Arusha. Mahakama ya Rufani imebatilisha mwenendo wa kesi na kufuta hukumu ya adhabu ya kunyongwa hadi kufa waliyokuwa wamehukumiwa wakazi watatu wa Bukoba mkoani Kagera, baada ya kubaini kasoro za kisheria katika mwenendo wa kesi hiyo.
Badala yake Mahakama hiyo imeamuru kesi hiyo isikilizwe upya mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu.
Mahakama imefikia uamuzi huo kutokana na rufaa waliyoikata warufani Renatus Misagalo, Mwendapole Andrea na Kalenzi Ruhinda.
Hata hivyo, imeamuru warufani hao kusalia kizuizini wakisubiri kesi yao kusikilizwa upya.
Awali Renatus na wenzake walihukumiwa adhabu hiyo baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la mauaji ya jirani yao, David Mbilahisha.
Katika kesi hiyo ya jinai, warufani hao walidaiwa kutenda kosa hilo katika Kijiji cha Rulenge ndani ya Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, ambapo Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba iliyosikiliza kesi hiyo iliwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Walikata rufaa iliyosikilizwa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani walioketi Bukoba ambao ni Stella Mugasha, Abraham Mwampashi na Paul Ngwembe.
Hukumu hiyo ya rufaa ya ilitolewa Machi 13, 2025 na majaji hao ambapo walibainisha kuwapo mapungufu ya kisheria yaliyojitokeza wakati kesi inasikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba.
Jaji Mwampashi amesema uhamishaji wa kesi hiyo ulikuwa na dosari na hakimu aliyeisikiliza hakuwa na mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo ya mauaji.
“Kwa hali hiyo, mwenendo mzima wa kesi ikijumuisha hukumu ya matokeo na amri ni ubatili,” amesema Jaji Mwampashi.
Kuhusu nini kinapaswa kufanyika baada ya kufuta mwenendo na hukumu hiyo, suala linalojitokeza mbele yao ni iwapo mazingira ya kesi yanaruhusu kusikilizwa upya au la.
“Tumezingatia mazingira ya kesi kwa ujumla, pia tunakumbuka kile kilichosemwa na Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki katika kesi ya Fatehali Manji dhidi ya Jamhuri, kwamba kusikilizwa upya kutaamriwa tu wakati kesi ya awali ilikuwa kinyume cha sheria au yenye kasoro.
“Kwamba kila kesi lazima itegemee ukweli wake na hali yake na zaidi kusikilizwa upya kunapaswa kufanywa tu pale ambapo masilahi ya haki yanahitaji hivyo. Kwa mtazamo huo na kwa masilahi ya haki tunaona inafaa na ni sawa kwamba kesi hii ya jinai inabidi irudishwe Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa tena,” amesema Jaji Mwampashi.
Majaji hao walibatilisha mwenendo na hukumu na kuamuru shauri hilo kupelekwa Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa upya.
“Kwa masilahi ya haki, tunaelekeza kwamba kesi hiyo isikilizwe tena haraka na Jaji wa Mahakama Kuu, wakati huohuo, warufani wanapaswa kusalia rumande wakisubiri kusikilizwa upya kwa kesi hiyo na Mahakama Kuu,”
Ilidaiwa Januari 29, 2017 marehemu akiwa amelala nyumbani kwake na wanawe akiwemo shahidi wa tatu, Deus David, alivamiwa na kuuawa na watu waliodaiwa kuwa ni majambazi.
Kwa mujibu wa ushahidi wa tatu Deus, alifanikiwa kuwatambua washambuliaji hao, kwani nyumba hiyo ilikuwa na mwanga wa balbu zinazotumia nishati ya jua na pia kwa sababu walikuwa majirani zao na kuwa warufani hao.
Katika utetezi wao, warufani walikana kuhusika kwa namna yoyote na kifo hicho, japokuwa walikiri kukamatwa katika msiba huo ambapo walikuwa wamekwenda kuomboleza kifo cha marehemu ambaye alikuwa jirani yao.
Katika rufaa hiyo warufani hao, waliwakilishwa na Wakili Samwel Angelo, ambapo sababu yao kuu ilikuwa Mahakama Kuu ilikosea kisheria kuhamisha kesi chini ya kifungu cha 45 (2) cha Sheria ya Mahakama ya Hakimu Mkazi kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi ambaye alipaswa kuongezewa mamlaka.
Wakili huyo aliipeleka mahakama katika ukurasa wa 28 na 35 wa kumbukumbu ya rufaa ambapo inaonyeshwa kuwa jalada la kesi hiyo lilihamishwa kwanza kutoka Mahakama Kuu kwenda kwa hakimu mwingine, ambapo uhamisho huo ulitolewa kinyume na sheria.
Amesema kesi hiyo ilihamishwa kinyume na sheria ambayo inatumika ambapo kisheria ulipaswa kufanywa chini ya kifungu cha 256A (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Wakili huyo amesema kifungu hicho kinashughulikia uhamishaji wa kesi za jinai ambazo kwa kawaida, husikilizwa na Mahakama Kuu kwenda kwa Mahakimu Wakazi walioongezewa mamlaka kwa ajili ya kusikiliza mashauri.
Wakili huyo amesema kutokana na dosari hiyo Hakimu aliyesikiliza kesi hiyo hakuwa na mamlaka ya kuisikiliza, hivyo kuomba mwenendo na hukumu iliyotolewa kubatilishwa na warufani kuachiliwa huru.
Kwa upande wao mawakili wa Serikali, walikubaliana na hoja ya wakili wa warufani kwamba kesi hiyo ilihamishwa kimakosa kutoka Mahakama Kuu kwenda Mahakama ya Hakimu Mkazi.
Hata hivyo, mawakili hao walipingana na nini kinapaswa kuwa njia ya kwenda mbele licha ya kukubali mwenendo wa kesi hiyo ni ubatili, alikuwa na maoni kwamba, chini ya mazingira ya kesi hiyo inapaswa kuamriwa kusikilizwa upya.
Crédito: Link de origem