Unguja. Mwakilishi wa Tunguu, Simai Mohamed Said ameishauri Serikali kutafuta taasisi inayojitegemea kufanya tathmini ya kodi zinazotozwa Zanzibar, ili kuweka usawa kulingana na matakwa ya kisiwa hicho.
Pia ameishauri Serikali kuacha kupanga kodi kwa kuangalia kodi za Tanzania bara kwani maeneo hayo yanatofautiana kwa kila kitu ikiwamo kimazingira, miundombinu na vyanzo vya mapato.
Simai ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Juni 5, 2025 wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, barazani Chukwani Unguja.
Amesema inawezekana kuna kodi ambazo hazipo rafiki zinazokwaza wafanyabiashara.
“Tutafute taasisi zinazojitegemea zikatufanyie tathmini katika kodi, maana inawezekana tukaona tupo sawa lakini hatuwezi kujipima sisi wenyewe na kujipangia tukaona changamoto,” amesema.
Pia Mwakilishi huyo ameishauri Serikali kuwa na mipango ya pamoja kuanzia ngazi za wizara kuyashusha chini ili kuwa na muunganiko wa pamoja katika utekelezaji wa miradi.
Ametolea mfano wa baadhi ya barabara zinazojengwa licha ya kuwa na pilika nyingi, lakini hakuna vituo vya daladala hivyo hatua hiyo inachangia kuongeza ajali.
Naye mwakilishi wa Fuoni, Yussuf Hassan Iddi amesema ipo haja wizara kuongeza kasi na mbinu ya kukusanya kodi kwani inaonekana kuna kiasi kikubwa hakikusanywi.
Pia ameitaka Wizara kupanga maoteo ya makusanyo kulingana na uhalisia wa makusanyo yenyewe, kwani kwa hali ilivyo sasa inaonekana maoteo yanayofanyika hayana uhalisia.
Katika kulithibitisha hilo, amesema maoteo ya makusanyo ya mwaka 2024/25 kati ya Sh4.9 trilioni iliyopangwa kukusanywa, lakini ni Sh2 trilioni pekee iliyokusanywa mpaka Machi mwaka huu sawa na asilimia 42.
“Tunakadiria makusanyo makubwa kuliko uwezo wetu, kwa hiyo ifike wakati sasa tufanye maoteo yenye uhalisia isiwe kama kujifurahisha,” amesema na kuongeza:
“Hili jambo lina athari kubwa katika mipango ya maendeleo, tumeona hapa katika bajeti za wizara, miradi inakwama kwa sababu hajaingiziwa fedha kama huku hakuna makusanyo, bajeti zinapangwa kubwa hazitekelezeki,” amesema.
Mwakilishi wa Mfenesini, Machano Othman Said amesema bado kuna mianya mingi inayotumiwa na wafanyabiashara kukwepa kodi hususan kupitia mashine za kielektroniki.
Ameishauri wizara kupitia mamlaka zinazohusika na kodi kuandaa utaratibu maalumu na kuongeza elimu kwa wananchi, ili kuhakikisha risiti zinadaiwa na wafanyabiashara wanazitoa.
Akihitimisha hoja ya bajeti hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amekubaliana na ushauri wa Simai akisema wataupeleka Serikali Kuu kuona namna watakavyoliendea jambo hilo la kuwa na taasisi huru.
Amesema kila wizara inatakiwa kuwa na utaratibu wake wa kufanya tathmini. Hata hivyo Waziri Saada amesema kila mwaka wanafanya tathmini ya kodi.
Kuhusu ukwepaji kodi, amekiri bado kuna wafanyabiashara wanafanya makusudi kwa kisingizio cha mashine kutokuwa na mtandao jambo ambalo sio kweli, kwani hata kama hakuna mtandao mashine hizo zinafanya kazi.
Amesema wizara imejipanga kuja na vyanzo vipya vya mapato vingine vitatajwa katika bajeti kuu ya Serikali, hivyo wasiwe na wasiwasi katika kupata fedha za kutekeleza miradi.
Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/26 itakusanya na kutumia Sh6 trilioni.
Crédito: Link de origem