Mwanza. Tatizo la utelekezaji wa familia limeendelea kuwa mjadala usio na jawabu la moja kwa moja, huku pande zote mbiliwanaume na wanawake zikirushiana lawama.
Kila kundi lina sababu zake, likidai kuwa upande mwingine ndio chanzo cha changamoto hii inayozidi kuathiri jamii.
Wanawake wanaamini kuwa mzigo wa lawama unapaswa kubebwa na wanaume, wakidai kuwa wao ndio hutoweka na kuziacha familia zikiteseka bila msaada wowote wa kifamilia au kifedha. Kwa upande mwingine, wanaume nao hawako tayari kubeba lawama zote, wakieleza kuwa mazingira wanayowekewa na wake zao ndiyo yanawasukuma kuondoka. Wanasema wanakumbana na manyanyaso ya ndoa, huku watoto wakipandikiziwa chuki dhidi yao, hali inayowafanya wajione hawana nafasi katika maisha ya familia zao.
Kwa mtazamo huu wa pande mbili, swali linalosalia ni nani hasa anayestahili kubeba lawama katika suala la utelekezaji wa familia na namna gani suala hili linaweza kuepukwa?
Hoja ya mtazamo wa wanawake, imeibuliwa pia na Dk Tulia Ackson, Spika wa Bunge aliyesema baadhi ya wanaume hawawajibiki ipasavyo kwenye malezi na makuzi ya watoto, jambo linalochangia vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Dk Tulia alitoa kauli hiyo Machi 5, 2025 wakati akifungua kongamano la maadhimisho ya siku ya wanawake mkoani Mbeya.
Katika hoja hiyo, alisema itakuwa ndoto kwa jamii kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia iwapo wanaume watakaa pembeni na kuiachia Serikali na wanawake pekee, jukumu la malezi na makuzi ya familia.
Ili kupata suluhisho, alisema muhimu wanaume wakashiriki kikamikifu katika malezi na makuzi ya familia, hasa kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Anachoeleza Dk Tulia, kinashabihiana na kilichotokea mkoani Simiyu, ambapo wanaume wanalalamikiwa kwa kuzitelekeza familia, kama anavyoeleza na Ofisa Maendeleo ya Jamii wa mkoa huo, Fadhili Wilhelmi.
“Wanaume wengi wanashindwa kuhimili mzigo wa kifamilia kutokana na matatizo ya kifedha… hivyo hutafuta njia ya kukwepa majukumu hayo hali hii inawaacha wanawake na watoto katika hali ya umasikini na mateso ya kiuchumi,” amesema Wilhelmi.
Kutokana na hilo, ofisa huyo amesema ofisi ya ustawi wa jamii imeanza kuendesha kampeni ya elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kutimiza jukumu la malezi, makuzi na kuhudumia familia.
Mzigo kama huo, unawashukia pia wanaume katika Manispaa ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga wakitajwa kuwa vinara wa kutelekeza familia, kwa mujibu wa Abrahamani Nuru, ofisa ustawi wa jamii wa manispaa hiyo.
Nuru anataja mila na desturi zisizofaa, ugumu wa maisha, kukosa kipato cha uhakika, kujihusisha kimahusiano na wanawake wengi, kuzaa watoto wengi na kutowajibika ipasavyo kuwa ni baadhi ya sababu za hali hiyo.
“Asilimia kubwa ya kesi tunazopokea wanaume wanaongoza kwa kutelekeza familia. Unakuta mtu ana mahusiano mengi, anazaa huku, anazaa kule halafu anategemea wale watoto watahudumiwa na mama zao na wakati huohuo anaangalia mwanamke mwenye kipato, anajiweka pale,” amesema Nuru.
Wanaume wajitenga na lawama
Wakati mzigo wa lawama ukielekea kwa wanaume, wenyewe wamejitenga na hali hiyo, kama anavyoeleza Fredy Mwaisumo anayeishi Mbeya, kuwa hadi wakati mwanaume anaikimbia familia yake, kuna mambo mengi anayapitia ndani ya nyumba, ambayo si rahisi mtu wa nje kuyajua.
“Mwanamke akiwa na uchumi mkubwa kuliko mwenza wake, hutoa lugha ngumu na kuwapa maneno ‘yenye sumu’ watoto… “huna mchango wowote” na wakati mwingine anakuita mwanaume suruali,” amesema Mwaisumo.
Gubu na kelele ndani ya ndoa ni sababu nyingine zinazotajwa na Yesia Joram, pia mkazi wa jijini Mbeya, kuwa ni chanzo cha wanaume kuzikimbia familia au kuanzisha familia nyingine kutafuta faraja.
Vilevile, hulka ya baadhi ya wanawake kudai haki sawa na wanaume ni suala linayotajwa na mkazi wa Kahama, Nelson Nicholaus kuwa miongoni mwa sababu zinazoibua migogoro ndani ya familia na kuwakimbiza wanaume nyumbani.
