Mbeya. Wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa kupotea kwa mwanaharakati na kada wa Chadema, Mdude Nyagali, viongozi na wafuasi wa chama hicho Mkoa wa Mbeya wameanzisha jitihada za kumtafuta katika maeneo ya porini.
Msako huo umeanza baada ya viongozi sita wa Chadema, wakiwa na wafuasi 58, kuandamana leo mchana, Jumamosi, Mei 3, 2025, hadi Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, wakitaka kupata taarifa kuhusu mambo mawili.
Mambo hayo ni kwanza, hatua zilizofikiwa katika uchunguzi wa tukio la kupotea kwa Mdude Nyagali, na pili, kufuatilia makubaliano yao ya awali ya kushirikiana na Jeshi la Polisi katika juhudi za kumtafuta.
Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu leo Jumamosi, Mei 3, 2025, Katibu wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Hamad Mbeyale, amesema kuwa kutokana na ukimya uliokuwepo kuhusu kupotea kwa Mdude Nyagali, leo baadhi ya viongozi na wafuasi 58 wa chama hicho wamelazimika kuandamana hadi Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya.
“Tumeenda na madai mawili. La kwanza ni kuhusu makubaliano yetu na Jeshi la Polisi tuliyofikia jana, Mei 2, 2025, ya kushirikiana katika kumtafuta kamanda wetu Mdude, hasa walipokuwa eneo la tukio. Hata hivyo, hadi leo asubuhi hakuna dalili yoyote ya ushirikiano wala harakati zozote kutoka kwa Polisi,” amesema Mbeyale.
Ameongeza kuwa lengo la maandamano hayo ni kufuatilia hatima ya kupatikana kwa kada huyo, pamoja na kupata uhakika wa usalama wao binafsi katika harakati wanazoendelea nazo.
“Kwa sasa tunahitaji kujua hatima yetu. Tumeamua kuwaeleza wanachama wetu kuwa umefika wakati ambapo mtu anapojitambulisha kuwa ni askari polisi, wasitoe ushirikiano moja kwa moja, bali wawachukulie kama watuhumiwa hadi pale itakapothibitika vinginevyo,” amesema Mbeyale.
Hata hivyo, amesema wanatambua na kushukuru juhudi za Jeshi la Polisi, hususan kupitia kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, kwa kueleza kuwa uchunguzi wa kumtafuta Mdude Nyagali bado unaendelea.
Chadema wamsaka Mdude porini
Amesemawanachama na viongozi wa majimbo wameamua kuingia maporini kwa ajili ya kumsaka Mdude Nyagali, awe hai au amekufa.
“Kwa sasa tupo eneo la Mlima Nyoka, barabara kuu ya kuelekea jijini Dar es Salaam, kwani mke wake na wazazi wake wametufuata hapa kama viongozi wakihitaji kujua hatima ya mtoto wao. Pia wanasubiri kauli rasmi kutoka kwa Jeshi la Polisi kuhusu hatua zinazofuata,” amesema Mbeyale.
Awali, Jeshi la Polisi mkoani Mbeya limesema linaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu kutekwa na kupotea kwa Nyagali, huku mke wake akiomba Serikali kuingilia kati kumtafuta mumewe.
Tukio hilo linadaiwa kutokea usiku wa kuamkia Mei 2, 2025, saa 8:00 usiku, nyumbani kwao eneo la Iwambi jijini Mbeya, ambapo watu wasiojulikana walivamia nyumba ya Nyagali, kuvunja mlango na kumchukua kwa nguvu, kabla ya kutoweka naye.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo asubuhi, Jumamosi, Mei 3, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema uchunguzi unaendelea, akibainisha kuwa kikosi kazi maalumu, kikiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa (RCO), kinafanyia kazi tukio hilo.
“Tunaendelea na uchunguzi. Naomba wananchi watulie na washirikiane na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kufanikisha kupatikana kwa Mdude Nyagali na kuwabaini waliomteka,” alisema Kamanda Kuzaga.
Awali, taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilidai kuwa waliomchukua Nyagali walijitambulisha kuwa ni askari polisi, madai ambayo Kamanda Kuzaga alikanusha Mei 2, 2025.
Mke wa Nyagali, Sije Mbugi (31), amesema anaishi kwa hofu kubwa tangu mumewe alipotoweka, na kuomba Serikali na vyombo vya usalama kuhakikisha anapatikana akiwa salama.
“Naomba wanisaidie, mume wangu apatikane akiwa hai au hata kama amekosea, basi angefikishwa kwenye vyombo vya sheria, si kuchukuliwa kimyakimya. Hili linaumiza sana,” amesema Mbugi kwa masikitiko.
Crédito: Link de origem