top-news-1350×250-leaderboard-1

Afariki kwenye ajali ya moto akiwa kibandani

Njombe. Mkazi wa mtaa wa sekondari uliopo kata ya Maguvani halmashauri ya mji wa Makambako wilayani Njombe,  Yohana Kilowoko (37) amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Mei 26, 2025 baada ya kulala na jiko la mkaa kwenye chumba ambacho amekuwa akifanyia biashara na kusababisha nyumba kuwaka moto.

Hayo yamesemwa leo Mei 26,2025 na Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Sekondari, Nsangalufu Mwakasumbula wakati akizungumza na waandishi wa habari huko Makambako wilayani Njombe.

Amesema saa tisa usiku alipigiwa simu na majirani wa marehemu kuwa kuna ajali ya moto, alipofika eneo la tukio licha ya kufanikiwa kuuzima moto huo lakini walichelewa kumuokoa Kilowoko, kwani walikuta ameshafariki.

Amesema baada ya kuuzima moto huo na kuingia ndani walikuta jiko la mkaa kwenye chumba hicho ambacho marehemu alikuwa amelala kwa ajili ya kulinda bidhaa alizokuwa akiuza ambazo ni mahitaji mbalimbali ya nyumbani. Hata hivyo bidhaa hizo  zote zimeteketea kwa moto.

“Hatukufanikiwa kuokoa maisha yake kwa kweli alikuwa amekwisha kabisa wataalamu wa zimamoto wametuambia ni jiko ndiyo limesababisha moto huo,” amesema Mwakasumbula.

Amewataka wananchi kulingana na hali ya baridi ilivyo sasa waache mazoea ya kukaa na jiko la mkaa (kigae) ndani kwani kinaweza kusababisha ongezeko la kabon diokside na kusababisha kukosekana oksijeni na kupoteza maisha.

Balozi wa nyumbani 10 katika eneo hilo, Daina Sambala amesema wananchi wajisitiri kwa makoti na mashuka mazito na kuacha matumizi ya majiko ya mkaa katika kuzuia baridi.

“Watu wengi wanapenda kujikinga na baridi kwa kutumia moto kwa sababu wanahisi ni njia rahisi lakini hii pia ni njia ya hatari zaidi” amesema Sambala.

Kaka wa marehemu huyo,  Oscar Kilowoko amesema taarifa za kifo cha ndugu yao amezipata kwa majirani na marehemu ameacha watoto wawili na mjane mmoja.

“Nimepigiwa simu usiku nikaja eneo la tukio nikakuta mdogo wangu amelala hapo amekufa nimeambiwa kwamba ni moto kinachoendelea kwa sasa ni maandalizi ya mazishi yatakayofanyika kesho” amesema Kilowoko.

Naye mkaguzi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Makambako,  David Ngulo amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa baada ya uchunguzi wamebaini chanzo ni moto ambao umesababishwa na jiko la mkaa, ambalo marehemu aliingia nalo kwenye chumba ambacho amekuwa akifanyia biashara.

“Ni kweli taarifa tumepata leo asubuhi saa 2:38 asubuhi kutoka kwa askari mwenzetu wa Jeshi la Polisi tulipata nafasi ya kwenda kufanya uchunguzi lakini kisababishi cha ndugu yetu kupoteza maisha ni kigae na kilichomuua zaidi ni moshi alikosa hewa safi na kupoteza nguvu akashindwa kujitetea” amesema Ngulo.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.