top-news-1350×250-leaderboard-1

Deam Team FC yatwaa ubingwa Samia Cup, mbungi kuhamia visiwani Zanzibar

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Timu ya soka ya Dream FC ya Ferry Kigamboni imefanikiwa kutwaa ubingwa wa michuano ya Samia Cup kwa kuichapa Wahenga FC mabao 2-0 katika mchezo wa fainali uliopigwa Aprili 5, 2025 kwenye Uwanja wa Mji Mwema, jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na Taasisi ya Twende Pamoja na Mama Sports Promotion chini ya Mkurugenzi wa Makunduchi Villa, Mohammed Hajji maarufu Boss Mo yalianza Februari 7, 2025 yakishirikisha jumla ya timu 32 kutoka maeneo mbalimbali ya jijini humo.

Akizungumzia mashindano hayo, mgeni rasmi wa mechi ya fainali, Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Ally Bananga amewapongeza waandaaji wa michuano hiyo kwa kufanya jambo katika kusheherekea miaka minne ya utawala wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Amesema mashindano hayo yanasaidia kuibua vipaji, huku akiwaomba waandaaji hao kufanya mashindano mengine yatakayohusisha wanawake hasa netiboli.

“Mheshimiwa Rais ni mwanamichezo namba moja katika nchi yetu. Suala la soka wote ni mashahidi kwani kwa sasa Tanzania si washiriki wa mashindano ya Afrika bali washindani wa mashindano ya Afrika,” ameeleza.

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Twende Pamoja na Mama Sports Promotion, Boss Mo amesema mashindano hayo yatakuwa endelevu na si Dar es Salaam pekee, kwani baada ya kumaliza Kigamboni wanaelekea visiwani Zanzibar kufanya michuano kama hiyo itakayoitwa Dk. Hussein Mwinyi & Samia Cup 2025.

“Nimefarijika kuona umati mkubwa wa watu wamekuja kushuhudia mashindano haya. Niahidi tu kuwa mashindano haya yatakuwa endelevu, si kwamba kuna kitu tunakitafuta bali ni kumuunga mkono kwa vitendo Daktari Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Kwa upande wake kocha wa Dream Team, Florian Mbelwa ameeleza siri ya kutwaa ubingwa huo kuwa ni uongozi bora wa timu pamoja na kupambana kwa wachezaji kujitoa kwa moyo wote uwanjani.

Amesema wamechukua ubingwa kwa kushinda mechi zote, nne wakipata ushindi ndani ya dakika 90 lakini mchezo mmoja wa robo fainali walishinda kwa mikwaju penalti.

“Katika mashindano haya mechi ngumu zaidi kwangu ilikuwa ya marudiano dhidi ya Miti Mirefu katika hatua ya 32 bora, mambo yalikuwa magumu ikanilazimu kutumia mbinu zangu zote na kufanya sub nyingi na tukafanikiwa kushinda 2-1,” amesema kocha huyo.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.