top-news-1350×250-leaderboard-1

ACT-Wazalendo yasema hakuna kukata tamaa

Dar es Salaam. Licha ya changamoto zinazojitokeza, Chama cha ACT-Wazalendo kimesema mapambano yataendelea na hakuna kukata tamaa.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Aprili 12, 2025 mkoani Songwe na kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu katika kongamano la nne la operesheni linda demokrasia lilofanyika mkoani humo.

Semu amesema: “Tunawajua maadui wa demokrasia, mtaji wao mkubwa ni hofu kuwatisha Watanzania, kuwavunja moyo na kuwafanya wakate tamaa.

“Lakini leo, mbele yenu, nasema wazi: Hatutakubali hofu iwe silaha yao! Tutapinga ukandamizaji kwa uasi wa haki, uasi wa wajibu, uasi wa imani yetu katika demokrasia ya kweli,” amesema.

Kuhusu maono kwa Tanzania ya kesho, Dorothy amesema wanachotaka ni demokrasia inayothamini kura ya kila Mtanzania, uchaguzi huru na wa haki na viongozi wanaochaguliwa kwa ridhaa ya wananchi, siyo kwa jeuri ya dola.

Kupitia operesheni hiyo, chama hicho kimeweka wazi madai sita ya msingi yanayoweza kutekelezwa sasa, ikiwa kuna utashi wa kisiasa.

Madai hayo ni makamishna wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) wajiuzulu na wateuliwe wapya kwa mujibu wa sheria ili kurejesha imani katika uchaguzi.

“Mawakala wa vyama wawe huru, wasitishwe. Wawe na haki ya kutekeleza majukumu yao bila kubughudhiwa na kupata fomu za matokeo bila vizuizi,” amesema.

Madai mengine ni wagombea wasienguliwe kwa sababu alizozitaja kuwa za kipuuzi, makosa ya kiufundi yarekebishwe kwa haki siyo kuenguliwa, kura haramu zidhibitiwe, uchaguzi uwe safi, bila wizi wa kura.

Kwa upande wa wakurugenzi wa halmashauri, amesema wasiwe wasimamizi wa uchaguzi, bali uchaguzi uendeshwe na watu huru.

“Vyombo vya ulinzi visihusike na uchaguzi, Polisi na jeshi viwe vya kulinda siyo kutisha wananchi. Madai haya si magumu yanahitaji tu uamuzi wa kisiasa,” amesema.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.