top-news-1350×250-leaderboard-1

CCT yatoa salamu za Idd El Fitr kwa Waislamu

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Moses Matonya amewataka Waislamu kuendelea kuyaishi mafunzo ya Mungu ili baraka zake ziweze kuenea kwa wengi.

Akizungumza leo katika Baraza la Idd El-Fitr lililofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam, Mchungaji Matonya amepongeza mshikamano wa kidini na kuhimiza waumini kuendeleza maadili waliyojifunza katika mfungo wa Ramadhani.

Akiangazia historia ya dini nchini, Mchungaji Matonya amesema Uislamu uliingia Tanzania karne ya tisa, ukifuatiwa na Ukristo, huku akieleza jinsi Waislamu walivyowapokea wamishionari wa Kikristo kwa moyo wa ushirikiano.

“Hii ni ishara ya mshikamano mzuri kati ya dini hizi mbili, hivyo ni muhimu kuendeleza umoja na maelewano kwa ajili ya kumpendeza Mwenyezi Mungu,” amesema.

Katika hotuba yake, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Al Haj Nuhu Mruma amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani, akisema kuwa amani ni zawadi kutoka kwa Mungu ambayo inapaswa kulindwa na kuendelezwa.

Aidha, ameeleza jitihada za Bakwata katika kuhakikisha malezi bora ya vijana kwa kuwanoa walimu wa madrasa na kuomba masomo ya dini yarasimishwe na kupewa uzito sawa na masomo mengine katika shule za awali na msingi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameahidi usalama wa wawekezaji na wafanyabiashara katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Amebainisha kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha amani inaendelea kutawala, akisema hakuna sababu ya hofu kwa wawekezaji au wafanyabiashara.

“Tunaendelea kutoa elimu kwa Watanzania kuhusu umuhimu wa amani, tukishirikiana na viongozi wa dini kuhakikisha mshikamano unadumu,” amesema Chalamila.

Amesisitiza kuwa Tanzania haina mahali pa kukimbilia iwapo amani itayumba, hivyo ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha nchi inaendelea kuwa tulivu.

Chalamila amepongeza mchango wa viongozi wa dini katika kudumisha mshikamano wa kitaifa na kuhamasisha maadili mema kwa jamii.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.