“Tunatelekeza familia baada ya kuona mwanamke hajui mipaka yake, wanatuvimbia na shida hapa nadhani hakuna mafunzo sahihi kabla ya kuingia kwenye ndoa kama ilivyokuwa zamani. Hivi sasa mnakutana tu hapohapo mnaanza maisha na kuzaa watoto,” amesema Nicholaus.
Lakini kwa upande wake George Jisabo, mkazi wa mji mdogo wa Lamadi wilayani Busega, anataja mila na desturi inayowapa wanawake jukumu la malezi ya watoto, kuwa inachangia baadhi ya wanaume kutozingatia malezi na makuzi kwa watoto.
“Baadhi ya wanaume hudhani jukumu lao ni kutafuta riziki pekee, wakiamini malezi ya kwa watoto ni jukumu la mama,” anasema.
Suala jingine linaiobuliwa na Frank John Mkazi wa Kinondoni jijini Dar es Salaam, anasema: “Unajua wanawake, unaweza kufanya kila kitu kwa watoto, lakini makelele hawaachi na haya makelele ndiyo yanawafanya baadhi wanaume kuacha kutoa matumizi na kuwatelekeza watoto.”
Ushuhuda wa waliotelekezwa
Akitoa ushuhuda wa matokeo ya hali hiyo, Joyce John, mama wa watoto watatu anayeishi Bariadi mkoani Simiyu, amesema alitelekezwa na mumewe yeye na wanawe na anadhani sababu ni mume kukimbia majukumu.
“Mume wangu alishindwa kuhudumia watoto, akaamua kuondoka hivyo inabidi nipambane mwenyewe kuhakikisha maisha yanaendelea,” amesema.
Mwingine mwenye ushuhuda huo ni Ashura Juma, anayedai mumewe alimtelekeza baada ya kuanzisha mahusiano na mwanamke mwingine mwenye uwezo wa kifedha.
“Mwanzoni mume wangu na huyu mwanamke walijifanya ni ndugu ambao wanatoka kijiji kimoja huko Tabora, nilimwamini na tukawa tunatembeleana, hata hivyo niliona mume wangu amezidisha mazoea na yule mama nilipomuuliza akakataa kuwa mahusiano naye,” amesema Ashura.
“Siku moja mume wangu akaniaga anasafiri kibiashara, wakati huo mimi tayari nilishapata taarifa kuwa hiyo safari ni ya uongo, asubuhi yake nikajifanya nakwenda kumtembelea yule mwanamke nyumbani kwake, ghafla nilikuta shati na suruali ya mume wangu zikiwa zimefuliwa na kuanikwa kwenye kamba, yule mwanamke aliponiona akajifanya amepata dharura akafunga mlango na kuniaga,” anasema.
Mbali na wawili hao, Angela Joseph amesema kwa sasa wanaume wengi wanakimbia familia zao kwa sababu ya ugumu wa maisha na kwamba wamekuwa wakikimbilia kwa wanawake wanaojiweza kiuchumi.
“Wanaume wengi wana tamaa ya kupata maisha mazuri bila kufanya kazi, wanatafuta wanawake wenye fedha na wakati mwingine mpaka wanaoa, lakini cha kushangaza ‘nyumba ndogo’ zikishawatema wanarudi kwa wenza wao wa awali,” amesema.
Hata hivyo, Kuluthum Abdi mkazi wa Kange mkoani Tanga, amesema baadhi ya wanawake wamekosa shukurani kwa kile wanachopewa na wenza wao kama malezi ya familia, ndio sababu wanaachiwa watoto.
“Utakuta mwanaume anafokewa, hadi analazimika kuacha kutoa huduma na baadaye mnakwenda kushtakiana. Na ukikutana na jeuri, hata umshtaki na fedha hatoi. Ni vizuri na sisi pia tubadilike,” amesema Kuluthum.
Mkuu wa dawati la jinsia na watoto Dk Mwanaidi Lwena amesema madhara ya wanaume kutelekeza familia zao ni pamoja kuongezeka kwa watoto wa mitaani.
“Tunafahamu baba ndio kiongozi na nguzo kwenye familia ikitokea ameondoka nyumbani, tena kwa migogoro, mama lazima ayumbe kimaisha na hasa kama hana shughuli ya kumwingizia kipato hapo sasa ndio watoto wataanza kuhangaika mtaani kujitafutia riziki na wengine kujiingiza kwenye tabia na mienendo michafu,” amesema.
Viongozi wa dini watia neno
Ili kuondokana na hayo, Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Amani, Maswa, Damiano Makala amesema wanaume wana wajibu wa kulea familia na asiyefanya hivyo “ni zaidi ya asiyemwamini Mungu.”
“Malezi ya watoto ni ya baba na mama maana hao ndiyo waliowaleta duniani na hata Bibilia inasisitiza katika kitabu cha kwanza cha Timotheo (5:8) kinachoeleza: ‘Lakini mtu yeyote asiyewatunza walio wake, na hasa wale wa nyumbani mwake mwenyewe, ameikana imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini,” amesema.
