top-news-1350×250-leaderboard-1

Baada ya TLP na SAU, Mgaywa aibukia ADC kuwania urais

Unguja. Mwanasiasa Mutamwega Mgaywa, baada ya kugombea urais wa Muungano mara mbili bila mafanikio kupitia vyama vya Tanzania Labour Party (TLP) na Chama cha Sauti ya Umma (SAU), sasa ameibuka kupitia Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) na tayari amechukua fomu za kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Hayo yamesemwa jana Juni 5, 2025 wakati watia nia ya kugombea nafasi za urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mgaywa na mtia nia wa urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Hamad Rashid Mohamed walipokuwa wakirejesha fomu za kuomba kuteuliwa na chama chao kuwania nafasi hizo katika ofisi kuu za chama hicho zilizopo Unguja.

Mwaka 2010, kupitia TLP, Mgaywa alijikita katika sera za kilimo, elimu, afya na utawala bora kama misingi ya kuboresha maisha ya wananchi na kuleta maendeleo ya taifa.

Katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, Mgaywa aligombea urais kwa tiketi ya SAU, akisisitiza sera za kilimo zenye lengo la kumkomboa mkulima na kuongeza tija ya uzalishaji.

Jana Mgaywa ametangaza sera zake kwamba anapanga kuanzisha bima ya afya kwa wote na kuboresha huduma za elimu na afya kwa kutumia madini kama dhahabu na chuma.

Pia, atapunguza matumizi ya Serikali kwa kuuza magari ya kifahari ya viongozi na kununua magari ya gharama nafuu kwa wakuu wa wilaya na mikoa, ili kuokoa fedha na kuwahudumia wananchi vyema.

Mgaywa anasema Tanzania ni nchi tajiri, lakini mipango mibovu imezuwia maendeleo na kupanua umasikini.

Kwa upande wa mtia nia wa urais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Hamad Rashid Mohamed amesema iwapo wataingia madarakani, ndani ya siku 100 za kwanza wataanzisha mchakato wa kuandaa katiba mpya kwa kuwasilisha andiko kwa wananchi na kuendesha mchakato shirikishi.

Amesisitiza kuwa wananchi ndio wataamua, huku Serikali ikitoa elimu na kusikiliza maoni yao.

Kuhusu maudhui ya katiba mpya, Hamad amesema; “Wala hili hupaswi kuumiza kichwa, kwani tayari zipo takribani tume tatu kuna tume ya Jaji (Francis) Nyalali, tume ya  Jaji (Robert) Kisanga na tume ya Jaji (Joseph) Warioba ambayo ilikuja kupigilia msumari , hizi tume zote zimeeleza kwa uwazi na uzuri kwa hiyo tayari tuna pahali pa kuanzia kilichopo ni kutekeleza matakwa hayo.”

Amesema iwapo wataingia madarakani, Serikali yake itahakikisha wakulima wanapewa pembejeo bure kwa kipindi cha miaka miwili ya awali ili kuimarisha kilimo, sekta ambayo ni mhimili wa uchumi na chanzo kikuu cha ajira kwa Watanzania wengi.

Hamad anagombea urais wa Zanzibar, mara ya kwanza aligombea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa tiketi ya ADC ingawa hakushinda, alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi huo.

Mwaka 2020, aliteuliwa kuwa Waziri wa Afya wa Zanzibar chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoongozwa na Rais Hussein Mwinyi wa CCM.

Awali, Katibu Mkuu wa Chama cha Alliance for Democratic Change (ADC), Mwalim Hamad Azizi, alieleza kuwa bado kuna nafasi kwa wanachama wanaotaka kuchukua fomu za kugombea urais, huku akibainisha kuwa zoezi hilo litahitimishwa rasmi tarehe 11 Juni 2025.

“Baada ya kufungwa kwa mchakato huo, sekretarieti ya chama itakutana Juni 12, na kufuatiwa na Mkutano Mkuu utakaofanyika Juni 14 jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kupitisha rasmi majina ya wagombea,” amesema Hamad.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.