top-news-1350×250-leaderboard-1

Chadema, Chaumma waendeleza vijembe, CCM yasimama katikati

Dar es Salaam. Vita ya hoja na vijembe imeendelea kupigwa kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kila upande ukiutuhumu mwingine kwa mwenendo usiofaa.

Chadema inautuhumu uongozi wa Chaumma kujaa usaliti, kwa kuwa wengi wao walikuwa makada wa chama hicho kikuu cha upinzani, lakini wamekihama katika nyakati ngumu, bila kujali walisaidiwaje kabla.

Kwa upande wa Chaumma, kinajibu mapigo dhidi ya Chadema kikiwatuhumu baadhi ya viongozi wake wa juu kwa tabia ya kutweza utu wa wanawake katika majukwaa ya kisiasa, huku kikiwataka watoke hadharani kuomba radhi.

Licha ya vijembe baina yao, vyama hivyo vilivyopo ziarani katika mikoa tofauti, Chadema ikiwa Dodoma na Chaumma ikiwa Geita, vyote vina uwiano wa hoja kuhusu rasilimali za nchi, vikisema wingi wake, hauakisi uchumi wa Taifa.

Katikati yao, kinapita Chama cha Mapinduzi (CCM), kinachoendelea na ziara yake mkoani Arusha, chenyewe kikisimama kati, kuwataka wananchi wawakatae viongozi wanaopandikiza chuki kwa kutumia dini.

Hayo yote yamejiri leo, Jumapili Juni 8, 2025 katika ziara za viongozi wa vyama hivyo vitatu CCM, Chadema na Chaumma katika mikoa ya Arusha, Dodoma na Geita, ikiwa ni mwendelezo wa maandalizi ya kuuza sera kuelekea uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu. Ingawa Chadema hakitashiriki uchaguzi huo kikidai kuwapo kwa mabadiliko kwanza.

Katika ziara ya No reforms no election mkoani Dodoma, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche ametupa kijembe kwa waliokihama chama hicho, akisema hakuna hata mmoja aliyewahi kuwa mbunge.

Licha ya kauli hiyo ya Heche, kati ya waliokihama chama hicho, yupo Suzan Kiwanga aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalum na baadaye wa Jimbo la Mlimba mkoani Morogoro, kadhalika Devotha Minja aliyewahi kuwa Mbunge wa Viti Maalumu.

Katika kauli yake hiyo, Heche amesema hatua ya wanasiasa hao kudai viongozi wa chama hicho wanaogopa uchaguzi sio sahihi, bali wanataka mchakato huo ufanyike katika mazingira ambayo kila atakayeshinda atatangazwa bila kujali chama chake.

“Hatuogopi uchaguzi kwani tulishakuwa wabunge, mimi nilikuwa Mbunge, Mnyika (John) alishakuwa mbunge, Lema (Godbles) alishakuwa Mbunge na Lissu (Tundu) alishakuwa Mbunge sasa tunaogopa nini, hao vikaragosi waliotoka hakuna hata mmoja aliyewahi kuwa Mbunge,” anasema.

Kinachofanywa na viongozi hao, amesema ni kutafuta mabadiliko na yakifanyika wakati wowote, wataingia kwenye uchaguzi.

Katika ziara hiyo, Heche amesema Tanzania imebarikiwa rasilimali lukuki, lakini haziakisi uchumi wake, kutokana na kuliwa na wachache.

“Tanzania ni nchi ya tatu kwa kuwa na wingi wa dhahabu duniani, lakini hakuna kinachofanyika, fikiria hata maziwa tunaagiza nje ya nchi na mwaka jana pekee zilitumika Sh24 bilioni kuagiza maziwa wakati hata Mpwapwa mna kituo cha mifugo ni kwa nini tusifanye maboresho makubwa kwenye mali zetu,” amehoji Heche.

Kwa mujibu wa Heche, umaskini unaowatesa wananchi wa Dodoma unatokana na kutokuwa na mabadiliko ya uongozi, akirejea mkoani humo tangu uchaguzi wa kwanza hakuwahi kutokea mbunge wa upinzani.

Wakati Heche akiendelea kutupa vijembe dhidi ya viongozi wa Chaumma, Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Chaumma-Bara, Devotha Minja amesema mwanasiasa huyo anajipambanua kwa tabia yake ya kutweza utu wa wanawake.

Kauli ya Devotha, inarejea kilichoelezwa na Heche alipokuwa mkoani Morogoro, akidai aliyekuwa Mbunge wa Mlimba, Suzan Kiwanga alisaidiwa na Chadema kupata ubunge, baada ya kumuona anafanya kazi za nyumbani, lakini amekosa shukurani kiasi cha kukisaliti chama hicho na kuhamia Chaumma.

