Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Bandari Kavu ya Kwala, iliyopo wilayani Kibaha mkoani Pwani, imeanza kuhudumia wastani wa kontena 823 kwa siku, sawa na kontena 300,395 kwa mwaka, ambayo ni takriban asilimia 30 ya kontena zinazohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam kwa sasa.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amebainisha hayo leo Machi 16, 2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kutembelea mradi wa kongani ya viwanda mkoani Pwani pamoja na Bandari Kavu ya Kwala, iliyojengwa chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Msigwa alieleza kuwa ujenzi wa bandari hiyo ni sehemu ya mkakati wa kupunguza msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam. Alisema, “Lengo la bandari hii ya Kwala ni kuhakikisha wafanyabiashara wanachukulia mizigo yao hapa, kwani hata wao foleni inawakera.”
Aidha, Msigwa alitoa wito kwa uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kudhibiti malori yanayoegeshwa kiholela katika makazi ya watu, kwani yanaongeza kero na uchafuzi wa mazingira pamoja na kusababisha usumbufu kwa wananchi. Alisema, “Kwa yale yanayopaki katika makazi ya watu, ni jukumu la Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha suala hilo linadhibitiwa na kuondoa kero kwa wakazi.”
Katika ziara hiyo, Msigwa alitembelea pia Kiwanda cha San Ton Park kilichopo katika eneo hilo, ambacho kimeajiri zaidi ya vijana 1,000 na kinazalisha bidhaa kama majokofu, nguo na vifaa vingine. Alisema, “Sekta ya viwanda imeleta mapinduzi chanya kiuchumi, huku mapato yake yakifikia shilingi trilioni 2 katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na ajira zaidi ya laki tano zimeongezeka kupitia miradi mbalimbali ya viwanda.”
Msigwa aliongeza kuwa ujenzi wa bandari hiyo na nyingine zinazojengwa katika maeneo mbalimbali nchini, kama Mwanza, Isaka, Tabora na mipakani mwa nchi za Burundi, Rwanda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), utasaidia kupunguza msongamano wa shehena katika Bandari ya Dar es Salaam. Alisema, “Tukitumia hapa na bandari zetu zingine tulizozijenga Dodoma, Tabora na Mwanza, zitataua changamoto ya msongamano wa mizigo katika Bandari ya Dar es Salaam.”
Pia, alifafanua kuwa eneo la Kwala limechaguliwa kwa sababu ya ukaribu wake na barabara kuu ya Dar es Salaam na Morogoro, pamoja na reli ya kisasa (SGR), hivyo kurahisisha usafirishaji wa mizigo. Alisema, “Tumejenga bandari hii kwa ajili ya kukabiliana na msongamano katika Bandari ya Dar es Salaam.”
Msigwa alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuboresha miundombinu na mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji zaidi na kuongeza ajira kwa Watanzania.
Crédito: Link de origem