Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Benki ya Akiba (ACB) imetoa msaada wa mahitaji mbalimbali katika kituo cha kuelelea watoto yatima cha Chakuwama kilichopo Sinza Dar es Salaam.
Akikabidhi msaada huo Machi 28,2025 Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Akiba, Dora Saria, amesema wamelenga kuboresha ustawi wa watoto na kuleta tabasamu kwenye nyuso zao.
Amesema msaada huo unaojumuisha mahitaji muhimu ya kibinadamu unaonyesha dhamira ya benki hiyo ya kusaidia watu wenye uhitaji na kujenga matumaini kwa mustakabali mwema na kwamba wanaamini katika kuunga mkono jamii na kuleta mabadiliko chanya.
“Akiba Commercial Bank tunaamini katika nguvu ya mshikamano kwa kubadili maisha. Msaada huu ni hatua muhimu ya kuhakikisha ustawi wa watoto hawa na kuleta matumaini kwa wenye uhitaji kwa maisha bora yajayo,” amesema Saria.
Mwakilishi wa kituo hicho Hassan Tabu, ameshukuru benki hiyo kwa ukarimu wao na kusema kuwa msaada huo utaboresha maisha ya watoto hao.
“Tunaishukuru sana Akiba Commercial Bank kwa kusimama nasi katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani na Kwaresma kwani kutoa ni moyo wala si utajiri waendelee hivyo na Mungu awabariki,” amesema Hassan.
Msaada huo utasaidia kukidhi mahitaji ya watoto na kuwapatia tabasamu na kupitia juhudi hizo, Akiba Commercial Bank Plc inathibitisha dhamira yake ya kuwajibika kwa jamii kwa vitendo, ikilenga kuleta mabadiliko chanya na ya kudumu kwa jamii inayoihudumia.
Crédito: Link de origem