top-news-1350×250-leaderboard-1

CRDB, UNDP kuwaunganisha wafanyabiashara soko huru Afrika, kampuni 11 zatia mguu

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Katika kuhakikisha wajasiriamali nchini wananufaika na Soko Huru la Afrika (AfCTA), Benki ya CRDB na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania zimeanza kuwaunganisha wafanyabiashara na fursa za soko hilo.

Utekelezaji wa Soko Huru la Afrika ulianza Januari 2021 na Bunge liliridhia Septemba 2021 na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa mataifa yaliyokidhi vigezo vya kushiriki na mpaka sasa kampuni 11 za Tanzania zimefanikiwa kuuza bidhaa zake katika nchi mbalimbali.

Akizungumza leo Machi 3,2025 wakati akizindua mpango wa uunganishaji wafanyabiashara wadogo na fursa za Soko Huru Afrika, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amesema hui ni mwanzo mzuri unaotoa hamasa kwa wajasiriamali wengine kufuata nyayo.

“Mkataba huu umezifanya nchi nyingi za Afrika kuondoa vikwazo vya kikodi na visivyokuwa vya kikodi vilivyokuwa vinarudisha nyuma wafanyabiashara wengi kupanua huduma zao.

“Kupitia programu hii washiriki watapata maarifa ya kipekee hasa wakati huu Tanzania inapojiandaa na mchakato wa Dira ya Maendeleo ya 2050,” amesema Kigahe.

Kwa mujibu wa Kigahe, bidhaa zilizouzwa kwa wingi ni nyuzi za katani tani 426.4, kahawa tani 275.3 na tumbaku tani 21.1 ambazo zimeuzwa kwenye nchi za Nigeria, Ghana, Morocco, Misri na Algeria.

Naibu Waziri huyo ameipongeza CRDB Bank Foundation kwa kuwa wanawake na vijana wanaunda zaidi ya asilimia 75 ya watu waliopo nchini na kuzitaka kampuni zingine kuiga juhudi hizo ili Watanzania wengi zaidi wanufaike na fursa za soko hilo.

Aidha ameitaka CRDB Bank Foundation na UNDP Tanzania kuhakikisha mafunzo yanawafikia wanawake na vijana wengi zaidi nchini ili kila Mtanzania mwenye uwezo aweze kunufaika na fursa za soko hilo.

Naye Mkurugenzi wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema mchakato wa kuwatambua na kuainisha wajasiriamali watakaoshiriki katika programu hiyo tayari ulishafanyika katika mikoa 18 na zaidi ya wanawake wajasiriamali 600 wamechaguliwa na kuanza kupatiwa mafunzo.

Amesema programu hiyo imejikita katika kuwawezesha vijana na wanawake wajasiriamali ili washiriki kikamilifu katika soko hilo .enye watu zaidi ya bilioni 1.5.

Amesema washiriki 300 wameshapatiwa mafunzo kutoka Mikoa ya Arusha, Manyara, Singida, Kagera, Mwanza, Iringa, Mbeya, Ruvuma na Songwe.

“Malengo ya mradi huu ni kuainisha na kutambua wajasiriamali, wadogo na wa kati wenye uwezo wa kushiriki katika biashara za ndani ya Bara la Afrika.

“Kukusanya taarifa muhimu kuhusu wajasiriamali ikiwa ni pamoja na bidhaa zao, uwezo wao wa kuzalisha, uzoefu wa biashara, changamoto na matarajio yao,” amesema Mwambapa.

Amesema pia kupitia mradi huo wataanzisha mfumo wa taarifa na kanzidata ya wajasiriamali kwa kusaidia juhudi za kuwajengea uwezo na kuwaunganisha na fursa hizo pamoja na kupima utayari wa wajasiriamali wa kushiriki katika soko hilo.

Washiriki wa mafunzo ya leo wametoka katika Mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Mtwara, Pwani, Tanga na Zanzibar.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.