Akiwa Katoro mkoani Geita katika mwendelezo wa ziara ya C4C, Devotha amesema analaani matamshi ya Heche, akimtaka ajitathimini na kujali mchango wa wanawake.

“Nilimsikiliza Heche akimshambulia Suzan, akiwa Morogoro alianza kumshambulia na kumdhalilisha eti alikuwa mama wa nyumbani, Chadema ikamuona na kumpatia ubunge, kwani mama wa nyumbani hafai kuwa mbunge?”

“(Heche) anapaswa kujitathimini na mjue chama kile kinatweza utu wa wanawake, kwani mama wa nyumbani hana mchango, ina maana unadharau kazi ya mama wa nyumbani, kama mwanamke nitasimama kupigania haki ya wanawake,” amesema.

Amekwenda mbali zaidi na kumtaka Heche ajitokeze hadharani kumwomba msamaha Suzan, kwa kuwa amefanya kazi kubwa ya kuwafundisha wengi siasa.

Mbali na hoja hiyo, Kada wa chama hicho, Edward Kinabo ametumia jukwaa hilo kueleza kukosekana mlinganyo kati ya wingi wa rasilimali za Tanzania na maendeleo yake kiuchumi.

“Tatizo lilipo ni kukosekana kwa usimamizi mzuri, Chaumma tunataka kuingia madarakani Oktoba baadaye mwaka huu moja ya kazi tunayoenda kuifanya ni kusimamia rasilimali ya madini ili wananchi wanufaike,” amesema.

Amesema iwapo watapewa ridhaa ya kuongoza nchi, watakabili rushwa na ufisadi ili kuokoa maisha ya Watanzania, kadhalika watahakikisha wachimbaji wadogo wanainuka na sio kuwa chini ya wakubwa.

Mwenyekiti wa chama hicho, Hashim Rungwe amesema bila chama mbadala matatizo ya Watanzania hayataisha kwa kuwa viongozi waliopo madarakani wamelewa.

“Tunataka kuwaletea neema Watanzania tuungeni mkono, Uchaguzi ukifika msijiulize maswali ipigieni Chaumma kwa watakao gombea ubunge, udiwani na urais tuna dhamira ya kweli kuwatatulia changamoto zenu,” amesema.

Akiwa Usariver mkoani Arusha, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amewasihi wananchi kuwakataa viongozi wanaopandikiza chuki au kuligawa Taifa kwa misingi ya udini au ukabila.

Kwa mujibu wa Makalla, ni muhimu kulinda amani kwani kwa kawaida Taifa linapoelekea kwenye uchaguzi huwa na maneno na fitina nyingi na CCM itahakikisha inashiriki uchaguzi huo kwa amani.

“Tuendelee kulinda amani tunapoelekea uchaguzi kwani kila unapotokea uchaguzi kuna maneno mengi kuna fitina nyingi, sisi CCM tunawaahidi tutailinda amani tutashiriki uchaguzi kwa amani na nyie muendelee kushirikiana na Serikali.

“Tuwakatae viongozi wenye kupandikiza chuki, hadaa, uongo, wanaotaka kuligawa Taifa kwa udini ukabila au jambo lolote,” amesema.

Katika ziara yake hiyo mkoani Arusha, Makalla amewaambiwa wananchi wa Jimbo la Hai wasirudie makosa waliyoyafanya zamani kwa kumchagua kiongozi kutoka upinzani aliyeongoza kwa miaka 20.

Kauli hiyo ya Makalla, inarejea kilichotokea mwaka 2000 hadi 2020, jimbo hilo lilipoongozwa na kada wa Chadema na Mwenyekiti wa zamani wa chama hicho, Freeman Mbowe.

“Nilikuwa Mkuu wa Mkoa jimbo hili lilikuwa upinzani ukilinganisha miaka mingi lilipokuwa upinzani na miaka michache ya CCM kuna maendeleo mengi yamefanyika. Msirudie makosa sumu haionjwi na ukibahatika ukatapishwa usirudie tena kuonja,” amesema.

Amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda kuendelea kulinda amani na utulivu wa mkoa huo ili kuendelea kuwavutia watalii zaidi.

“Ukiwa kama Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama hakikisha mkoa wa Arusha unaendelea kuwa salama watalii wamiminike mapato yamiminike ili tujenge uwezo wa Serikali kuwaletea wananchi maendeleo maendeleo,” amesema.

Aliposimama kuzungumza katika msafara huo wa Makalla, Makonda amesema jimbo hilo kuwa na changamoto za barabara na kwa mwaka huu wa fedha itajengwa kwa njia nne kuanzia Usa River hadi Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro kilomita 11.3.

Imeandikwa na Janeth Mushi (Arusha), Tuzo Mapunda (Geita) na Habel Chidawali (Dodoma).

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.