top-news-1350×250-leaderboard-1

Fikiria, itakuaje wote tukiacha kutumia pesa taslimu

Fikiria siku moja ambapo hakuna Mtanzania atakayehitaji tena kutumia pesa taslimu. Kuanzia muuza chipsi wa Buguruni hadi kwa wavuvi wa Mafia na mwambao wa Tanga, kila mtu anapokea na kufanya malipo kwa njia ya kidijitali.

Watoto watafunguliwa akaunti za akiba kwa kutumia tu namba ya cheti cha kuzaliwa kupitia simu ya mkononi, bila kwenda benki. Wakulima wa alizeti Singida watapokea bima ya mazao na mikopo papo hapo kupitia programu za simu, huku taarifa zao za mavuno, mapato na matumizi zikiwa zimehifadhiwa kidijitali.

Hili ni kama ndoto, lakini ni ndoto ambayo tunaendelea kuifanikisha kupitia elimu ya fedha, uvumbuzi wa kiteknolojia, na juhudi za mashirika ya kifedha na serikali. Lakini siku hiyo itakapowadia ambapo kila mtu atakuwa ameunganishwa rasmi na mifumo ya kifedha hali itakuwaje?

Pengine huduma kama TASAF zitafika moja kwa moja kwenye kaya masikini. Ufanisi wa miradi kama hiyo unaweza kuongezeka maradufu. Mama muuza mboga ataweza kuweka akiba salama bila kuficha pesa chini ya mkeka. Elimu ya kifedha itakuwa imeenea kiasi cha kumuwezesha wengi kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.

Dereva wa bodaboda Morogoro ataweza kupata mkopo wa haraka kutengeneza pikipiki yake bila hitaji la dhamana. Kwa sababu taarifa zake, historia ya miamala, na mwenendo wa biashara yake zipo wazi kidijitali. Kila Mtanzania atakuwa na rekodi ya kifedha, jambo litakalowezesha upangaji bora wa maisha na biashara.

Lakini ndoto hii haikosi changamoto.

Ujumuishi wa kifedha unamaanisha kuwa taarifa za watu binafsi na biashara zitakuwa zinapatikana rasmi. Katika jamii yetu ambapo shughuli nyingi bado zinafanyika kwenye sekta isiyo rasmi, inaweza kutia hofu. Mfano, muuzaji wa mkaa kule Njombe ambaye hajawahi kulipa kodi, anaweza kuogopa kwamba taarifa zake za kifedha zikitambulika, ataanza kufuatwa na mamlaka za kodi.

Vivyo hivyo, uraibu wa kukopa kupitia simu nao unaibua changamoto mpya. Programu za mikopo mtandaoni sasa zinatoa mikopo kwa urahisi sana, lakini urahisi huo unaweza kuwaingiza watu kwenye mzunguko wa madeni wa kila siku.

Wapo wanaokopa ili kulipa mkopo mwingine. Dalili zake tunaziona: unapomtumia mtu pesa kwa simu, si ajabu kusikia: “Usitume kwa namba hiyo,” akimaanisha namba hiyo inadaiwa, na pesa yoyote itakayowekwa itakatwa papo hapo.

Kwa zama hizo zijazo, sheria kuhusu matumizi ya taarifa binafsi zitahitaji kuwa thabiti zaidi. Wamiliki wa data kama benki, mitandao ya simu na taasisi za fedha, watakuwa na jukumu kubwa la kuhakikisha usalama, matumizi sahihi, na uwazi wa taarifa hizo. Bila hivyo, mazingira haya mapya yanaweza kuwa mwiba kwa watumiaji badala ya kuwa faraja.

Vikundi vya jadi vya akiba kama VICOBA na Upatu vina mchango mkubwa katika maisha ya Watanzania, hasa katika jamii za kipato cha chini. Hata hivyo, navyo havitaepuka mabadiliko ya nyakati. Kadri huduma za kifedha za kidijitali zinavyozidi kuenea, kuna uwezekano kuwa baadhi ya wanachama watahamia kwenye mifumo ya kisasa, hali ambayo inaweza kupunguza ushawishi wake vikaanza kuchukua sura na tabia mpya kabisa.

Swali la kujiuliza ni je, mifumo rasmi ya kifedha itaweza kuwapa watu hisia zilezile za kuaminiana na mshikamano walizozoea katika kikundi cha akiba cha Jirani? wakati utatujibu.

Lengo si kusema kuwa ujumuishi wa kifedha ni jambo baya—la hasha. Ujumuishi huu ni nyenzo yenye nguvu ya kuleta maendeleo na haki ya kiuchumi kwa wote. Lakini baada ya kila mtu kuunganishwa, changamoto kubwa itakuwa kuhakikisha kuwa ujumuishi huo hautageuka kuwa mtego wa kumnyonya mtumiaji au fimbo ya kumchapa mnyonge.

Mazingira ya usimamizi wa sekta ya kifedha ni lazima yaende sambamba na kasi ya mabadiliko ya kidijitali, huku yakihakikisha kwamba haki, heshima, na usalama wa mtumiaji vinalindwa.

Tanzania ya baadaye inaweza kuwa jamii isiyotumia pesa taslimu, inayotegemea data na teknolojia. Hata hivyo, huduma za kifedha hazipaswi kubuniwa kwa lengo la kupata wateja tu na sheria hazipaswi kulinda miamala tu, bali pia mambo muhimu katika maisha ya wale wanaofanya miamala hiyo.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.