Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
Chama Cha ACT Wazalendo, kimejivunia msingi na sera yake inayohakikisha mwanamke analindwa na aina zote za unyanyasaji wa kijinsia unaotokea katika siasa na jamii.
Akizungumza wakati wa hafla ya maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani iliyokwenda sambamba na utoaji wa tuzo mbalimbali Machi 8, 2025 iliyoandaliwa na Ngome ya Wanawake ya ACT Wazalendo jijini Dar es Salaam, Kiongozi wa Chama hicho Dorothy Semu amesema wanamchukulia mwanamke kama sehemu bora ya kujenga Taifa na chama cha siasa.
“Sisi kipekee tumeamua kuwa chama ambacho kinaheshimu nafasi ya mwanamke na kinamuona kama sehemu bora ya kujenga Taifa na Chama cha siasa. Hatumuono mwanamke kama sehemu ya kusherehesha au kupiga kura pekee,” amesema Dorothy.
Ameeleza kuwa kutokana na kuthamini nafasi ya mwanamke, sera yao imekuwa na usawa katika meza ya maamuzi.
Aidha amewataka wanawake kote nchini kuungana kwa pamoja kudai mageuzi na kupigania haki zao bila kujali tofauti ya vyama vyao hasa katika kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu.
Amewaomba wanawake kujitokeza kwa wingi katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kupitia vyama vyao, huku akisisitiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ili kuweza kushiriki katika chaguzi zijazo.
Dorothy ameeleza kuwa wametumia wiki ya maadhimisho hayo kwa namna bora wakifanya tamasha la wajasiriamali, kuchangia damu pamoja na kutoa elimi kwa wanawake na kupima saratani ya matiti na kizazi.
Crédito: Link de origem