top-news-1350×250-leaderboard-1

AKU yaanzisha shahada mpya ya uzamili kwa wauguzi

Dar es Salaam. Katika hatua ya kihistoria inayolenga kuboresha utoaji wa huduma ya afya ya msingi nchini, Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) kimezindua programu ya kwanza wa Shahada ya Uzamili kwa wauguzi nchini.

Hatua hiyo inaendeleza dhamira ya taasisi hiyo ya kuboresha huduma za afya kupitia wataalamu waliobobea, wenye utu, na wanaojali jamii.

Uzinduzi umefanyika leo Mei 31, 2025 ukiambatana na kufunguliwa kwa Kituo cha Ubunifu wa Elimu ya Tiba (CIME) chenye miundombinu ya kisasa kitakachoziba pengo kati ya nadharia na vitendo kwenye elimu ya afya nchini.

Uamuzi wa AKU kuja na programu hiyo unakuja wakatia ambao Tanzania inapanua wigo wa uboreshaji wa miundombinu ya afya. Hata hivyo, uhaba wa wataalamu waliobobea hasa maeneo ya vijijini bado unatishia kuharibu mafanikio hayo.

Utambulisho wa Mpango wa Uuguzi wa Vitendo vya Juu (APN) wa AKU, ni hatua muhimu na imekuja wakati mwafaka.

“Huu si tu programu ya Shahada ya Uzamili ni harakati ya kubadili namna wauguzi wanavyoonekana, kuthaminiwa, na kupewa uwezo ndani ya mfumo wetu wa afya,” anasema Naibu Makamu Mkuu wa AKU, Profesa Eunice Pallangyo.

Kwa mujibu wa Profesa Pallangyo, darasa la kwanza la APN tayari lina wauguzi 15 waliodahiliwa, wakiwemo viongozi, na kundi jingine 15 likitarajiwa kujiunga hivi karibuni.

Amesema miongoni mwao ni wataalamu kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, pamoja na wakuu wa uuguzi wa mikoa na wilaya mbalimbali jambo linaloonyesha kiwango cha wataalamu wanaotafuta mafunzo ya juu ya uuguzi.

“Tumezalisha viongozi wengi wa juu wa uuguzi nchini Tanzania, kuanzia mkurugenzi wa zamani wa huduma za uuguzi kitaifa hadi wakuu wa hospitali muhimu wote ni sehemu ya urithi wetu.” amesema Profesa Pallangyo.

Amesema dira ya AKU inaendana moja kwa moja na vipaumbele vya Taifa vya kuimarisha huduma ya afya ya msingi ambayo ni ngao ya kwanza kwa mamilioni ya Watanzania.

Amefafanua kuwa mpango wa APN umeundwa kuhimiza ubora wa kitaalamu na uongozi, ukilenga kuwaandaa wauguzi kuchukua majukumu mapana katika kliniki za jamii, hospitali za mikoa, na taasisi za kitaifa za afya.

Rais wa AKU, Dk Sulaiman Shahabuddin amesema  kituo cha kwanza nchini cha ubunifu wa elimu ya tiba kwa vitendo.

Amesema kituo hicho kinachanganya teknolojia, mafunzo kwa kutumia mazingira halisi (simulation), na elimu ya pamoja baina ya fani mbalimbali, yote yakilenga kuakisi ugumu halisi wa kuhudumia wagonjwa.

“Watu milioni nane hufariki kila mwaka katika nchi zenye kipato cha chini kutokana na sababu zinazozuilika.Asilimia 16 ya vifo hivyo vinatokana na mapungufu ya uongozi na ushirikiano miongoni mwa wahudumu wa afya. CIME na mpango wa APN vinakabiliana moja kwa moja na changamoto hizi.” amesema Shahabuddin 

Naibu Mkurugenzi wa Elimu ya Juu katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Kenneth Hosea aliyezindua mchakato huo amesema,” hii ndio hasa aliyoielekeza Rais Samia Suluhu Hassan, elimu inayozingatia ujuzi na kujibu mahitaji halisi,”

Dk Hosea aliisifu AKU kwa kuendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 (iliyorekebishwa mwaka 2023), ambayo inasisitiza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi pamoja na maboresho ya mitaala ili kuendana na soko la ajira.

Amesema wizara iko tayari kushirikiana na taasisi kama AKU katika kuziba mapengo ya rasilimali watu katika sekta ya afya.

“Tumeshajenga vituo zaidi ya 1,800 vya afya kupitia awamu ya tano na sita ya uongozi wa serikali, lakini vingi havitumiki kikamilifu kwa sababu ya uhaba wa wataalamu waliobobea. Baadhi ya vituo vya vijijini, vifaa vimewekwa lakini hakuna aliye na ujuzi wa kuvitumia, mpango huu ndio suluhisho.” amesema.

“Aga Khan si hospitali tu ni uwanja bora wa mafunzo, nimeweza kushuhudia ubora wake. Tunaishauri AKU kuongeza idadi ya wanafunzi huku ikidumisha ubora wake uliotukuka.” amesema.

Mshauri mwandamizi wa afya kutoka Mwanza, Dk Miriam Mponda amesema,” wauguzi ndio uti wa mgongo wa mfumo wetu wa afya. Wakiwa na ujuzi na mamlaka sahihi, wanaweza kuongoza kliniki, kushughulikia magonjwa sugu, na kupunguza msongamano hospitalini.”

Dk Mponda amebainisha kuwa mpango huo unavunja mitazamo ya kijamii kuhusu uuguzi mara nyingi huonekana kama taaluma duni kulinganisha na fani nyingine za tiba.

“Unainua taaluma ya uuguzi hadi pale inapostahili kuwa taaluma ya uongozi, maamuzi ya kitabibu, na mguso mkubwa kwa jamii,” amesema.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.