Dar es Salaam. Wakati wiki ya Azaki mwaka huu ikitarajiwa kufanyika Juni, moja ya jambo litakaloangaliwa ni njia gani zinaweza kutumika ili waweze kufikia malengo yao hasa katika kipindi hiki cha uwapo wa tishio la kusitishwa kwa misaada kutoka nje.
Hili linakwenda kufanyika wakati ambao Marekani imeendelea kuweka vibano na kusitishwa kwa misaada kwenda nchi mbalimbali hasa baada ya kuchaguliwa kwa Rais wa nchi hiyo, Donald Trump.
Kukatwa kwa misaada hii kumefanya baadhi ya mashirika yaliyokuwa yakidhaminiwa na Marekani kutofanya kazi kama ilivyokuwa awali jambo ambalo limefanya baadhi ya watu kupoteza kazi zao.
Wiki ya Azaki mwaka huu inafanyika Juni tofauti na mara nyingi ilipokuwa ikifanyika Oktoba kutokana na kuwapo kwa uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani.
Hayo yamebainishwa jana usiku wakati wa uzinduzi rasmi wa wiki wa Azaki uliofanyika jijini hapa ambao uliwakutanisha wadau mbalimbali wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ili kujadili vitu mbalimbali kuelekea maandalizi ya wiki hiyo.
Akizungumza, Mwenyekiti wa Kamati ya Asasi za Kiraia, Nesia Mahenge amesema
wanafahamu kuwa katika kipindi cha uendeshaji wa mashirika kunaweza kuwa na uhaba lakini hilo ni moja ya jambo ambalo wamekubaliana halitawarudisha nyuma.
“Huwa kuna msimu ambao una uhaba, msimu huu usitutoe katika reli badala yake tuangalie yale yaliyofanywa ndani ya nchi na sisi kama sekta hasa katika kushughulikia matatizo mbalimbali na changamoto ya sasa matokeo yake,” amesema.
Amesema katika kutambua hili, kipaumbele cha kwanza kinachowekwa ili kusaidia asasi za kiraia ni kujijeneana uwezo ndani ya wiki hiyo ili kuhakikisha wanakuwa na ustahamilivu wa hali ya juu kwa kuwa na mbinu za uchangiaji shughuli mbalimbali ambazo zitawawezesha kupata mapato endelevu.
“Lengo la hiki ni kuhakikisha huduma mbalimbali zinazotolewa zinaendelea. Ni changamoto katika upande mmoja, matokeo yake yameathiri maeneo mengi na si tu Tanzania lakini kama nchi ni wakati wa kusimama imara kusaidiana pamoja ili kuvuka hapa,” amesema Nansia.
Akizungumzia wiki ya Azaki amesema mbali na mengi yatakayozungumzwa pia watatathmini kazi ambazo mashirika ya kiserikali yamefanya ikiwemo matokeo chanya na maendeleo yaliyofikiwa Tanzania.
Huu ukiwa ni mwaka wa nane wa wiki hii kufanyika pia amesema zipo faida nyingi ambazo zimepatikana ikiwemo kufanya kazi mbalimbali za jamii nchini.
“Tulikuwa tukifanya wiki hii Dodoma na tukahamia Arusha kutokana na mapendekezo ya wananchi wenyewe na jamii kwani mashirika haya yako maeneo ambayo jamii ipo, badala ya kufanya mkoa mmoja wananchi waliomba tuwe tunazunguka ili kuleta mwamko wa kisekta katika eneo linaloweza kufikiwa na watu wengi,” amesema.
Mkurugenzi wa Shirika la Mfuko wa Asasi za Kiraia (FCS), Justice Rutenge amesema serikali za nje sasa haziamini mashirika yasiyokuwa ya kiserikali.
Kufuatia hilo amesema kazi kubwa ambayo inapaswa kufanyika ili kujua ni namna gani wanaweza kuhakikisha shughuli zao zinaendelezwa hata katika nyakati hizi.
“Huu ni wakati ambao tunatakiwa kuinuka na kuonyesha kuwa tunaweza kuvuka mazingira haya mazingira ambayo ni magumu kwa sekta yetu,” amesema.
Amesema jambo la muhimu linalopaswa kufanyika kwa wakati huu ni ushirikiano ndani ya sekta.
Wiki hii inafanyika wakati ambao nchi mbalimbali ikiwemo za Afrika zimeendelea kukabiliana na sheria mbalimbali zinazowekwa na Rais Donald Trump ikiwemo fedha za afua mbalimbali ikiwemo Ukimwi.
Crédito: Link de origem