Dar es Salaam. Chama cha Wananchi (CUF) kimetangaza ratiba ya uchaguzi wa ndani kwa ajili ya kupata wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
Mbali ya hayo, CUF kimetoa wito kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kuthibitisha dhamira yake ya kuendesha uchaguzi huru, wa haki na wa amani kikisema hakuna mtu au chama chenye haki miliki ya Taifa.
Kauli hiyo imetolewa leo Aprili 25, 2025 na Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi Taifa wa chama hicho, Yusuph Mbungiro alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ratiba ya kura ya maoni ndani ya CUF kuelekea uchaguzi mkuu.
“Dunia inaitazama Tanzania, tunamuomba Rais Samia kuonyesha kwa vitendo kuwa uchaguzi huu hautakuwa wa kupendelea chama au mtu, bali utaangalia masilahi ya Taifa na watu wake,” amesema.
Amesema bado kuna changamoto ya kutokamilika kwa mchakato wa Katiba mpya na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Mbungiro amesema CUF itaendelea kupigania kupatikana kwa Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi mpaka pale watakapofanikiwa kwa kuwa suala hilo siyo kwa masilahi ya chama hicho, bali kwa ustawi wa Taifa na Watanzania kwa ujumla.
“Tunajua malalamiko yetu mengi bado hayajafanyiwa kazi ipasavyo, ikiwemo madai ya Katiba mpya na Tume huru ya uchaguzi lakini jambo hilo halitufanyi tuache kuingia katika uchaguzi,” amesema.
Mbungiro amewataka wanachama na wafuasi wa CUF kutoyumbishwa na kubabaishwa na maneno ya upotoshaji dhidi ya misimamo na mitazamo ya chama chao bali kuendelea na harakati za ujenzi wa chama hicho.
Amesema harakati za ujenzi wa chama ni kupigania demokrasia na kaulimbiu ya CUF kuelekea uchaguzi mkuu ni ‘Kipato cha msingi ni haki ya kila Mtanzania: Ni haki yako ni haki yangu’.
Amewataka wanachama waende kwenye uchaguzi kuomba ridhaa ya wananchi ili kutekeleza sera ya chama chao.
Mbungiro ametoa wito kwa wananchama kujitokeza kwenye shughuli ya uandikishwaji wa awamu ya pili katika Daftari la Kudumu la Mpigakura itakayoanza Mei Mosi, 2025.
Mwenyekiti wa INEC, Jaji Jacobs Mwambegele Aprili 14, mwaka huu alitangaza kuanza kwa ngwe ya pili ya uboreshaji wa daftari hilo kuanzia Mei Mosi hadi Julai 4, 2025.
Mchakato huo ni sehemu ya utekelezaji wa masharti ya kifungu cha 16(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024, kinachoelekeza kufanyika kwa maboresho hayo mara mbili kati ya uchaguzi mkuu uliopita na uteuzi wa wagombea wa uchaguzi ujao.
CUF kikitangaza ratiba yake ya uchaguzi wa ndani, kimetoa wito kwa wanachama wake kujitokeza kwa wingi kushiriki mchakato huo kwa lengo la kukiimarisha na kushika hatamu za dola.
Amesema uchukuaji na urejeshaji wa fomu kwa nafasi ya udiwani utaanza Aprili 26 hadi Julai Mosi, 2025, huku kura ya maoni itafanyika kati ya Julai 11 hadi 20, 2025.
Kwa ngazi ya ubunge na uwakilishi, amesema uchukuaji na urejeshaji fomu ni kati ya Juni 6 hadi Julai 7 na kura ya maoni iyafanyika kati ya Julai 10 hadi 20, mwaka huu.
Kwa nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na urais wa Zanzibar, fomu zitachukuliwa na kurejeshwa kati ya Juni 15 hadi 30, na mkutano wa uteuzi wa wagombea ufanyika Julai 27, 2025.
“Tunatoa wito kwa wanachama wote wa CUF wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kujitokeza kwa wingi, kwa kuzingatia katiba ya chama, kanuni za uchaguzi na miongozo ya ndani ya chama. Lengo letu ni kuhakikisha tunatekeleza sera za chama kwa ajili ya maendeleo ya kweli kwa Watanzania wote,” amesema.
Crédito: Link de origem