Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imemhukumu kunyongwa hadi kufa mfanyabiashara Khamis Luwonga baada ya kupatikana na hatia ya kumuua mkewe Naomi Marijani na kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa.
Hukumu hiyo imetolewa leo Februari 26,2025 na Jaji Hamidu Mwanga wa Mahakama Kuu baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Akisoma hukumu hiyo Jaji Mwanga amesema upande wa mashitaka umethibitisha bila kuacha shaka yoyote kwamba mshtakiwa alimuua mkewe na alifanya hivyo kwa makusudi.
“Baada ya kuangalia vielelezo vinaunga mkono stori nzima ya namna tukio la mauaji lilivyotokea. Baada ya tukio kutendeka mshtakiwa alimkunja marehemu kwenye shuka mbili kisha akaupeleka mwili kwenye banda la kuku alikokuwa amechimba shimo.
“Akamkalisha kisha akachukua gunia mbili za mkaa na kumchoma na akahakikisha kila kitu kinateketea halafu mabaki akayapeleka na kwenda kuyafukia shambani kwake.
“Kitendo hiki si cha kibinadamu, kinanifanya niseme alifanya kwa kudhamiria huyu mtu ateketee kabisa…tukio lilifanyika akiwa na akili timamu,” amesema Jaji Mwanga.
Upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ashura Mnzava, umeiomba mahakama mabaki ya mwili wa Naomi yakabidhiwe kwa ndugu zake ili wafanye mazishi kwa kuwa hakupewa haki ya maziko.
Wakili anayemtetea mfanyabiashara huyo, Precious Hassan, amesema wanakusudia kukata rufaa kutafuta haki zaidi katika mahakama za juu.
Naye baba mdogo wa marehemu, Robert Marijani, amesema wameridhika na hukumu iliyotolewa na mahakama na wanasubiri mabaki ya mwili wa mtoto wao ili wafanye maziko.
Luwonga alipandishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam Julai 30,2019 kipindi hicho akiwa na umri wa miaka 38, akishtakiwa kwa kosa moja la mauaji ya mkewe Naomi eneo la Gezaulole, Kigamboni.
Crédito: Link de origem