Dar es Salaam. Mjadala unaoendelea kuhusu matishio ya kiusalama yakiwemo matukio ya ama watu kutekwa au kuuawa ambayo yamezua wasiwasi nchini, umemlazimu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba kutumia hotuba ya Bajeti bungeni kuzungumzia hali hiyo kwa kina, akitoa hakikisho la vyombo vya dola kutuliza hali hiyo.
Akiangazia hali ya ulinzi na usalama nchini, Dk Mwigulu alisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama bado vina uwezo na nguvu ya kuhakikisha amani na utulivu nchini vinakuwepo, na haviwezi kushindwa kukabiliana na vitisho vinavyohatarisha maisha ya wananchi.
Katika hotuba yake, Dk Mwigulu alieleza namna vyombo hivyo vimekuwa imara katika awamu zote zilizopita, hususan wanapojitokeza watu au makundi yenye dalili za kuhatarisha usalama wa nchi.
Kauli hiyo imekuja katika kipindi ambacho baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wanahoji ukimya wa vyombo vya dola kuhusu matukio ya utekaji, wakitaka kufahamu nafasi ya vyombo hivyo katika kulinda amani na kusimamia haki kwa wote.
Juni 11, 2025, Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila alihoji suala hilo akitoa mfano kwamba kama zamani wauaji wa albino na hata waliogushi vyeti walikuwa wanapatikana haraka, kwa nini wanaoua na kuteka watu sasa hawakamatwi.
Vilevile, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Yuda Tadeus Ruwaichi katika tukio tofauti alisema ni muhimu kushughulikia mambo ya kitaifa kwa ukweli, haki na amani ili “tuweze kudai kweli kwamba sisi ni kisiwa cha amani”.
Alishauri Tanzania isijiite kisiwa cha amani kutokana na haya yanayoendelea, na wananchi wamuombe Mungu awape amani yake.
Wiki chache zilizopita, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima alizungumzia masuala ya utekaji akieleza kwamba ni jambo linaloipa sifa mbaya nchi hii, huku akisema anaamini si vyombo vya dola vinavyofanya masuala ya utekaji, kwa kuwa vyenyewe vina uwezo wa kufanya mambo yake kwa weledi.
Si hao tu, hata Askofu Mkuu Renatus Nkwande alizungumzia masuala hayo kwenye ibada ya mazishi ya Mzee Silvin Mongella, akitoa ushuhuda alivyokuwa anafuatiliwa gari fulani kwa umbali mrefu.
Akiwasilisha hotuba yake bungeni jijini Dodoma jana Dk Mwigulu alitoa rai kwa Watanzania wasiruhusu misingi na nguzo za Taifa zitikiswe na wasiingie kwenye mtego wa adui.
“Sote ni mashahidi kuwa mataifa yaliyowahi kuingia kwenye mfarakano kwa kiasi kikubwa ulisababishwa na mizaha mizaha na kutokuheshimu misingi ya kitaifa, maneno ya rejareja yasiyo na ushahidi ya mtu mmoja mmoja, yasiyo na ushahidi kwa baadhi ya taasisi zisizo za serikali na yasiyo na ushahidi kwa baadhi ya vyombo vya habari,” alisema.
Alisema wakati mwingine uhalifu wa mtu mmoja mmoja au vikundi hujitokeza na kuwa tishio kwenye maisha ya kila siku ya wananchi.
Akitoa mifano, alisema katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tatu, walijitokeza wahalifu ambao walikuwa wanateka magari ya mizigo na mabasi ya abiria katika maeneo mbalimbali nchini. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vilisimama imara na kukomesha uhalifu huo.
Aidha, alisema katika kipindi cha Serikali ya awamu ya nne, ulitokea uhalifu wenye sura ya ugaidi uliohusisha urushwaji wa mabomu kwenye nyumba za ibada, mikusanyiko ya watu na mashambulizi ya mtu mmoja mmoja wakiwemo watu wenye ulemavu wa ngozi.
Katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tano, amesema ulitokea uhalifu wa watoto kutekwa na kuuawa, mtu mmoja mmoja kupigwa risasi kwenye makazi yake au katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Mtakumbuka, waliuawa wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa wanaotokana na CCM na tulishuhudia pia miili iliyokuwa kwenye magunia na mifuko ikiwa imetupwa baharini. Na haya tumesahau? Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vilisimama imara na kukomesha uhalifu huo,” alisema.
Alisema hata sasa vimejitokeza viashiria vya uhalifu kama huo, ambavyo havipiganwi kwa kupeleka vikosi na kampeni au kusema tunapigana vipi.
Alionya kwamba Watanzania wakiendelea kunyoosheana vidole, vyombo vya ulinzi na usalama vitaacha adui aendelee na uhalifu.
“Vita vya aina hii vinapiganwa kwa intelijensia, hivyo niwasihi Watanzania wenzangu, tuviache vyombo vya ulinzi na usalama vifanye kazi yake na tuendelee kufanya kazi kwa maendeleo ya Taifa letu,” alisema Dk Mwigulu.
