Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kinafuatilia kwa karibu tuhuma zinazosambazwa mitandaoni juu ya kupigwa kwa Mratibu wa Uenezi wa Baraza la Wanawake wa Chama (Bawacha), Sigrada Mligo.
Mbali na hilo, kimemuonya kiongozi huyo kuwa makini na asitumiwe kisiasa na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Sigrada (34) anadaiwa kupigwa Machi 25, 2025 na mmoja wa walinzi wa Chadema kwenye kikao cha ndani kilichoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, John Heche mkoani Njombe.
Siku iliyofuata, Machi 26, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga alimtaja Noel Olevale, anayedaiwa kuwa mlinzi wa Chadema, kuwa ndiye anayetuhumiwa kufanya shambulio hilo la mwili.
Banga alisema tukio hilo lilitokea wakati viongozi wa Taifa wa Chadema walipokuwa kwenye kikao cha ndani kilichoongozwa na Heche.
Tangu kutokea kwa tukio hilo, viongozi mbalimbali wa CCM kwa nyakati tofauti wamekuwa wakililaani, na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla ameendesha harambee katika moja ya mikutano yake kumchangia kada huyo fedha za matibabu.
Aidha, Makalla amemtembelea Mlingo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa mkoani Dodoma alipolazwa kwenye wodi ya watu mashuhuri (VIP).
Mwenyekiti wa Jumuya ya Wanawake wa CCM (UWT), Mary Chatanda pia amelaani tukio hilo na kulitaka Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) kujitokeza kukemea tukio hilo.
Leo Jumatatu, Machi 31, 2025, Chadema imetoa taarifa kwa umma ikisema inafanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli wa jambo hilo na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa katiba, kanuni na miongozo yake.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi, Brenda Rupia, chama hicho pia kinafuatilia “kwa makini kile njama za CCM za kutumia tukio hilo kwa manufaa yake binafsi.”
“Tunatoa wito kwa Sigrada Mligo kuwa makini na mahusiano yake na CCM ili kuepuka kutumiwa kwa malengo yasiyo na nia njema, ambayo yanaweza kuathiri si tu hadhi ya chama bali na ya kwake pia kama kiongozi na usalama wake binafsi,” imesema taarifa hiyo.
Chadema pia kiemesema kinaendelea kufuatilia kwa karibu kila hatua inayochukuliwa kwa kushirikiana na vyombo husika vya ndani na nje ya chama na baadaye watatoa kauli rasmi kuhusu suala hilo, kadri itakavyofaa.
Tamko hilo limetolewa wakati ambao Mlingo alishalisimulia sababu ya kushambuliwa na mlinzi huku akilalamikia kunyimwa nafasi ya kujitetea juu ya tuhuma alizopewa, kwenye kikao cha ndani cha chama hicho kilichofanyika mkoani Njombe.
Akizungumza na Mwananchi, alisema miongoni wa tuhuma dhidi yake ambazo ziliwasilishwa kwa Heche aliyeongoza kikao cha ndani, ni kuendesha vikao bila kufuata utaratibu wa chama.
Mligo aliyasema hayo Machi 27, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Hospitali ya Kibena, Njombe ambako alikuwa amelazwa kabla ya kuhamishiwa Benjamin Mkapa.
Amesema ndani ya kikao hicho muda ulipofika wa yeye kuzungumza, alikatishwa na alipomweleza Heche ampe nafasi ya kuzungumza, aliambiwa akae chini.
Mligo alisema alimwambia Heche: “Utakuwa hutendi haki nisikilize, naomba unipe muda nikusimulie vizuri hili jambo, kwa sababu unatakiwa ulijue kiundani, lakini yeye akaniambia nikae chini, nikasema sawa mwenyekiti, lakini tunaonewa, naomba utusikilize. Akasema toka nje, nikasema sawa bosi wangu,” alidai Mligo.
Mligo alisema alipotoka nje aliamua kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kwa Heche akiomba aruhusiwe kurudi kwenye mkutano, lakini Heche hakujibu.
Alidai akiwa bado nje, kuna watu walimfuata wakamweleza aingie ukumbini kuendelea na kikao, ili kumalizia hoja yake.
Mligo alidai wakati akienda kuingia ukumbini, ghafla alitokea mtu wa ulinzi na usalama wa chama na kumshambulia.
Alidai mtu huyo alimpiga ngumi kichwani na kudondoka sakafuni.
Mligo alidai aliokolewa na polisi waliokuwa kwenye doria na kumpeleka nyumbani kwake, na siku iliyofuata aliamka na maumivu yaliyosababisha alazwe hospitali kwa matibabu.
Crédito: Link de origem