Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko amesema licha ya jitihada za kuwainua wanawake kiuchumi kufanikiwa, bado kuna changamoto zinazohitajika kutatuliwa, ili kufungua fursa zaidi kwao.
Kiongozi huyo, amezitaja changamoto hizo kuwa ni ubaguzi na ukatili wa kijinsia hususan maeneo ya vijijini, uelewa mdogo wa masuala ya jinsia, changamoto za kifamilia, mila na desturi kandamizi.
Dk Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati, ameeleza hayo usiku wa kuamkia leo Aprili 5, 2025 wakati wa kilele cha msimu wa tisa wa tuzo za ‘Malkia wa Nguvu’zilizoandaliwa na Clouds Media Group zilizokuwa na kaulimbiu ‘malkia wa nguvu 2025 twende duniani’.
“Zipo jamii zinamuona mwanamke kama hana haki sawa na mwanamke, mila na desturi kandamizi lazima tuzipige vita kwa pamoja na jukwaa hili la malkia wa nguvu, liwe sehemu ya kukemea ukatili wa aina yoyote wa jinsia kwa mwanamke,” amesema Dk Biteko.

Amefafanua kuwa katika misingi ya kinjisia mtoto wa kiume anapata haki zaidi kuliko wa kike, akisema ni jambo linalohitaji kupigiwa kelele na majukwaa mbalimbali, likiwemo la malkia wa nguvu.
“Changamoto hizi zinahitaji mipango madhubuti na ushirikiano wa wadau wote wa sekta ya umma na sekta binafsi, msemo unasema umoja ni nguvu. Nitoe rai kwa wadau wote muhimu kushirikiana na Serikali, ili kutokomeza changamoto za namna hii,”amesema Dk Biteko.
Licha ya hayo, Dk Biteko amesema Serikali imepiga hatua kubwa ya kuhakikisha mwanamke anakuwa sehemu ya maendeleo katika jamii na miongoni mwa hatua ilizochukua ili kufanikisha hilo ni kuboresha elimu iliyongeza wasomi wengi wanawake.
Dk Biteko ametaja hatua nyingine kuwa ni mazingira wezeshi ya kiuchumi, fursa za biashara, uwekezaji na fursa za kifedha mikopo yenye masharti nafuu. Pia, ushirikiano wa Serikali na jumuiya za kimataifa.
Mwenyekiti wa Kamati ya Malkia wa Nguvu, Liliane Masuka amesema lengo kuu la jukwaa hilo ni kuhamasisha na kuunga mkono wanawake katika nyanja za ujasiriamali, maendeleo ya kiuchumi na masuala mengine mbalimbali ya kijamii.
“Malkia wa Nguvu si tu tuzo ni harakati ya kuamsha thamani ya mwanamke wa Kitanzania na kumjengea jukwaa la mafanikio. Kupitia Malkia Wa Nguvu, 2025 tumejipanga kutekeleza miradi mikubwa yenye dira ya kimataifa,”amesema Masuka.
Masuka amesema miradi hiyo ni pamoja na jukwaa la kidijitali kwa wanawake kupata maarifa, masoko na mitandao, mfuko wa kusaidia wasichana wanawake wabunifu kupata mitaji ya biashara, kuwapeleka 100 nchini China wanawake kujifunza teknolojia, viwanda, na masoko mapya.
Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Zena Ahmed Said aliibuka mshindi wa tuzo ya uongozi na utumishi wa umma, huku Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson akiibuka mshindi wa tuzo ya heshima ya malkia wa nguvu.
Crédito: Link de origem