top-news-1350×250-leaderboard-1

Dk. Joyce awasihi wazazi kuwahimiza watoto kupenda elimu na ujuzi wa maisha

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Afisa Mkuu Mtaala Mwandamizi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk. Joyce Kahambe, amewasihi wazazi waendelee kuwahimiza watoto wapende elimu na kuhakikisha wanatumia ujuzi wanaojifunza shuleni katika shughuli za maisha yao ya kila siku, kama vile kilimo, ufugaji, muziki, na nyinginezo, hata kama wanapendelea kufuata taaluma zao rasmi.

Dkt. Kahambe alitoa wito huu wakati akizungumza katika Mahafali ya Saba ya Shule ya Sekondari ya Wavulana Christon, iliyofanyika Wilaya ya Kisarawe, Mkoani Pwani, leo, Februari 28, 2025. Alisema kuwa TET, ambayo ipo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ina jukumu la kuboresha na kusimamia mtaala wa elimu nchini ili kuhakikisha kuwa watoto wanajengewa ujuzi na nidhamu, ambayo itawawezesha kuwa na maisha bora katika jamii. Alisisitiza kwamba mtaala wa sasa umejikita katika kuwajengea wanafunzi ujuzi ambao utawasaidia kujiajiri au kuajiriwa, na hivyo kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira.

“Katika mtaala huu mpya, msisitizo umewekwa kwenye ujuzi, na ni muhimu watoto wasione kupata ujuzi kama mwisho wa safari yao ya kimasomo. Ujuzi huu una levels mbalimbali, na hata baada ya kumaliza shule, ujuzi huo utaendelea kuwasaidia. Kwa mfano, watoto watakaoendelea na masomo ya kidato cha tano na masomo ya amali wataendelea kutumia na kuendeleza ujuzi wao, ambao pia unatambuliwa na taasisi mbalimbali,” alieleza Dk. Kahambe.

Aidha, Dk. Kahambe aliwataka wazazi kuwasaidia watoto wao kuendeleza ujuzi waliopata shuleni, kwa kuwa mafunzo haya si adhabu, bali ni sehemu ya kujenga msingi wa maisha yao ya baadaye. Aliwahimiza wazazi kuwaunga mkono watoto wao katika shughuli mbalimbali, hasa zinazohusiana na ujuzi waliojifunza, kwa kuwashauri kuhamasika na kuwa na motisha ya kufanya kazi na kutumia ujuzi wao katika kilimo, ufugaji, muziki na nyinginezo. Alitolea mfano kilimo, akisema kwamba ni sekta muhimu inayohitaji ujuzi mkubwa, hasa kwa kuwa Watanzania wengi wanategemea kilimo kwa chakula na kujipatia kipato. Alisema kuwa kilimo kina faida kubwa na kwamba vijana wanapaswa kujivunia kuwa sehemu ya mabadiliko hayo kwa kujiunga na kilimo.

Dk. Kahambe pia alisisitiza kwamba mafunzo haya siyo adhabu, bali ni sehemu ya mchakato wa kuwajengea vijana ujuzi wa maisha na kuwawezesha kutambua mchango wao katika maendeleo ya jamii. Aliwashauri wazazi kuendelea kuwa msaada wa kimsingi kwa watoto wao, kuwawezesha kupata nafasi ya kujifunza na kutumia ujuzi wao katika maisha ya kila siku.

Naye, Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kilutheri Tanzania (KKT), Richard Hananja, alisisitiza umuhimu wa wazazi kuwa mfano mzuri wa maadili kwa watoto wao. Alisema kuwa watoto mara nyingi hutazama na kuiga vitendo vya wazazi wao, hivyo ni muhimu wazazi kuwaonyesha maadili bora kama vile uaminifu, heshima, na upendo.

Alifafanua kuwa wazazi wanapaswa kuwa na ushawishi mzuri kwa watoto wao kwa kuwafundisha maadili siyo tu kwa maneno, bali pia kwa vitendo. Alieleza kwamba watoto wanapojifunza kusaidiana na kushirikiana, wanaweza kujenga moyo wa kutoa na kuwa na uhusiano mzuri na wenzao.

“Thamani ya kazi ni bora kuliko mshahara. Hakuna mtu ambaye hakupita mikononi mwa mwalimu. Waalimu wanatumbua mchango wao katika maadili na maendeleo ya watoto wetu,” alisema Mchungaji Hananja.

Aliongeza kuwa Shule ya Sekondari ya Christon siyo tu ni shule, bali ni chuo cha maadili. Alisema kwamba kizazi cha leo kimepoteza maadili ya msingi, na wazazi wanapaswa kuwafundisha watoto wao umuhimu wa kwenda kwenye nyumba za ibada ili kuwa na maadili bora katika jamii. Aliendelea kusema kwamba ni muhimu wazazi waendelee kuwa mfano mzuri wa maadili na kuwafundisha watoto wao kuhusu maisha ya jamii za Kitanzania.

Mchungaji Hananja aliendelea kwa kusema kuwa wanafunzi waliofanya mahafali wanapaswa kuelewa kuwa elimu ni ya msingi na inawahitaji kuchukua hatua nzuri katika maisha yao. Alisisitiza kuwa wanapaswa kuepuka makundi hatarishi, kama vile madawa ya kulevya, ambayo yanaweza kuharibu maisha yao. Alisema kuwa kutumia dawa za kulevya siyo ujanja, na kwamba vijana wanapaswa kujiepusha na vishawishi vyote vya kujiingiza kwenye vitendo vya kijinsia, ikiwa ni pamoja na mapenzi ya jinsia moja. Aliwahimiza wazazi kuendelea kuwaongoza watoto wao katika misingi ya maadili na kuwaandaa kwa mustakabali bora.

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Christon, Augustine Minja, alielezea mafanikio ya shule hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015. Alisema kuwa shule ilianza na wanafunzi 86, lakini hadi sasa ina wanafunzi 615.

Alifafanua kuwa maono ya shule hiyo ni kuwa walimu wake wangeweza kuelimisha shule zingine kuhusu mbinu za mafundisho na kuhakikisha wanafunzi wanafaulu vizuri katika mitihani yao ya mwisho. Alisisitiza kwamba ingawa baadhi ya wazazi hawataki watoto wao kufanya kazi za mikono, hiyo siyo changamoto bali ni fursa ya kuwaandaa watoto kuwa viongozi bora katika jamii baadae.

Minja alikiri kwamba wazazi wanatengeneza changamoto kwa watoto wao kwa kutokubaliana na kuwaunga mkono katika kufanya kazi za mikono, lakini aliwataka waone umuhimu wa kusaidia watoto wao kujifunza na kujitolea katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.