top-news-1350×250-leaderboard-1

Joto la uchaguzi, UWT Tanga yatoa onyo kwa wenye wagombea mfukoni

Handeni. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Handeni, Sophia Masimba, ametoa onyo kwa baadhi ya wajumbe wa jumuiya hiyo kuacha kuwachafua wabunge na madiwani waliopo madarakani, ikiwa ni mpango wa kuanza kuunda timu za wagombea wao kwenye uchaguzi ujao.

Kauli ya mwenyekiti huyo inakuja baada ya kudai kuwa wapo baadhi ya wanachama wa CCM waliyoanza kujitokeza kutaka kugombea nafasi za ubunge na udiwani, ambapo wanawatumia viongozi wa mashina na kata wa chama ili kuanza kuwanadi kwa wenzao.

Amesisitiza kwamba yupo mmoja wa wanachama anayetajwa kuanza kujinadi hadharani bila woga, na akiendelea kufanya hivyo ataripoti na kuitwa kwenye kamati ya maadili kujieleza kwa nini anajinadi kabla ya muda, wakati wenzake wapo madarakani na wanatakiwa kuendelea kutekeleza majukumu yao.

Akizungumza kwenye kikao maalumu cha baraza hilo cha kujadili ujenzi wa nyumba za makatibu wa jumuiya za CCM, kilichofanyika leo Jumatatu, Machi 10, 2025, wilayani Handeni, mwenyekiti huyo amesema wanaofanya hivyo wanafuatiliwa, kwani kuna taarifa ya kuandaa wagombea wao.

Amesema kwa kiongozi yeyote wa jumuiya hiyo ni marufuku kumchafua mbunge au diwani wa eneo lake, kwani wao walishiriki kama wajumbe kwenye mchakato wa kuwaweka madarakani. Amehoji iweje leo waanze kuwapaka matope kuwa hawafai?

Mwenyekiti huyo amesema viongozi hao kutoka ngazi ya mashina na kata ndio wanaodiriki kuwachafua madiwani na wabunge kwa lengo la kuwawekea mazingira mazuri wanachama wanaotaka kugombea, jambo ambalo bado halijafika muda wake.

Amesema haiwezekani leo wabunge na madiwani waliopo kwenye maeneo yao wachafuliwe, ilhali wajumbe hao ndio waliowapitisha kugombea nafasi hizo.

“Mbunge mbaya tulimuweka sisi, mbunge mzuri tulimuweka sisi, diwani mbaya tulimuweka sisi wenyewe, kwani sisi ndio tulikuja na wajumbe na kupiga kura. Sasa ninachosema, kiongozi yoyote wa kata atakayediriki kumchafua kiongozi wa Chama cha Mapinduzi, ikiwa wewe ni kiongozi wake, sitocheka naye,” amesema Mwenyekiti Masimba.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Handeni, Amiri Changogo, akiwa kwenye kikao hicho, amewataka wajumbe wa jumuiya hiyo ya wanawake kuacha tabia ya kugombanishana na kuchukiana.

Amesisitiza umuhimu wa kuambiana ukweli pale inapobidi, kwani chama kinaitegemea jumuiya ya wanawake kutokana na kuwa na wanachama wengi, hasa wanawake.

Amesema kama kuna changamoto ni vema wajumbe hao wakakaa pamoja na kuanza kuzijadili kwa kutafuta njia ya kuzitatua, badala ya kuleta ugomvi na chuki, jambo ambalo linaweza kusababisha mpasuko ndani ya CCM.

Mjumbe wa mkutano huo na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Mwanaisha Ulenge, amewataka wajumbe wenzake kujikita kwenye shughuli za kiuchumi, ili kuepuka kudanganyika kwa kupewa fedha na wagombea.

Amesema mwanamke akiwa na kipato, itamsaidia kujiendeleza kiuchumi na kufanya shughuli zake kwa uhuru, bila shinikizo linaloweza kusababisha misukosuko, hata katika ndoa zao.

Amekiri kuwa si jambo jema kwa viongozi wa chama kuwachafua wenzao waliopo madarakani, kwani wao walihusika katika mchakato wa kuwaweka madarakani.

Kumekuwa na ongezeko la joto la uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, ambapo viongozi waliopo madarakani wamekuwa wakituhumu wenzao kuanza kunyemelea nafasi zao.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.