Miaka mitano iliyopita, wanafunzi 14 pekee wa kike ndiyo walikuwa wakisoma kozi ya ubaharia kwenye chuo cha Bahari Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Tumaini Shaban Gurumo anasema, mtazamo hasi juu ya fani ya ubaharia ndiyo chimbuko la wanawake wengi kuchelewa kuingia kwenye fani hiyo.
“Ubaharia ilidhaniwa ni kazi ambayo ni ya mtaani, uhuni uhuni fulani ili mradi tu mtu akizamia meli akasafiri basi tayari huyo anaonekana ni baharia, lakini haipo hivyo, ubaharia ni fani kama nyingine,” anasema Profesa Tumaini katika mahojiano maalumu na Mwananchi.
Anasema ukiachana na wanaume, kati ya mwaka 2021 hadi 2024, fani hiyo ilikuwa na wanawake 14 pekee waliosoma kwenye Chuo cha Ubaharia Dar es Salaam.
“Wazazi walikuwa hawataki kuona mabinti zao wanaingia kwenye hii fani, zilitolewa hadi ofa za masomo lakini bado wengi walikataa kutokana na mtazamo hasi juu ya ubaharia. Tuliendelea kuwaelimisha na hadi mwaka 2025 wanawake na wasichana wanaosoma fani hii wanafika 104,” anasema.
Hata hivyo, Profesa Tumaini anasema licha ya kupiga hatua hiyo, bado mwamko wa wanawake sio mkubwa kwani 104 waliopo ni sehemu tu ya wanafunzi 5900 wanaosoma ubaharia chuoni hapo.
Achana na zile fikra za mtaani kuhusu ubaharia, Profesa Tumaini anasema mabaharia ni wale tu wanaosoma na kufanya mitihani ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac).
“Kabla ya kuingia kwenye meli wanafanya mafunzo melini, wanatembea na chombo ndipo wanafanya mitihani ya Tasac, wakifaulu wanakuwa mabaharia au wafanyakazi wa melini,” anasema.
Anasema hadi kuwa baharia kuna njia kuu mbili za kusoma. Hatua ya kwanza ni wale wanaosoma ubaharia moja kwa moja.
“Hii tunaiita umahiri, lazima uwe umetoka kidato cha nne, unaingia darasani, hii ni kozi ya lazima ya usalama baharini unaisoma kwa wiki tano, hiyo ndiyo hatua yako ya kwanza. Hapo unafundishwa namna ya kukaa salama baharini, baada ya hapo sasa utaingizwa kwenye chombo ukajifunze mazingira yalivyo,” anasema.
Profesa Tumaini anasema utakuwa kwenye chombo kwa miezi sita, katika kipindi hicho utakuwa umeshajisikia kama wewe ni wa humo au urudi nchi kavu.
“Humo ndani ya chombo utakuwa ukisaidia kazi wakikuelekeza hiki na kile, ukitoka huko tayari utakuwa ulishajua unataka kuwa nahodha ukae juu kuongoza chombo au uwe injinia ukae kwenye mitambo. Utaendelea hatua nyingine ya darasani mwaka mmoja na kurudi baharini miaka miwili, ubaharia una hatua zake utaanza kuwa msaidizi, kisha ofisa, utaendelea hivyo hadi kufika hatua ya kapteni mkuu,” anafafanua.
Anasema hatua ya pili, wameitengeneza kwa namna ambayo unaunganisha umahiri huo pamoja na ubaharia, ambapo mtu aliyesoma kozi hiyo atapata cheti cha diploma au cheti, lakini ndani yake kina kozi ya ubaharia.
“Pamoja na haya, baharini lazima utakwenda japo hatua hii kuna mahali utapata advantage (faida) kwa wale wanafunzi wanaoanzia kwenye diploma au shahada ya kozi ya Marine Engineering au Maritime Transport and Nautical Science. Hawa wanasoma miaka mitatu hadi minne darasani kisha wanaingia kwenye chombo kwa miezi 12. Akitoka atafanya mtihani Tasac, akifaulu atapata cheti cha kuwa ofisa,’’ anaeleza.
