Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuwa uchumi wa Taifa unatarajiwa kuendelea kukua kwa kasi katika robo ya pili ya mwaka 2025, ambapo ukuaji wa Pato la Taifa (GDP) unakadiriwa kufikia asilimia 6.1 kwa Tanzania Bara na asilimia 6.5 kwa Zanzibar.
Hata hivyo, Kamati hiyo imeonya kuwa kutokutabirika kwa sera za biashara na migogoro ya kisiasa duniani kunaweza kuathiri mwelekeo wa mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi, hivyo hatua zilizochukuliwa zinalenga kuilinda nchi dhidi ya athari zinazoweza kutokea.
Akizungumza leo Aprili 4, 2025 jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, Naibu Gavana wa Sera za Uchumi na Fedha, Dk. Yamungu Kayandabila, alisema Benki Kuu imeamua kuendelea na riba ya msingi ya asilimia 6.
“Kwa muktadha huu, BoT itaendelea kutekeleza Sera ya Fedha ili kuhakikisha riba ya mikopo ya siku saba baina ya benki inabaki ndani ya wigo wa asilimia 4 hadi 8. Lengo ni kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya kiwango cha muda wa kati, cha asilimia tano, sambamba na ukuaji endelevu wa uchumi,” alisema Dk. Kayandabila.
Mfumuko wa bei wapungua
Katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, Kamati imebaini kuwa mfumuko wa bei uliendelea kupungua, ambapo Tanzania Bara ilikuwa na wastani wa asilimia 3.2 huku Zanzibar ikiwa asilimia 5.1 mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 6.9 mwaka 2023. Mfumuko wa bei kwa ujumla ulishuka hadi asilimia 4.8 mwezi Februari 2025 kutoka asilimia 5.3 mwezi Januari 2025.
Kupungua huko kumechangiwa na:
- Uwepo wa chakula cha kutosha nchini,
- Kushuka kwa bei za nishati duniani,
- Utekelezaji thabiti wa sera ya fedha na bajeti.
Mfumuko wa bei unatarajiwa kubaki katika kiwango cha asilimia 3.2 katika robo ya pili ya mwaka 2025.
Sekta ya fedha yaimarika
Kwa mujibu wa Dk. Kayandabila, sekta ya fedha nchini imeendelea kuwa thabiti, ikiwa na ukwasi wa kutosha, mtaji imara na faida. Uwiano wa mikopo chechefu (NPLs) umeshuka hadi asilimia 3.6 mwezi Februari 2025, chini ya kiwango kinachokubalika cha asilimia 5.
Aidha, mikopo kwa sekta binafsi imekua kwa wastani wa asilimia 12.7, hasa kwenye biashara ndogo na za kati, kilimo, biashara na viwanda. Ujazi wa fedha pia umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 12 mwaka 2024.
Utendaji wa mapato na matumizi
Kamati imeeleza kuwa utekelezaji wa bajeti kwa robo ya tatu ya mwaka 2024/25 ulikuwa wa kuridhisha. Mapato ya kodi kwa Tanzania Bara na Zanzibar yalifikia malengo, kutokana na usimamizi bora wa mapato na matumizi ya serikali yaliyoendana na rasilimali zilizopo.
Biashara ya nje na akiba ya fedha za kigeni
Deni la serikali limeendelea kuwa himilivu huku sekta ya nje ikiimarika. Nakisi ya urari wa malipo ya kawaida ilishuka hadi asilimia 2.6 ya Pato la Taifa kufikia Machi 2025, kutoka asilimia 3.7 mwaka 2024. Zanzibar ilirekodi ziada ya dola milioni 563.5 ikilinganishwa na dola milioni 407.4 mwaka uliopita, kutokana na ongezeko la mapato ya utalii.
Akiba ya fedha za kigeni ilifikia zaidi ya dola bilioni 5.6, ikitosheleza kuagiza bidhaa na huduma kwa miezi 4.5. Shilingi ya Tanzania inatarajiwa kuimarika sambamba na kuongezeka kwa mapato ya fedha za kigeni.
Maoni ya sekta binafsi na viashiria vya kimataifa
Dk. Kayandabila alisema kuwa tathmini ya maoni ya wakurugenzi wa makampuni pamoja na taarifa ya Shirika la Moody’s ya Machi 2025 imethibitisha kuwa Tanzania bado inabaki katika daraja la B1, ikiwa na mwelekeo imara wa kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Umoja wa Mabenki Tanzania (TBA), Theobald Sabi, aliipongeza BoT kwa hatua madhubuti zilizochukuliwa kulinda uchumi wa Taifa, akisema ni ishara nzuri ya kuimarika kwa sekta ya fedha na ustawi wa uchumi kwa ujumla.
Crédito: Link de origem