top-news-1350×250-leaderboard-1

Askofu Mwamakula awasihi viongozi wa dini kukemea uovu bila hofu

Singida. Askofu Emmaus Mwamakula amewasihi viongozi wa dini zote nchini kutumia nafasi zao kuonya na kukemea uovu katika jamii kwa sababu hilo ni miongoni mwa wajibu na jukumu lao kwa jamii.

Akihutibia mkutano wa hadhara mjini Singida leo Juni 9, 2025, Askofu Mwamakula amesema pamoja na mahubiri na mafundisho ya kiimani, kukemea uovu, kushauri na hata kukemea kwa faida na manufaa ya jamii ni miongoni mwa wajibu muhimu wa viongozi wa dini.

“Viongozi wa dini zote nchini walikuwa sehemu muhimu wakati wa mapambano ya kudai uhuru kwa kusimama kidete kupinga udhalimu wa Serikali za kikoloni; hata leo, viongozi wa dini bado tunao wajibu huo wa kukemea uovu na uonevu katika jamii. Tufanye hivyo bila hofu, uonevu wala upendeleo kwa mtu wala kundi lolote,” amesema Askofu Mwamakula.

Huku akitaja majina ya baadhi ya viongozi wa dini akiwemo Desmon Tutu wa Afrika Kusini, Askofu Mwamakula amesema Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere alipata msaada wa hali na mali ukiwemo ushauri kutoka kwa viongozi wa dini zote nchini.

“Tofauti na ukweli huo, tumeanza kuona mashambulizi ya maneno na hata kuumizwa mwilini dhidi ya viongozi wa dini wanaojitokeza kukemea, kuonya na kushauri kuhusu maovu yanayotokea nchini vikiwemo vitendo vya watu kutekwa, kushambuliwa na baadhi kupotezwa,” amesema Askofu Mwamakula.

Ametoa mfano wa tukio la kushambuliwa kwa Katibu wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki (TEC), Padri Charles Kitima kuwa miongoni mwa vitisho dhidi ya viongozi wa dini wenye uthubutu wa kupaza sauti kukemea maovu yanayotokea katika jamii.

Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), Deogratius Mahinyila ameutumia mkutano huo kuipongeza na kuushukuru umma kwa kuunga mkono kampeni ya kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi kwa kusambaza kaulimbiu ya ‘No reforms, no election’ kupitia mitandao ya kijamii.

“Mwamko wa Watanzania kusambaza kaulimbiu ya No reforms, no election kupitia mitandao ya kijamii ni ishara ya umma kuelewa na kukubali hoja ya Chadema ya mabadiliko kuweka sawa uwanja wa siasa kwa wagombea na vyama vyote vya siasa. Haya ni mafabikio makubwa katika madai ya haki na demokrasia kwa wote,” amesema Mahinyila.

Kiongozi huyo ambaye ni wakili kitaaluma, amesema Chadema inaendelea kudai mabadiliko ya sheria na mfumo wa uchaguzi kutokana na mabadiliko madogo yaliyofanyika kuacha mianya ya uonevu dhidi ya wagombea na vyama vya upinzani.

Amesema mabadiliko hayo bado yanatoa mwanya kwa watendaji na watumishi wa halmashauri ambao wengi wao ni makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kusimamia uchaguzi.

“Vyama vya upinzani tulikuwa tunalalamikia mawakala wetu kunyimwa fomu za viapo na matokeo ya kura katika vituo vya kura; sheria imebadilishwa ambapo sasa msimamizi wa uchaguzi ndiye atawasilisha fomu za viapo huku fomu za matokeo ya kura ikitolewa kwa hisani iwapo vitakuwepo. Haya marekebisho yamekuwa mabaya kuliko hata yale tuliyolalamikia,” amesema Mahinyila.

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Magharibi, Dickson Matata ameunga mkono ubaya wa mabadiliko ya Katiba na sheria ya uchaguzi akitolea mfano Ibara ya 74 (12) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kinachokataza kuhoji mahakamani utendaji na maamuzi ya Tume Huru ya Uchaguzi (INEC).

Matata ambaye ni wakili kitaaluma amesema Ibara ya 74 (11) ya katiba hiyo pia inaipa INEC mamlaka ya kutekeleza shughuli zake bila kuzingatia wala kusikiliza ushauri kutoka chombo, taasisi wala wadau.
Xx

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.