Unguja. Wizara ya Afya Zanzibar imetiliana saini mkataba wa makubaliano na Taasisi ya Aga Khan kuhusu ushirikiano katika mapambano dhidi ya magonjwa ya saratani kwa wananchi wa Zanzibar.
Akizungumza baada ya utiaji saini wa mkataba huo Machi 24, 2025 Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui amesema mkataba huo utafanya kazi kwa miaka minne kisiwani humo.
Amesema kupitia mkataba huo Zanzibar itafaidika na hisa yake, ikiwemo kupatiwa gari ya matibabu ya maradhi hayo kwa kuwafanyia uchunguzi wananchi wa vijiji tofauti Unguja na Pemba, mafunzo kwa wafanyakazi na watoa huduma katika jamii.
“Mkataba huo ni hatua muhimu ya Serikali ya Ufaransa ya kuipatia msaada wa mradi wa mapambano ya maradhi ya saratani kwa nchi za Afrika Mashariki, ikiwemo Kenya na Tanzania,” amesema Mazrui.
Waziri Mazrui amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kuimarisha huduma za maradhi ya saratani hapa nchini.
Amesema, wizara hiyo inaendelea kuwapatia mafunzo watoa huduma ili waweze kukabiliana na maradhi ya saratani ambayo ni tatizo linaloendelea kuongezeka.
Pia, amesema ipo haja ya kuwa na hospitali maalumu ya maradhi hayo, ili kuondokana na usumbufu kwa wananchi wanaohitaji huduma mbalimbali.
Meneja mradi mtambuka wa saratani kwa Afrika Mashariki, Dk Sara Jenifa Maongezi amesema mradi huo una malengo makuu manne, ikiwemo kuwajengea uwezo watoa huduma wa afya katika kukinga na kugundua mapema maradhi hayo.
Malengo mengine ni kutoa elimu ili kuhakikisha kuwa jamii inakuwa na uelewa kuhusiana na maradhi hayo na kuhakikisha kunafanyika tafiti ambazo zinalenga maradhi hayo kwa Afrika ya Mashariki.
Dk Sara amesema jambo lingine watahakikisha jamii inapata uelewa wa maradhi hayo na kuwafikia watoto ambao wana umri wa miaka tisa, kwa ajili ya chanjo ya kuwakinga dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi.
Katibu Mkuu wizara hiyo, Dk Mngereza Mzee Miraji amesema kuwa ni mafanikio makubwa kuja kwa mradi huo utakaowezesha kupambana na maradhi ya saratani nchini.
Amesema ifikapo mwaka 2029 kupitia mradi huo yatakuwa yamekamilika, yakiwemo masuala ya matibabu ya maradhi hayo.
Crédito: Link de origem