Aliongeza kuwa: “Wakati mwingine uchochezi wa adui huwa ni kwa lengo la kuzifikia rasilimali nyingi au za kipekee zinazopatikana katika Taifa husika.
Tunayo mifano yote ikiwemo ya mataifa yaliyokuwa na migogoro iliyochochewa na waliotamani kupora rasilimali hizo na pindi zilipoisha, migogoro nayo iliisha huku mataifa hayo yakiachwa masikini.”
“Tumeshuhudia uchochezi katika mataifa mengine ukijipenyeza nyakati za uchaguzi kupitia wananchi kuchukiana wao kwa wao au wao na Serikali zao. Sote tuwe macho!” ameonya Dk Mwigulu katika hotuba yake ya bajeti.
Waziri huyo amesema Watanzania hawana Taifa lingine zaidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wala hawana mbadala wa amani, usalama, utulivu na Muungano wao.
Amewataka watambue kuwa, kinacholengwa ni rasilimali zao na sifa ya kipekee ya Tanzania kuwa kisiwa cha amani. Amewataka Watanzania kuilinda amani yao, ikituponyoka ni vigumu kuirejesha.
Kwa upande wa awamu ya sita, Dk Mwigulu alisemaSerikali imeendelea kuhakikisha kuwa mipaka yote ya nchi inakuwa salama, pamoja na kuwepo kwa umoja, amani, mshikamano na utulivu.
Alisema Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeendelea kutoa mchango kwa kushiriki katika operesheni mbalimbali za ulinzi wa amani kupitia misheni za Umoja wa Mataifa na jumuiya za kikanda.
“Ninavipongeza vyombo vyetu vya ulinzi na usalama chini ya Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan kwa jitihada kubwa zinazoendelea kuchukuliwa ili kuhakikisha hali ya ulinzi, usalama, amani na utulivu inaendelea kuimarika,” alisema Dk Mwigulu.
Akizungumzia eneo hilo la hotuba ya Mwigulu, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Magdalena Sakaya amesema alikuwa na shauku ya kusikiliza bajeti kutokana na mambo mawili; kujua itakujaje na hali ya kisiasa, kwa kuwa wengi wanaona nchi ipo kwenye hali tete.
“Sikuona kauli yenye nguvu kuashiria hali halisi ya Taifa hapa tulipo, waziri alikuwa anachombeza tu kwamba haoni shida, lakini uhalisia ukoje? Tuna hali gani? Haoni yote hayo, hakutoa kauli ya kiongozi, haya yanayoendelea hayamhusu au kwa kuwa yeye yuko salama?” amehoji Sakaya alipozungumza na Mwananchi leo Juni 13, 2024.
Alisema alitarajia bajeti ingetoa sauti ya kiutendaji, ingetoa kauli yenye nguvu maana Watanzania hawako salama, watu wanapotea, hawaonekani, wengine wanatekwa.
“Tungesikia kauli kama Taifa, ni hatua zipi zinachukuliwa, labda katika bajeti hii kinaundwa kikosi maalumu kufanya uchunguzi wa kina kubaini watekaji wako wapi,” amesema.
Amesema alitegemea waziri atasema kama mipaka iko salama, wanaoteka watu ni watu wanaokuja na kuondoka au wapo ndani?
“Nilitegemea bajeti ingekuja tofauti kutokana na mazingira tunayoyaona, lakini imekuwa kinyume na matarajio, swali la kujiuliza ni kwamba; watu wanatekwa, wanaoteka wako wapi?” amehoji Sakaya.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Ramadhani Manyeko amesema pamoja na waziri kueleza hivyo, wananchi wengi hawaoni jitihada za dhati katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kuwajibishwa kwa wahusika.
“Kuna matukio mengi yanatokea ya utekaji na watu kupotea, lakini hatuoni uwajibikaji. Imezoeleka mtu akishindwa kutimiza wajibu wake, anatakiwa kuwajibika lakini hatuoni,” amesema huku akimtaka Mwigulu asiseme tu, wakati wananchi hawaoni uwajibikaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza), Profesa Mohamed Makame amesema alimsikiliza waziri katika hotuba yake, alifanya rejea ya matukio kama hayo (ya utekaji, mauaji) katika nyakati tofauti za utawala.
“Alisisitiza kuwa katika kipindi chote, vyombo vya ulinzi vilisimamia kurejesha amani na kuleta hali utulivu na kuwa hivi sasa kuna wimbi la mawazo na kauli za watu, ambazo pengine zinachochewa na kuwa ni kipindi cha uchaguzi,” amesema.
Amesema sheria za nchi zipo na zinatumika na kubainisha kuwa mambo ya ulinzi na usalama yana nidhamu na taratibu zake.
“Wananchi ni vema kupaza sauti zao kwa njia ya ustaarabu na ya misingi ya sheria, si kujibebesha kazi za mamlaka. Wanachopaswa kufanya wananchi ni kutoa taarifa za matukio hayo na vyombo vipewe nafasi ya kufanya kazi yake,” amesema Profesa Mohamed.
Crédito: Link de origem