top-news-1350×250-leaderboard-1

Almasi ya Sh1.7 bilioni yakamatwa ikitoroshwa Mwanza

Mwanza. Madini ya almasi yenye thamani ya zaidi ya Sh1.7 bilioni yamekamatwa yakitoroshwa nje kupitia uwanja wa ndege wa Mwanza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Mwanza usiku wa Mei 23, 2025, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema madini hayo yalikamatwa Mei 18, 2025 kwa ushirikiano kati ya vyombo vya ulinzi na taasisi mbalimbali za Serikali.

Amesema raia wa kigeni ambaye hakumtaja jina anashikiliwa kwa mahojiano na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo

“Uchunguzi wa kina unaendelea kubaini mtandao wa wanaohusika na utoroshaji kuwezesha hatua za kisheria dhidi ya wote, ikiwemo kufikishwa mahakamani, kutaifisha madini na kuwafutia leseni,” amesema Mavunde.

Katika kikao chake kilichofanyika saa 5:00 usiku katika Ukumbi wa mikutano Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Waziri Mavunde amesema vitendo vya kutorosha madini siyo tu ni kosa la jinai, bali pia vinaikosesha Serikali mapato kupitia kodi na ushuru mbalimbali.

Amesema Serikali imeboresha biashara ya madini kwa kufungua masoko 43 na vituo 49 vya kuuza na kununua madini kote nchini; hivyo hakuna sababu ya watu kutumia njia za panya kuuza na kununua madini.

“Wasiotaka kufuata sheria kwa kutorosha madini wanakabiliwa na hasara kadhaa ikiwemo kutiwa mbaroni, kushtakiwa, madini yao kutaifishwa na kufutiwa leseni. Tutawafutia leseni na kuwazuia kujihusisha na shughuli yoyote ya madini watu wote watakaobainika kujihusisha na utoroshaji wa madini nje ya nchi,” amesema Mavunde.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde akitoa taarifa ya kukamatwa madini ya almasi yaliyokuwa yakitoroshwa kupitia uwanja wa ndege wa Mwanza, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema Wizara ya Madini imeunda kikosi kazi maalumu kukabiliana na utoroshaji wa madini na tayari imefanya kazi eneo la Tunduru na sasa inaelekea eneo la  Nyamongo kwa kazi ya usimamizi wa biashara ya madini.

Waziri huyo amesema udhibiti wa biashara ya madini umesaidia ongezeko la makusanyo ya mapato kupitia sekta hiyo kutoka zaidi ya Sh162 bilioni mwaka wa fedha wa 2015/16 hadi kufikia zaidi ya Sh753 bilioni kwa mwaka wa fedha wa 2023/24.

“Mwaka huu tuna malengo ya kukusanya Sh1 triolini na hadi kufikia sasa tayari tumekusanya zaidi ya Sh925 bilioni,” amesema.

Waziri Mavunde ameupongeza uongozi wa Serikali Mkoa wa Mwanza, uongozi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza, ofisi ya madini, vyombo na taasisi za Serikali mkoani humo kwa mikakati madhubuti ya kukabiliana na vitendo vya kutorosha nje madini.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda ameahidi kuwa ofisi yake kwa kushirikiana na vyombo na mamlaka nyingine za Serikali itaendelea kuziba mianya yote za kutorosha nje madini.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.