top-news-1350×250-leaderboard-1

Padri asimulia safari ya jimbo jipya Bagamoyo, alivyotokwa machozi

Bagamoyo. “Nilitokwa machozi ya furaha, sikutarajia jambo hili, maana tulisubiri kwa muda mrefu, lakini wakati wa Mungu ni wakati sahihi, tumshukuru yeye kwa hilo.”

Haya ni maneno ya Paroko wa Parokia ya Moyo Safi wa Bikira Maria, Dk Thaddeus Siya akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Machi 9, 2025, ikiwa ni Jumapili ya kwanza tangu Papa Francis alipounda jimbo jipya Katoliki la Bagamoyo.

Machi 7, 2025, Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki Duniani aliunda jimbo hilo jipya na kumteua Askofu Msaidizi Stephano Musomba kuwa askofu wa kwanza kuliongoza.

Kabla ya uteuzi huo, Askofu Musomba alikuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam tangu alipouliwa na Papa Julai 7, 2021 na kuwekwa wakfu Septemba 21, 2021.

Padri Richard Mjigwa, katika taarifa aliyoandika kwenye tovuti ya Vatican News Machi 7, 2025 alisema jimbo jipya la Bagamoyo limeundwa kwa kumega sehemu ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam na la Morogoro.

Jimbo Katoliki la Bagamoyo linakuwa na parokia 22, mapadri wa jimbo wanane, mapadri watawa 37 na watawa wanane.

Katika misa ya leo Jumapili ambayo mwandishi wa Mwananchi alihudhuria, Paroko Siya amewaeleza waumini namna alivyotokwa machozi alipopokea taarifa za kanisa hilo kuwa Kanisa Kuu la Jimbo.

“Nilitokwa machozi ya furaha, sikutarajia jambo hili, maana tulisubiri kwa muda mrefu, lakini wakati wa Mungu ni wakati sahihi, tumshukuru yeye kwa hilo,” Padri Siya amewaambia waumini ambao walishangilia wakipiga makofi na vigeregere.

Machi 7, 2025, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Jude Thadaeus Ruwa’ichi alitaja parokia 17 zilizomegwa kutoka jimbo hilo kwenda Bagamoyo kuwa Bahari Beach, ⁠Boko, ⁠Bunju,⁠ Kinondo, ⁠Madale, Mbopo, ⁠Mbweni Mpiji, Mbweni  Teta, ⁠Mbweni, ⁠Mivumoni, ⁠Muungano, Nyakasangwe, ⁠Tegeta Kibaoni, ⁠Tegeta, Ununio, ⁠Wazo na ⁠Mbweni JKT (Parokia Teule).

Alisema mapadri waliopo kwenye parokia hizo na waumini wake watakuwa Jimbo la Bagamoyo chini ya uongozi mpya wa jimbo hilo na si kwake tena.

Miaka saba wakisubiri tamko

Nje ya misa, Padri Siya amefanya mazungumzo na Mwananchi kuhusu masuala mbalimbali ya jimbo hilo jipya akisema katika eneo hilo la kanisa, ndipo asili ya chimbuko la Kanisa Katoliki Tanzania na Afrika Mashariki.

Paroko wa Parokia ya moyo safi wa Bikra Maria, ambalo sasa ndilo kanisa kuu la jimbo jipya la Bagamoyo. Dk Thaddeus Siya

“Wamisionari walipokuja Tanzania mwaka 1868 walifikia hapa, wakasimika msalaba na misa ya kwanza walisali eneo la wazi katika Chuo cha Adem (kipo pembeni ya kanisa hilo),” anasema.

Anasema mwaka 1872 ndipo walijenga kanisa dogo ambalo lipo hadi leo na wao wameachiwa upande kama kumbukumbu.

“Mwaka 1913 ndipo walijenga kanisa hili (la Moyo Safi wa Bikira Maria) ambalo ndilo Kanisa Kuu la Jimbo,” anasema Padri Siya mwenye shahada ya uzamili (PhD).

Japo baadhi ya waumini walisema Bagamoyo iliwahi kuwa na jimbo wakati wa ukoloni na kisha kuondolewa, Padri Siya anasema kanisa hilo ni la kwanza la Katoliki Afrika Mashariki.

Akizungumzia alivyopokea taarifa za kuwa jimbo, Padri Siya anasema alizipata mchana wa Machi 7, 2025.

“Nilipigiwa simu na kuambiwa kuanzia saa 7 hadi saa 8 hapa tusiondoke kuna jambo kubwa. Nilipewa maelekezo ikiwamo ya kufungua mlango mkubwa wa kanisa na kupiga kengele.

“Tulijikusanya sisi tuliokuwa karibu, ndipo tukatangaziwa jambo hili kwamba Papa Francisco ameunda jimbo hili na kumteua Askofu Musomba kuwa askofu wa jimbo,” ameeleza huku akionekana mwenye tabasamu.

Anasema taarifa ile ilimtoa machozi ya furaha kwa kuwa mpango wa Mungu umetimia.

“Waumini waliokuwa kanisani walifurahi, waliimba kwa furaha, jambo ambalo walilisubiri kwa miaka saba limetimia,” anasema.

Anasema mwaka 2018 kulikuwa na taarifa za kwamba Bagamoyo inatangazwa kuwa jimbo: “Ilikuwa ni katika Jubilei ya miaka 150, minong’ono ilikuwepo, lakini kanisa lina taratibu zake na leo zimetimia.”

Wajiandaa kumpokea Askofu

Licha ya kutangazwa kuwa jimbo na kupewa askofu siku tatu zilizopita, Paroko huyo anasema walishajenga nyumba ya askofu miaka sita iliyopita.

“Siwezi kusema kwa nini tulijenga, lakini tulijiandaa, nimewambia waumini wetu kwamba tumekuwa wakubwa na majukumu yameongezeka, hivyo tunajiandaa katika hilo,” anasema.

Katika ibada ya leo, ilifanyika harambee ya kuboresha jengo la kanisa ,ambayo itaendelea pia Jumapili ijayo.

“Tunachokisubiri ni kusimikwa kwa askofu wetu ili kuanza kazi kwenye jimbo lake, itakuwa ni ibada kubwa sana kwetu,” amesema Padri Siya.

Naye Sista Evelyne Changa amesema ngazi ya parokia na ngazi ya jimbo ni vitu viwili tofauti, wamefurahia kuwa jimbo na wanajipanga zaidi ya vile walivyokuwa.

“Inatupasa kwenda mbele zaidi kwa kuwa sasa ni jimbo,” amesema Sista Evelyne

Paulo Luis ambaye ni mpiga kinanda wa kanisa hilo, pia amesema taarifa za Bagamoyo kuwa jimbo walikuwa wakizisikia muda mrefu.

“Sisi waumini tulihitaji kujua kwa haraka lini jambo ili litatokea, lakini kumbe kanisa nalo lina utaratibu wake, tulikuwa tukisikia tetesi, lakini hatimaye taratibu zimetimia,” amesema.

Amesema siku amepata taarifa hizo alikuwa kazini kwake yeye ni fundi wa marumaru na siku hiyo aliweka kila kitu chini na kufurahia.

Peter Mbuligwe anasema taarifa hizo amezipata leo baada ya Paroko kuwatangazia kwenye misa ya kwanza.

“Sikuwa nafahamu, nilipomsikia Paroko nilifurahi sana kwa kuwa tayari tulishaanza mchakato muda mrefu ikiwamo ujenzi wa nyumba ya Askofu,” amesema.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.