Bamako. Nchi za Niger, Burkina Faso na Mali zimetangaza rasmi kujiondoa katika Shirika la Kimataifa la Mataifa yanayozungumza Kifaransa la ‘Francophonie’ (OIF).
Uamuzi huo umefanywa na viongozi wa mataifa hayo yenye serikali za kijeshi, Niger inaongozwa na Jenerali Abdourahamane Tchiani, Mali inaongozwa na Kanali Assimi Goïta na Burkina Faso inayoongozwa na Kapteni Ibrahim Traoré.
Viongozi hao wamedai OIF na taasisi zingine zilizo chini ya Ufaransa ni ukoloni mamboleo.

OIF ni shirika lililoundwa kwa madhumuni ya kukuza lugha ya Kifaransa na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi zinazozungumza Kifaransa.
Gazeti la Le Monde limeripoti kuwa taarifa ya pamoja ya nchi hizo tatu ilisema kwamba OIF imegeuka kuwa ‘chombo cha kisiasa’ kinachoendeshwa na Ufaransa ili kuongeza unyonyaji wa rasilimali za mataifa hayo.
Viongozi hao wa kijeshi waliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi yakiwemo ya Mali mwaka 2020, Burkina Faso (2022) na Niger (2023), wamevunja uhusiano wa kidiplomasia na Ufaransa na yenyewe (Ufaransa) imewaondoa wanajeshi wake kwenye nchi hizo.
Taarifa ya pamoja ya viongozi hao imeeleza kuwa badala ya OIF kuziunga mkono nchi hizo katika kufanikisha matarajio halali ya wananchi wao, kwa mujibu wa malengo yake ya amani, ushirikiano na mshikamano, yenyewe (OIF) imekuwa na uamuzi wa kisasi wa kuziwekea vikwazo.
“Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS), taasisi nyingine ya kikanda inayoonekana kama chombo cha ukoloni mamboleo kinachohusiana na Ufaransa na Marekani, ilienda mbali zaidi na kuweka vikwazo vya kiuchumi vinavyodhoofisha, hata kutishia uvamizi wa kijeshi katika taifa la Niger kwa msaada wa Ufaransa mwaka 2023,” ilisema taarifa ya muungano huo.
Kwa mujibu wa Le Monde nchi hizo tatu ni miongoni mwa waasisi wa OIF.
OIF ilianzishwa mwaka 1970 katika mkutano wa viongozi uliofanyika mjini Niamey nchini Niger, kama Shirika la Ushirikiano wa Kitamaduni na Kiufundi (ACCT), ambao baadaye ulibadilishwa kuwa Shirika la Kiserikali la Dunia katika mataifa yanayozungumza Kifaransa (AIF) mwaka 1998 kabla ya kubadilishwa jina na kuwa OIF mwaka 2005.
Licha ya kuchangia katika kuimarisha shirika hilo kwa miaka 55, nchi hizo zimekuwa zikilalamika kuwa OIF ilionyesha kutoheshimu mamlaka yao kwa kuyawekea vikwazo mataifa hayo ya Afrika Magharibi.
Kwa mujibu wa taarifa ya AES, vikwazo hivyo vinavyowekwa na mataifa ya Ulaya hususan Ufaransa na Marekani, vinalenga kuleta upendeleo kwa vibaraka wa Ulaya ambao ni marais waliopinduliwa na wanajeshi hao.
Wakati wa maandamano ya kudai kuondolewa kwa wanajeshi wa Kifaransa katika nchi zao, viongozi wa sasa wa mataifa hayo wakiongozwa na Kapteni Traore na majeshi yao yaliunga mkono harakati ya kupinga ukoloni mamboleo.
“Mali haiwezi kubaki mwanachama wa shirika ambalo matendo yake hayaendani na misingi ya katiba inayozingatia mamlaka ya taifa,” ilisema taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali.
Ni watu milioni 3.7 pekee kati ya zaidi ya milioni 23 nchini Mali ndio wanaozungumza Kifaransa.
Hata hivyo, Kifaransa kilikuwa lugha rasmi hadi katikati ya mwaka 2023, wakati Serikali mpya yenye msimamo wa kutetea mamlaka ya taifa ilipopunguza hadhi yake kuifanya kuwa ‘lugha ya kazi’ huku ikipandisha hadhi ya lugha mbalimbali za Kiafrika kuwa lugha rasmi za mali.
Kuondoka kwao kunatarajiwa kuanza kutekelezwa ndani ya miezi sita. Kwa sasa, OIF ina wanachama 93. Hata hivyo, harakati za wananchi katika makoloni ya zamani ya Ufaransa ndani ya Sahel na Afrika Magharibi zinatajwa kuzidi kuimarika na tayari zimeanza kusambaa katika mataifa mengine ikiwemo Benin, Ivory Coast, Chad, na kwingineko huku ushawishi wa Ufaransa kupitia taasisi ukiongezeka.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika ya Habari.
Crédito: Link de origem