top-news-1350×250-leaderboard-1

Dereva ajali iliyoua saba akamatwa, waliofariki watajwa

Mwanga. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linamshikilia dereva wa basi la Kampuni ya Mvungi, lililopata ajali na kusababisha vifo vya watu saba na majeruhi 42.

Abiria hao walikuwa wakisafiri kutoka Ugweno, Wilaya ya Mwanga, kuelekea jijini Dar es Salaam.

Ajali hiyo imetokea leo, Alhamisi, Aprili 3, 2025, saa moja asubuhi, katika eneo la Kikweni, Kijiji cha Mamba, Kata ya Msangeni, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro.

Basi walilokuwa wakisafiri abiria liliacha njia na kupinduka kwenye bonde, na kusababisha vifo vya watu hao.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema kuwa wanamshikilia dereva huyo kwa mahojiano zaidi kuhusiana na ajali hiyo.

“Leo, Aprili 3, 2025, watu saba wamefariki dunia na wengine 42 wamejeruhiwa, baada ya basi mali ya Kampuni ya Mvungi, lililokuwa likitokea Ugweno kuelekea jijini Dar es Salaam, kupinduka kwenye bonde katika eneo la Kijiji cha Mamba, Kata ya Msangeni. Ajali hiyo imesababisha vifo vya watu saba,” amesema Kamanda Maigwa.

Kamanda Maigwa amesema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva kushindwa kulimudu gari wakati alipokuwa akipishana na jingine kwenye kona kali, na hivyo kuacha barabara na kutumbukia bondeni.

“Kwa sasa tunamshikilia dereva kwa mahojiano zaidi,” amesema Kamanda Maigwa.

Aidha, Kamanda Maigwa amewataja waliofariki dunia kuwa ni Ashura Omari Sakena (47), mkazi wa Vuchama, Zaituni Hashimu Mwanga (52), mkazi wa Masumbeni, Halima Omari (02), na Judithi Safieli Mwanga (43), mkazi wa Mangio.

Wengine ni Haji Abubakari, (50) mkazi wa Kifula, Hamadi Hussein Mshana (64) mkazi wa Ngalanga Ugweno na Benadetha (20) mfanya kazi wa ndani aliyetajwa kwa jina moja.

Pia, amesema majeruhi wote wanaendelea na matibabu katika hospitali za Kifula, Hospitali ya Wilaya ya Mwanga, KCMC na Hospitali ya Mkoa ya Mawenzi huku miili ya marehemu ikihifadhiwa hospitali ya Wilaya ya Mwanga kusubiri uchunguzi na taratibu nyingine.

Ajali hiyo imetokea ikiwa zimepita siku nne tangu kutokea ajali nyingine, Machi 30, 2025, iliyoua watu saba katika matukio mawili tofauti wilayani Same.

Moja ya ajali hizo ilikuwa ni ile iliyoua wanakwaya sita wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mmeni Chome, Dayosisi ya Pare, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka katika milima ya Pare.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.