Arusha. Tamaa mbaya, ndivyo unavyoweza kusema kilichomkuta mkazi wa eneo la Chemchem wilayani Kondoa Mkoa wa Dodoma, Rashid Kimolo, aliyembaka bibi mwenye umri wa miaka 68.
Kama haitoshi baada ya kumaliza kumfanyia bibi huyo ukatili huo, inadaiwa alilala mtupu bila kuvaa nguo kitandani kwa bibi huyo. Kwa mujibu wa maelezo, bibi huyo alitoka nje na kwenda kutoa taarifa kwa majirani, waliokwenda kumkamata mtuhumiwa huyo aliyekutwa amelala chumbani humo akiwa mtupu.
Mahakama ya Rufani Tanzania iliyoketi Dodoma na kutoa hukumu yake Machi 19,2 025 imebariki kifungo cha miaka 30 alichohukumiwa Rashid.
Katika rufaa hiyo ya mwaka 2023, hukumu ilitolewa na majaji watatu, Winfrida Korosso, Sam Rumanyika na Abdul-Hakim Amer Issa.
Hii ni rufaa yake ya pili kukwaa kisiki ambapo ya kwanza aliikata Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, hivyo inamaanisha Rashid amefikia mwisho wa kupigania haki kwani ndiyo ngazi ya mwisho ya rufaa.
Majaji hao walieleza kuwa kesi ya upande wa mashitaka imethibitishwa bila kuacha shaka na kuwa mrufani ndiye aliyembaka bibi huyo, na ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa pili ulioaminika katika mahakama mbili za chini na hakukuwa na ushahidi mwingine wa kuupinga.
Kuhusu hoja ya mrufani kulala eneo la tukio, majaji hao walieleza suala hilo liliisumbua Mahakama pia kwani siyo kawaida mkosaji kubaki eneo la tukio baada ya kufanya uhalifu.
“Kwa kawaida angekimbia, lakini mambo ya ajabu yalitokea na mrufani akakutwa amelala kwenye eneo la tukio na kulikuwa na mashahidi wawili wa kuaminika waliomwona pale, kwa hiyo, hatuna sababu ya kutilia shaka ushuhuda wao, tunaona sababu hii haina mashiko na tunaitupilia mbali,” amesema Jaji Issa.
Kuhusu kutokuwepo eneo la uhalifu siku ya tukio, majaji hao wameeleza Mahakama Kuu ilizingatia utetezi kwenye ukurasa wa 29 wa kumbukumbu na kubaini kuwa, utetezi wa mrufani kutokuwepo eneo hilo haikuungwa mkono na ushahidi wowote na ilitolewa bila taarifa kinyume na kifungu cha 194 (4) cha CPA, na kuutupilia mbali.
“Katika hitimisho letu, tunakubaliana shahidi wa kwanza alibakwa bila ridhaa yake na mrufani ndiye aliyembaka. Kwa hiyo hii rufaa inatupiliwa mbali kwa ujumla wake,”amehitimisha Jaji Issa
Kulingana na ushahidi wa mwathirika wa tukio hilo ambaye alikuwa shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, alisema kuwa siku ya tukio Februari 11, 2021 katika eneo hilo la Chemchem, usiku alisikia kelele kutoka kwenye chumba kingine.
Alisema alichukua taa inayotumia umeme wa jua na kwenda kuangalia, alipofungua mlango wake alikutana uso kwa uso na mrufani ambaye alikuwa amevaa kaptula na fulana ya kahawia.
Alisema bila kusema neno lolote, mrufani alishika shingo yake na kutupa taa hiyo, kisha akamshika na kumpeleka kitandani ambapo alimvua nguo ya ndani, kisha akambaka na alivyokidhi haja yake alilala akiwa mtupu kitandani hapo.
Mwathirika wa tukio hilo alisema mrufani alipolala, yeye aliinuka na kwenda kutoa taarifa kwa majirani.
Shahidi wa pili, Mwanahamisi Bakari, aliyekuwa jirani yake, alisema aliitikia wito huo na alipoenda kimyakimya nyumbani kwa bibi huyo alimkuta mrufani akiwa mtupu kitandani na amelala fofofo ambapo alichukua baadhi ya picha.
Alisema baadaye mumewe alifika eneo la tukio, kisha wakatoa taarifa kwa balozi wa nyumba kumi na mrufani akakamatwa eneo la tukio.
Shahidi wa tatu ambaye ni ofisa Polisi Grayson, alisema Februari 16, 2021, alirekodi maelezo ya onyo ya mrufani ambapo alikana kutenda kosa hilo.
Katika utetezi wake, mrufani huyo alikana kutenda kosa hilo na kudai siku ya tukio alilala nyumbani kwake na kuwa alikamatwa soko la zamani akiwa katika shughuli zake za kila siku.
Baada ya mahakama kusikiliza pande zote mbili iliridhika kwamba upande wa mashitaka umethibitisha kesi bila kuacha shaka, kumtia hatiani na kumuhukumu adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela.
Baada ya kutoridhishwa na uamuzi huo alikata rufaa ya kwanza Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma ambayo iliitupilia mbali rufaa yake.
Katika rufaa hiyo alikuwa na sababu 13 ikiwemo kutokana na mikanganyiko, ushahidi usiolingana na madhubuti wa upande wa mashitaka, kesi hiyo haikuthibitishwa bila kuacha shaka.
Nyingine ni kwamba kulikuwa na ukiukwaji wa kifungu cha 10(3) na 9(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Mahakama ya rufaa ya kwanza ilishindwa kutathmini ukweli wa ushahidi wa shahidi wa kwanza na pili na kuwa hukumu hiyo ilitokana na ushahidi dhaifu.
Sababu nyingine ni mahakama ya kwanza ya rufaa (Mahakama Kuu) ilishindwa kuzingatia jinsi mrufani alivyobaki eneo la tukio baada ya kutenda kosa.
Rashid ambaye hakuwa na uwakilishi wa wakili alieleza kuwa anaunga mkono hoja hizo na kuiomba mahakama izingatie sababu zake za kukata rufaa huku Jamhuri ikiwakilishwa na mawakili wawili.
Mawakili hao walipinga rufaa hiyo ambapo moja ya sababu anazolalamikia mrufani huyo ni picha zinazodaiwa kupigwa akiwa mtupu katika nyumba ya bibi huyo kutowasilishwa mahakamani, mawakili hao walieleza kuwa hakuna sharti la kutoa picha hizo kama vielelezo ili kuthibitisha kesi ya ubakaji.
Walidai kiongozi aliyechukua picha hizo hakushuhudia kutendeka kwa kosa hilo, na alimshuhudia mrufani akiwa amelala kwenye kitanda cha bibi huyo na kuwa hoja hiyo ilithibitishwa na mashahidi waliomuona mrufani akiwa amelala kwenye kitanda hicho.
Crédito: Link de origem