Si Biblia pekee, hata cha Qur’an Tukufu inaeleza wajibu wa mwanaume katika familia na inalaani utelekezaji familia, kama inavyofafanuliwa na Sheikh wa Wilaya ya Maswa, Issa Eliasa.
“Katika Qur’an, Suratuh An-Nisa 4:34 inaeleza wanaume ni walinzi wa wanawake, kwa kuwa Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yao juu ya wengine na kwa kuwa wanatoa mali zao,” amesema.
Sheikh Eliasa anaungwa mkono na mwenzake wa Wilaya ya Kahama, Alhaj Omary Damka kuwa katika Uislamu mwanaume ndiye mwenye jukumu la kuitunza familia, hivyo anapoitelekeza anatenda dhambi mbele za Mungu.
Amesema suala la kuoa ni hiari na mwanaume ndiye anayeshawishi kumuoa mwanamke kwa kumlipia mahari, hivyo inapotokea akaitelekeza familia, ni kosa katika dini hiyo.
“Uislamu umegawa majukumu ya kuiangalia familia upande wa mwanaume na majukumu yanaanzia wakati wa kuoa na mwenye jukumu la kumpatia mwenzake kitu cha kumfanya kukubali kufunga ndoa ni mwanaume, ndiye anatakiwa kutoa mahari licha ya kuwa wote wanaoana,” amesema.
Amesema Uislamu umeenda mbali zaidi hadi kutoa jukumu la kunyonyesha mtoto kwa mwanaume na mwanamke anaruhusiwa kumuuzia maziwa mumewe kwa ajili ya kunyonyesha watoto.
Kwa mtazamo wake, Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Kahama, Amos Paulo amesema si sawa mwanaume kutelekeza watoto au kutoa talaka, akidokeza yote hayo yanasababishwa na wengi wao kuwa na vipato duni visivyotosheleza mahitaji.
“Msisitizo mkubwa kwa sisi viongozi wa dini Biblia inasema kwenye kitabu cha Waefeso 5:25: Enyi waume wapendeni wake zenu kama Kristo alivyolipenda kanisa, unaanza kugundua kwamba mwanaume atakapompenda mwanamke atampenda na mtoto wake,” amesema.
Sababu wanaume kunyanyaswa
Mtaalamu wa Saikolojia, Silvest Mwashuya amesema mifumo ya maisha ndiyo inayosababisha wanaume wanyanyaswe na wenza wao ndio sababu wengi wanazikimbia nyumba.
Pamoja na kuzitelekeza familia, amesema mazingira hayo huwasababisha baadhi ya wanaume hata kuingia kwenye ulevi au uraibu wa dawa za kulevya au kujidhuru.
“Pia kuna athari kwa mwanamke iwapo mwenza wake ataondoka anakosa ulinzi, hali ambayo humkwamisha katika malezi na matunzo ya watoto,” amesema.
Mtaalamu wa mahusiano na maisha, Mwalimu Yatabu amesema mtoto anajifunza zaidi kwa kuona kuliko kusikia na kwamba wanawake wengi wanaoshindwa kuishi na wenza, ni kwa sababu nao walilelewa na mama pekee.
Amesema kwa sababu wakati mwanamke huyo anakua, akili yake inamweleza kwamba hata yeye anaweza kuishi bila mume na akafanikiwa.
Amesema mtoto wa kiume anayelelewa na mama anakua na upungufu, ikiwemo kudeka kwa sababu mama alimdekeza na hata alipokuwa akifanya makosa kwenye jamii alimtetea, akiona ndio upendo kumbe anaharibikiwa hadi ukubwani.
Yatabu amesema mara nyingi wazazi wa kike wanakuwa na maneno makali ambayo mtoto hukua nayo akilini na baadaye kutengeneza chuki kwa baba zao na jamii kwa ujumla, hivyo kushindwa kuwa hata kiongozi kwa sababu alilelewa kibinafsi.
“Na kama mtoto huyu ni wa kiume ataona nimelelewa na mama peke yake na sijawahi kuona mfano mzuri wa baba nyumbani, kwa hiyo anaona kama hakuna sababu ya kuoa.
Kama mtoto wa kike pia amelelewa na mama peke yake, na namna ya maneno pia mzazi anayotoa yanamuathiri mtoto kwa sababu mtoto anahitaji apate asilimia 50 kwa mama na 50 kwa baba haijalishi nini wazazi wote watatoa kwa watoto wao,” amesema.
Naye, Mwalimu wa saikolojia, Lucas Gabriel amesema moja ya athari ya wanawake kutelekezwa ni pamoja na kushuka kwa hali ya maisha ya familia.
Imeandikwa na Saada Amir (Mwanza), Hawa Mathias (Mbeya), Amina Mbwambo (Kahama), Samwel Mwanga (Simiyu), Hamida Sharrif (Morogoro) na Rajabu Athuman (Tanga).
Crédito: Link de origem