Anasema atafanya kazi mwaka mmoja akiwa msaidizi huku akijifunza, kisha atakuwa ofisa wa daraja la tatu kwenye meli.
“Akitaka kupanda atarudi tena darasa, atasoma kitu kinaitwa class two la ubaharia mwaka mmoja, kisha atarudi baharini mwaka mmoja, atafanya mtihani, unapoendelea kusoma na kufaulu unapanda hadi kufika hatua ya kuendesha chombo kikubwa kabisa, ubaharia ndio upo hivyo ni kama kwenye taaluma nyinginezo,” anasema.
Anasema uzoefu wa kwenye maji na masomo ya darasani ndiyo vinafanya mtu aitwe captain ambaye ni baharia wa ngazi ya juu kabisa ambaye elimu yake si chini ya miaka saba.
Changamoto za wanawake kwenye ubaharia
Pamoja na wanawake na wasichana 90 kuongezeka kusoma fani hiyo kulinganisha na 14 waliokuwa wakisoma katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Profesa Tumaini anasema kuna changamoto kubwa tatu zilizokwamisha kujiunga kwenye fani hiyo.
“Si kwa wanawake na wasichana tu hata kwa wanaume, sababu ya kwanza ni fani hii haikuwa ikijulikani sana, hivyo hii nayo imechangia.
“Kingine hapa Tanzania hatuna meli nyingi, japo sekta ya usafirishaji asilimia 80 ni maji, nchini hatuna vyombo vingi, meli za mizigo nyingi zinatoka nje ya nchi zinaleta vitu na kuondoka, hii pia ilichangia mwamko wa watu kusoma ubaharia kutokuwa mkubwa,” anasema na kuongeza:
“Uchache wa vyombo ulisababisha mwamko usiwepo, watu wengi hawakuona kama kwenye bahari au maji napo wanaweza kufanya kitu. Kingine ni mtazamo hasi juu ya ubaharia, ambapo ilidhaniwa ni kazi ambayo ni ya mtaani, ili mradi tu mtu akizamia meli akasafiri basi huyo tayari ni baharia, lakini sivyo, hii ni fani.’’
Anasema vijana wengi waliokuwa na nia na matamanio ya kuwa mabaharia familia zao ziliwarudisha nyuma kwa kiasi kikubwa.
“Ilikuwa tunakutana na vijana unaona wana passion (wanapenda) na wako tayari hata kutengwa na familia ili waingie kwenye fani hii, ambacho tulipambana kukifanya na tunaendelea nacho ni kufanya ushauri nasaha kwa wazazi kuwambia hakuna ubaya vijana wao kusoma ubaharia na taratibu wanaelewa,’ anaeleza.
Anasema wapo wazazi si wa watoto wa kike tu hadi wanaume, mtoto akisema anataka kusoma ubaharia hawamuelewi kwa sababu tu ya dhana potofu.
Anasema mtu anayesoma na kuhitimu chuoni hapo, una uwezo wa kufanya kazi popote duniani, kwa kuwa kozi wanazozitoa zimethibitishwa kimataifa.
Kwa wasichana na wanawake, profesa Tumaini anasema changamoto kubwa zaidi kwa jinsia hiyo ni kukosa watu wa kuwatia moyo na kuwajenga kuhusu fursa zilizopo kwenye ubaharia.
“Familia nyingi zinawazuia kusoma fani hii kwa sababu ya ile dhana potofu, wanaona mtoto wangu wa kike aende kuwa baharia? Kuna wakati tulitoa hadi ofa ya masomo, mtu alijitolea kuwasomesha vijana wa kike, lakini wazazi walikataa wakasema hawapeleki mabinti zao kufanya kazi melini, ‘’ anasema.
Anasema kama chuo, ili kuondoa dhana potofu, kikubwa wanachokifanya ni kutoa elimu kuhusu ubaharia, wakipita shuleni na kwa walimu kuwaeleza fursa zilizopo katika ubaharia.
