top-news-1350×250-leaderboard-1

Dk Tulia alivyoacha mnyukano ubunge CCM Mbeya Mjini

Mbeya. Siku chache baada ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson kutangaza nia ya kugombea ubunge katika Jimbo jipya la Uyole, makada wawili wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wameanza kupigana vikumbo Mbeya Mjini, huku wengine wakitarajiwa kutia nia muda wowote kuanzia sasa.

Wawili hao wanaopigana vikumbo, yumo Mwenyekiti wa chama hicho Mbeya Mjini, Afrey Nsomba na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mbeya ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, Charles Mwakipesile.

Vikumbo hivyo, vinakuja baada ya Mei 23 mwaka huu, Dk Tulia kutangaza upande atakaokwenda kugombea, siku chache tangu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ilipotangaza mgawanyo wa Jimbo la Mbeya Mjini na kuzaa jimbo la Uyole.

Mbali na wawili hao kutangaza nia ya kulitaka jimbo hilo, wengine wanaotarajiwa kutupa karata zao katika nafasi hiyo ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Ndele Mwaselela na Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge.

Awali, vigogo hao wenye ushawishi ndani ya CCM, walitajwa kuyawinda majimbo ya Rungwe kwa upande wa Mwalunenge, kwa kuwa ni nyumbani kwao.

Kwa upande wa Ndele anayeonekana kuwa na ushawishi zaidi kutoka kwa wananchi, awali alihusishwa na Jimbo la Mbeya Vijijini.

Lakini, wote hao kwa sasa wamelitolea macho Jimbo la Mbeya Mjini baada Spika wa Bunge, Dk Tulia kutangaza kwenda Uyole kuwania nafasi hiyo.

Licha ya kuhusishwa na nia hizo, hadi sasa hakuna yeyote kati yao aliyezungumzia mpango huo wala kutia nia rasmi, isipokuwa wamekuwa wakifanya shughuli za chama na ziara za kusikiliza kero za wananchi.

Akizungumzia uamuzi wake wa kugombea Mbeya Mjini alipozungumza na Mwananchi leo Jumapili Mei 25, 2025, Nsomba amesema kutokana na Dk Tulia kutangaza kuwa atagombea Uyole, amejipima na kuona anafaa kuwania nafasi hiyo Mbeya Mjini.

Kwa kuzingatia taratibu za chama chake, amesema muda utakapofika atakwenda kuchukua fomu, kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.

“Nimejipima na kuona nafaa, lakini yeyote mwenye kutaka nafasi asikate tamaa kwa kuwa Mwenyekiti nimetia nia, chama chetu kina utaratibu na kinafuata miongozo, pale muda utakapofika Juni 28, nitachukua fomu” amesema.

Iwapo chama hicho kitaridhia kumpa nafasi ya kupeperusha bendera yake na wananchi wakamchagua, amesema ataendeleza pale alikoishia Dk Tulia.

Amemsifu Dk Tulia kwa uongozi wake uliochochea maendeleo jimboni humo, kiasi cha kufanikisha utekelezwaji wa miradi mbalimbali mikubwa.

“Unapofika wakati wa mchakato, nitapisha vikao vya chama kufanya uamuzi, kwa maana hiyo nitakuwa nje ya uamuzi kuondoa mgongano wa kimasilahi, hakuna uchochoro nisioujua katika maisha ya wananchi,” amesema.

“Niwaombe wana-CCM wenzangu tusiwe na makundi, tumpiganie Rais Samia Suluhu Hassan apate kura nyingi na sehemu ya madiwani washinde sawa na wabunge na kwa nafasi yangu nitapigania hilo,” amesema.

Kwa upande wa Mwakipesile, amethibitisha kutangaza nia ya kulitaka jimbo hilo, ikiwa ni mara ya tatu kwa kada huyo aliyebobea katika taaluma ya habari.

Kwa kuwa ni haki kikatiba, amesema anasubiri rasmi Juni 28 kuwa miongoni mwa wengine wengi watakaochukua fomu kuomba ridhaa kwa wajumbe wampitishe agombee nafasi hiyo.

“Mimi ni mzaliwa wa hapa najua kila eneo lakini kila hitaji la wananchi, nimejipima na kuona nafaa kurudi tena kugombea nafasi hii, kwa kuheshimu nafasi ya Dk Tulia baada ya kwenda Uyole naona hapa Mbeya Mjini pananifaa,” amesema.

Mdau wa Siasa jijini Mbeya, Patrick Ezekiel amesema huenda watia nia wakaongezeka zaidi kwa sababu wanaamini ubunge ndio fursa inayomwezesha mwanasiasa kuwa na nguvu.

“Siyo Mbeya Mjini pekee, hata huko Uyole usidhani vita ni ndogo kwamba Dk Tulia atapita bila kupingwa, wapo wafanyabiashara na wanasiasa wengine wamenyamaza muda wowote idadi itaongezeka,” amesema.

Kwa upande wa Victor Mwashilindi amesema wakati CCM ikinyukana, wasisahau nguvu ya vyama vya upinzani, jambo alilodai litaufanya uchaguzi kuwa mgumu na shughuli itakuwa pevu.

“Tunaweza kuwa tunazungumza CCM lakini upinzani wakashangaza, naona ushindani ukiwa mkubwa katika uchaguzi huu, siasa kwa sasa ni fursa kubwa lazima wanyukane” amesema.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.