top-news-1350×250-leaderboard-1

ACT-Wazalendo, CCM Zanzibar hapatoshi | Mwananchi

Unguja. Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo (Taifa), Othman Masoud Othman amesema haki na maendeleo ya kweli havitapatikana iwapo wananchi wa kisiwa hicho hawatafanya uamuzi wa kubadilisha viongozi walipo kwa sasa kisiwani kupitia uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

Wakati Othman akisema hivyo, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kauli zinazotolewa na chama hicho ni za kujifurahisha kwani kimefanya kazi kubwa kuhakikisha maendeleo yamepatikana ambayo hayahitaji kuelezwa na wananchi wamekikubali hivyo wataendelea kushika dola.

Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ametoa kauli hiyo Mei 2, 2025 akiwahutubia wanachama, wafuasi na wananchi katika viwanja vya mpira vya Azimio, Mkoa wa Kusini Pemba, akiwa ziarani.

Amesema kutokana na ukweli kwamba viongozi wanaotokana na CCM siyo tu hawapo kwa ajili ya masilahi ya umma, bali pia wameshindwa kuwaletea maendeleo wananchi kwani Zanzibar ni tajiri na ina rasilimali nyingi.

“Ndugu zangu tunasema huu ni mwaka wa kuinusuru Zanzibar, ni kwa maana kwamba tuondokane na matatizo yanayoendelea ikiwamo dhuluma,” amesema.

Othman amesema wanapaswa kuweka mazingira mazuri ambayo wananchi pamoja na vizazi vijavyo wataishi kwa amani, heshima na usalama. Pia, maendeleo yanayoleta hadhi na matumaini ya maisha kwa watu wote bila ya ubaguzi.

Ametoa wito kwa wananchi wote kuendelea kuunga mkono harakati za kudai mageuzi, akiwaambia wasije kuwaangusha Wazanzibari katika kutekeleza azma yao hiyo.

Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa ametahadharisha wananchi wa Pemba wasikubali kudanganywa kwamba kisiwa hicho kimefunguliwa.

Amesema ufunguzi wa kweli utapatikana chama hicho kitakaposhika dola baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

“Tunaambiwa Pemba imefunguka, tusikubali ghiliba hizi, kuna mabadiliko gani mnayaona hapa? Pemba itakuja kufunguka kweli baada ya ACT kushika hatamu na hilo linakwenda kutimia katika uchaguzi mkuu Oktoba, mwaka huu,” amesema.

Akizungumzia kauli hizo, Katibu wa Kamati Maalumu ya NEC ya CCM, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo Zanzibar, Khamis Mbeto amesema wanajifurahisha kwani mambo yanayofanyika chini ya utawala wa CCM hayahitaji kusimuliwa bali kila mmoja anashuhudia kwa macho yake.

Mbeto amesema kauli zinazotolewa na chama hicho zinaonyesha kimekosa sera, baada ya vitu vingi kutekelezwa na CCM hivyo hawana tena mbadala wa hoja.

Amesema ili chama chochote cha siasa kikubalike na kiweze kushinda lazima kiwe na mikakati imara na kuwashawishi wananchi kwa sera nzuri na imara, vitu ambavyo CCM kimefanya kwa kuleta maendeleo na si maneno ya majukwaa ya kisiasa.

Kwa mujibu wa Mbeto, CCM kinaamini kimefanya kazi kubwa ya mikakati ya kimageuzi kuelekea maendeleo ya kweli Zanzibar.

“ACT wasema wamefanya nini kuwatumikia wananchi, kwa sasa kimebaki kulitumia jina la Maalim Seif Sharif Hamad kama mtaji wa kisiasa, huko tumeshatoka wananchi wanataka kuona kwa vitendo na CCM kweli kimetenda na miradi mingi inaonekana, sasa hizo kauli za dhuluma ni porojo za majukwaani,” amesema Mbeto.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.