“Hata huu mkakati wa Serikali wa uchumi wa bluu umetuinua sana, kama chuo tumelibeba kwa kufanya makongamano kuelezea fursa za uchumi wa bluu ambao unahusiana na shughuli tunazozifanya.Vilevile kuna taasisi ya wanawake walioko katika sekta ya bahari, nao wana bidii ya kuleta wanafunzi wa kike katika sekta ya ubaharia na kuwasaidia kuipenda,” anasema.
Ukiachana na fursa ikiwamo ajira katika uchumi wa bluu, Profesa Tumaini anasema huko duniani kuna uhitaji mkubwa wa mabaharia.
“Vijana wetu wakisoma wakafaulu na kupata vyeti vinavyostaili ajira zipo wazi huko duniani na matunda ya fani hii siku si nyingi jamii itayaona,” anasema.
Anasema kuna fursa nyingi zimefunguka, hivi sasa kuna kampuni ya meli ya Ulaya ambayo chuo kimezungumza nao itakuwa ikichukua vijana wa kike kwenda kufanya mazoezi.
“Watakaofaulu kampuni ile inawaajiri, tumeanza nao mwaka huu, tutapeleka kundi la kwanza, wakifanya vizuri maana yake watafungua mlango kwa wengine,” anasema.
Anasema tabia za wanawake katika fani yoyote kuna vitu wanafanana na alipo mwanamke, kuna uaminifu zaidi ndiyo sababu katika fani mbalimbali wanakubalika.
“Sio rahisi kukuta mwanamke anaiba au anapokea rushwa, akipewa kazi huwa anataka jambo lake litimie, wanawake tumezaliwa ni viongozi kuanzia ngazi yaa familia,” anasema.
Licha ya uchache wa wanawake na wasichana kuingia kwenye fani ya ubaharia, profesa Tumaini anasema Tanzania ina makapteni wa melini na wahandis daraja la tatu ambao ni wanawake.
“Mwingine yupo hapa chuoni, huyu ni icon (nembo) yetu, ni mwanamke wa kwanza kuwa baharia alisoma chuo hiki hiki, sio kapteni ni injinia, alifanya kazi hiyo na baadaye alirudi kufundisha hapa,” anasema.
Profesa Tumaini alivyoweza
Akizungumzia safari yake hadi kumudu kwa ufanisi kuwa mkuu wa chuo licha ya mtazamo hasi wa jamii, Profesa Tumaini anasema kilichofanya awe hapo ni msaada kutoka kwa wengine.
“Baba yangu alikuwa akinisapoti, aliweka imani kwangu na hakunichukulia kama mtoto wa kike tu, aliamini ninaweza na nilimthibitishia hilo na kila kitu nilichoshika alinisapoti,” anasema.
Anasema alipoingia kazini alikutana na mazingira hayo kutoka kwa mabosi ambao walimuona ana kitu na kuendelea kumsaidia.
“Katika sapoti yao nilijikuta nafanya jitihada, nikijua na kuamini naweza, unapofanya kitu ukapata msaada ni tofauti na ile unafanya halafu kuna mtu anakuvuta shati kukurudisha nyuma akiona wewe ni mwanamke tu huwezi,” anasema.
Anasema kingine kilichomfikisha hapo ni kujiamini baada ya kuaminika, hivyo kuwa na nguvu mara mbili .
“Vikwazo vipo hakuna mwanamke aliyekaa kwenye uongozi akakutana na mambo laini lainj, hayupo, lakini ukijiamini na kutimiza wajibu wako hata wakitokea watu wa kukuvuta shati hawakurudishi nyuma,’’ anasema na kuongeza:
“Ambacho naweza kuwambia wanawake na mabinti wenye mapenzi ya kuingia kwenye fani hususani sekta ya bahari, sekta hii imekuwa pana ina fursa nyingi za ajira na masomo. Wazitumie wasijifungie na kuona kama wanawake ni kama zamani kwamba kazi zao ni laini laini tu, ukiweka nia utafanya kazi yoyote kwa ufanisi.’’
Crédito: Link de origem