top-news-1350×250-leaderboard-1

CCM Simiyu yakerwa na kusuasua kwa ujenzi wa Veta Busega

Simiyu. Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Simiyu kimeeleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kinachojengwa katika Wilaya ya Busega kwa gharama ya Sh1.48 bilioni kwa awamu ya kwanza.

Akizungumza leo, Jumanne Aprili 8, 2025, Katibu wa CCM mkoa huo, Eva Ndegeleka, akiongoza wajumbe wa kamati ya siasa ya chama hicho ya Mkoa wa Simiyu kukagua ujenzi wa chuo hicho, amesema kuwa ujenzi huo unasuasua.

“Serikali imetoa fedha kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, lakini maendeleo ya ujenzi wa chuo hiki unasuasua, hali ambayo inatia mashaka juu ya usimamizi na utekelezaji wake,” amesema.

Hivyo, amemtaka Mkuu wa Mkoa huo, Kenani Kihongosi, kushirikiana na chama hicho ili kuwasiliana na wizara hiyo kwa ajili ya ukamilishaji wa ujenzi huo ifikapo Juni mwaka huu.

Akizungumzia hilo, Kihongosi ambaye ni mjumbe wa kamati hiyo amesema kuwa ni muhimu kwa wahusika kuongeza kasi, ili kuhakikisha kuwa ujenzi huo unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa mafunzo kwa vijana wa wilaya hiyo.

Amesema kuwa ujenzi huo una changamoto kubwa katika utekelezaji wake, licha ya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega pamoja na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo kuwa wakichukua hatua mbalimbali, ikiwemo kuwakumbusha kwa maandishi juu ya utekelezaji wake na umuhimu wa mradi huo, lakini bado kuna shida kidogo.

“Wizara wanapoleta hii miradi, wajue kuna viongozi kama Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa halmashauri kwenye eneo husika wanaopaswa kujua utekelezaji wake ili waguswe zaidi na miradi hii, kwa sababu hapa leo tunaulizana gharama ya jengo, hakuna anayejua zaidi ya wizara.”

“Hii ni changamoto, kama fedha zimeletwa zaidi ya Sh429 milioni lakini bado majengo hayajakamilika, Wizara ya Elimu wana wajibu wa kufanya, hapa, sisi kama mkoa hatujaridhika na huu mradi,” amesema.

Amesema kuwa changamoto zote zilizojitokeza, ikiwemo nondo kuoza, zinaweza kusababisha majengo kubomoka na kuitaka wizara hiyo kuhakikisha wanasaidia ujenzi wa chuo hicho unakamilika kwa wakati kwani tayari Serikali imeshatoa fedha.

Ofisa Uthibiti Ubora wa Shule wilaya ya Busega, William Thomas, akitoa taarifa ya ujenzi huo amesema lengo la mradi huo ni kupata wataalamu watakaosaidia nchi baada ya kuhitimu mafunzo ya vyuo, kuwajengea ujuzi na uwezo wa kujiajiri vijana pamoja kupunguza tatizo la ajira hapa nchini.

Amesema kuwa ujenzi wa chuo hicho ukikamilika utakuwa na majengo 18, ambapo awamu ya kwanza itahusisha majengo tisa na awamu ya pili majengo tisa, na hadi sasa Sh429 milioni zimeshatolewa.

“Jengo la utawala limefikia asilimia 50, madarasa yako asilimia 50, kuna changamoto ya ukosefu wa nondo kwa ajili ya kufunga lenta, nguzo za kunyanyua majengo ya karakana na mbao hazijaletwa ili kuendelea na upauaji wa majengo sita,” amesema.
  

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.