Dodoma. Bunge limepitisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2025/26 huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisema Serikali itaendelea kuhakikisha kuna hali ya usalama, amani na utulivu kipindi chote cha uchaguzi.
Ofisi hizo zimepitishiwa Sh782.08 bilioni katika mwaka huo wa fedha.
Hotuba hiyo ilichangiwa na wabunge 103 lakini Majaliwa akasema mambo mengi atayatolea majibu kwa maandishi.

Akihitimisha hoja hiyo leo Aprili 14, 2025, Majaliwa alisisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika maboresho ya awamu ya pili ya Daftari la Kudumu la Wapigakura ili wapate haki yao kwenye uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika mwisho.
Majaliwa amesema Serikali iko tayari kushirikiana na vyama vya wafanyakazi likiwamo Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), ili wafanyakazi wapate stahiki zao.
Hata hivyo, wakati wa kupitisha vifungu, hakuna mbunge aliyesimama kuhoji jambo lolote, hivyo vimepita kama vilivyoombwa.
Awali, akichangia mjadala wa bajeti hiyo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema wamekamilisha mfumo unaounganisha taarifa za Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi unaojulikana kwa jina la ESMIS.
Amesema mfumo huo utawezesha Watanzania wanaoishi Ughaibuni kuunganishiwa taarifa za benki ili marejeo ya fedha zinazoletwa nchini yaweze kujulikana.
“Hili ni moja ya jambo kubwa ambalo Bunge lako katika michango ya wabunge limeelezwa kwa kiwango cha juu sana sababu ya marejeo kidogo yanayoletwa nchini kwetu,” amesema.
“Nataka nikuhakikishie mheshimiwa spika, moja ya kipengele ambacho kimekuwa changamoto kwetu ni kukosekana kwa mfumo sahihi tunaoweza kupata taarifa sahihi ya fedha ngapi zinaletwa nchini, watu wangapi na wanafanya nini na kingapi kinachopatikana.”
Ridhiwani amesema mfumo huo utaanza kufanya kazi mwaka 2025/26.
Akizungumzia kuhusu kuhamasisha matumizi ya dawa za kupunguza makali ya virusi vya Ukimwi, (ARVs), Waziri wa Nchi katika Ofisi Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi amesema wameupokea ushauri wa wabunge wa kuongeza kasi ya kuelimisha wananchi kupima.
Pia, amesema Serikali inachukua hatua madhubuti kuhamasisha vijana kujilinda na wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU) kutumia ARVs kikamilifu.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega alisema Rais Samia Suluhu Hassan atalizindua Daraja la Kigongo hadi Busisi (JPM) lenye urefu wa kilomita tatu, Mei mwaka huu.
Ujenzi wa daraja hilo litakalokuwa la sita kwa ukubwa barani Afrika, ulianza Februari 25, 2020 na ulitarajiwa kukamilika Desemba 2024 na litagharimu Sh716.33 bilioni.
Ulega amesema Rais Samia alilikuta daraja hilo likiwa limejengwa kwa asilimia 20 tu na sasa lililopewa jina la JPM.
Akijibu hoja za wabunge kuhusu kufumua kwa barabara ya kusini, Ulega amesema wanatafuta fedha kwa ajili ya kuifumua barabara ya kwenda mikoa ya kusini, mbali ya madaraja yanayoendelea kujengwa.
“Wakati tunasubiri hayo tayari, tunayo maelekezo ya kutengeneza vipande kwa vipande hasa katika maeneo yaliyoaribika sana. Eneo la kutoka Ikwiriri, Chumbi, Marendego hadi Somanga hii ni sehemu iliyoaharibika sana,” amesema.
Amesema barabara hiyo tayari imewekwa katika mipango ya bajeti mwaka 2025/26 ili kuhakikisha wanalifanyia kazi agizo hilo la kutengeneza vipande vya barabara.
Ulega amesema kuna ujumbe unasambaa katika mitandao kuwa daraja la muda la Somanga limekatika jambo ambalo sio kweli kwa kuwa bado liko sawa.
Amesema mvua zinavyoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali na kuingiza maji katika Bahari ya Hindi, zimefanya maji yapite juu ya daraja hilo la muda.
“Na kwa msingi huo kwa ajili ya usalama wa watu, tukasema tusubiri kwanza na hiki ni kitu tunafanya maeneo mengi pamoja na Daraja la Jangwani kwa lengo la kuangalia usalama wa watu,” amesema Ulega.
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ameitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutowalazimisha wakulima kuwa na mashine za kutoa risiti za kieletroniki (EFDs) kwa sababu hakuna sheria iliyopitishwa na Bunge inayowalazimu kufanya hivyo.
Amesema sio shughuli ya wakulima wala vyama vya ushirika; na hakuna sheria iliyopitishwa na Bunge inayowalazimisha wakulima na vyama vya ushirika kuwa na mashine hizo.
“Kinachotakiwa ni kurasimisha wafanyabiashara wawe na mashine, waingie katika orodha ya walipa kodi…Niwaombe TRA wawaache wakulima wafanye kazi ya uzalishaji,” amesema.
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali imetoa Sh98 bilioni kwa Wizara ya Afya kwa ajili ya kuziba pengo la fedha zilizopangwa kupokewa kutoka nje, lakini hazijaletwa kutokana na mabadiliko ya kisera kutoka mataifa ya nje.
Bila kutaja Taifa lililobadili sera zake na kuondoa misaada, Dk Mwigulu amesema Tanzania iko imara na itaendelea kuwa imara wakati wote, hivyo wananchi wasiwe na hofu juu ya hilo.
Dk Mwigulu amesema Serikali itaendelea kutoa fedha zaidi ili kusaidia maeneo yaliyoguswa ikiwamo kusaidia fedha kwenye viwanda vya kuzalisha dawa na nyingine kupelekwa Mfuko wa Bima ya Afya kwa wote.
Crédito: Link de origem