mfumo dume unaotawala karibu dunia yote mbali na ujinga na ukale.
Mengi hutoka kwa ndugu na maadui wa mhusika. Je, kuna mtu asiyependa kuzaa duniani? Je, kuna mtu anayechangia, kwa hiari au mipango yake kutozaa au kuwa mgumba?
Je, hali inakuwaje tatizo linapokuwa ni la muoaji na si muolewa? Ni kwanini anayeshutumiwa ni mwanamke pekee hata bila ushahidi wa kisayansi au stahiki zaidi ya ujinga na unyanyasaji wa kijinsia?
Karibu tudurusu kadhia hii ambayo imeumiza, kutaliki, hata kuua wengi.
Tatizo la kutopata watoto lipo, na ni kubwa. Kwanza, kama halijakupata, wapo wanaokuhusu wawe marafiki hata ndugu zako wanaohangaishwa nalo, na linajadilika na kutatulika.
Hivyo, si vibaya kulijadili. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO, 2023), katika kila watu sita, mmoja ni mgumba duniania ambao ni asilimia 17. 5 ya wakazi wote wa duniani.
Shirika la habari la Al Jazeera (2024), limesema hadi kufikia mwaka 2100, kutakuwa na upungufu wa idadi ya watu katika nchi 198 kati ya 204 za dunia.
Hivyo, kwa mujibu wa taasisi ya Health Metrics and Evaluation (IHME) ya Chuo Kikuu cha Washington iliyokaririwa na Al Jazeera, ni Somalia, Tonga, Niger, Chad, Samoa na Tajikistan zitakazoweza kuepuka tatizo hili.
Takwimu hapo juu zinaonyesha kuwa hili tatizo si dogo wala la nchi au mtu mmoja. Ni la kidunia, hivyo, lazima kulijua na kulitafutia suluhisho.
Lengo kuu la ndoa, kuliko yote, ni kuendeleza kizazi. Kwani, bila kizazi, wanadamu au viumbe watatoweka.
Kwa vile viumbe vyote vimepewa uwezo wa ‘kuumba’ kupitia njia hii, kuna wakati wahusika husahau kuwa bado wapo waliojaliwa kutozaa.
Hali hii huitwa ugumba kutokana na mwanamke kukosa uwezo wa kushika mimba, hivyo, kutoweza kuzaa. Japo tatizo hili linaonekana kuwa la kijinsi ambapo waathirika wengi ni wanawake, pia wapo wanaume wasio na uwezo wa kutungisha mimba ambao hatujui Kiswahili chake.
Tunapodurusu hali hii, tujiulize swali la msingi sana, je, nani asiyetaka kuzaa? Japo, siku hizi, kuna watu wenye uwezo wa kubeba au kubebesha mimba wanaoamua kutozaa kwa sababu wajuazo, tatizo la kutopata watoto limekuwapo kwa miaka mingi. Tunaliona kwenye vitabu vya dini na hata kwenye maeneo yetu kila uchao. Tujiulize maswali yafuatayo:
Je, ni tatizo ni la kujitakia? Je, tatizo ni baba au mama? Kwanini hakuna wanaume wanaojaza vyoo?
Tutadurusu baadhi ya mambo ya kufanya kupambana na tatizo la kutozaa. Mosi, pimeni afya zenu na kujua tatizo ni nini na liko kwa nani ili mlitatue.
Pia, shirikianeni katika hili hasa ikizingatiwa kuwa mlipofunga ndoa, mliahidiana kushirikiana katika dhiki na raha.
Pili, kwanini kuzaa iwe raha pekee mnayoitafuta na kuikubali wakati kunaweza kutokea adha au dhiki ya kutoweza kupata watoto? Ni bora wanandoa wakashirikiana kulitatua tatizo hili.
Tatu, mnapohangaikia tatizo hili, muwe na subira na imani huku mkizingatia, kukubali, na kutambua kuwa hili tatizo siyo la kujitakia na linaweza kumpata yeyote.
Nne, fuateni au tumieni njia zinazokubalika kisayansi badala ya imani na mahitimisho ya haraka.
Tunajua waathirika wana imani tofauti, hata hivyo, si vizuri kutegemea imani au miujiza zaidi ya njia zinazokubalika kisayansi.
Tunasema haya kutokana na kujua au kusikia namna wanawake wengi walivyoharibikiwa, kuteseka, hata kuvunja ndoa zao kwa kutumia njia zisizo za kisayansi kama vile maombi, waganga wa kienyeji ambao wengi ni matapeli na waharibifu tu.
Tano, tuonye. Waganga wengi wa kienyeji wameongezeka na wateja wao wakubwa ni kinamama hasa wasio na uwezo wa kuzaa au walio na changamoto kwenye ndoa zao.
Hivyo, waathirika wanapaswa kuwa macho wasiongeze matatizo mengine wakiamini na kudhani wanatatua tatizo.
Sita, jamii ielimishwe kuwa tatizo hili siyo la kurogwa, kulaaniwa, au la baadhi ya watu. Hivyo, chuki, kejeli, na lugha za kujaza choo ziepukwe. Kwani, aliyewanyima waathirika ndiye aliyekupa wewe unayewanyanyapaa.
Kimsingi, jamii itafute namna ya kuwasaidia wasioweza kupata watoto kwa kuwapatia ujuzi na ulinzi kijamii.
Saba, jamii na watu wanaowazuguka waathirika zielimishwe juu ya kuwathamini na kuelewa kutozaa siyo tatizo la wanawake hawa.
Crédito: Link de origem