Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amewakumbusha wanachama kuwa changamoto ya usawa wa kijinsia lipo pia ndani ya chama hicho, hivyo wasiwanyooshee vidole watawala, bali walitatue ndani kwanza.
Lissu ametoa wito huo wakati wa sherehe za Siku ya Kimataifa ya Wanawake (IWD) zilizoandaliwa na Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) jijini Dar es Salaam leo Machi 8, 2025, yeye akiwa ndiyo mgeni rasmi.
Amesisitiza kuwa tatizo la kutozingatia usawa wa kijinsia linakihusu pia Chadema, akitolea mfano katika uongozi wa juu wa chama hicho, wote ni vijana wa kiume. Amesema wanapaswa kujiangalia ndani ya chama kama jukumu hilo linazingatiwa.

“Naomba tuulizane kwa viongozi na wanachama wote mlioko hapa mara ya mwisho lini mliona mwanamke akikaa meza kuu, mara mwisho ilikuwa lini? Mimi nina miaka 21 ndani ya Chadema, sikumbuki kama nimewahi kuona mwanamke kwenye meza kuu,” amehoji Lissu.
Kabla ya kueleza hayo, Lissu amewaomba msamaha wanachama na viongozi wa Bawacha waliohudhuria maadhimisho hayo akisema yale atakayoyazungumza huenda yatawakera baadhi yao.
Huku kukiwa na utulivu ndani ya ukumbi, Lissu ambaye ni mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, amewataka wanaChadema kuacha kuwanyooshea vidole CCM iliyotawala kwa muda mrefu kuhusu usawa wa kijinsia.
“Tusinyooshe vidole kwa hawa waliotawala muda wote, vilevile tunyoosheane vidole wenyewe. Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema, kamati ikitimia inapaswa kuwa na wajumbe 35, walioko hivi sasa ni 26, kati yao wanawake ni watano.

Katibu Mkuu wa Bawacha, Pamela Maassay akizungumza na wanawake waliojitokeza katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambapo Kitaifa Bawacha wameadhimisha mkoani Dar es salaam, katika ukumbi wa Mlimani City.
“Ukiondoa hawa watano, wengine wote kina kaka au nakosea? Kwa hiyo, hili tatizo la kuwaangusha wanawake linatuhusu na sisi kama chama. Sisi tunaopiga kelele sana, ajabu sijawahi kusikia mbona hakuna usawa kijinsia kwenye vikao vikuu vya chama, kwa nini tumenyamaza au tumelinyamazia hili?”
Amefafanua kwamba Chadema wasipolizungumzia hilo, changamoto ya usawa wa kijinsia halitatulika. Amesema wanatakiwa kwenda mbele kwa kufanya mjadala wa ndani ya Chadema kuhusu usawa wa kijinsia.

Kwa mujibu wa Lissu, asilimia 51 ya wapigakura nchini ni wanawake huku akihoji inakuaje ndani ya chama kikuu cha ukombozi na upinzani, uongozi wake wa juu wote ni wanaume.
“Tukiogopa huu mjadala basi tuzibe midomo yetu juu ya mambo yanayofanywa na chama cha… Tukiweza kuzungumza mambo yetu wenyewe kwa wenyewe, hatutakuwa na haki ya kuzungumza.
“Maandiko si yanasema toa kwanza boliti kwenye jicho lako ili kuona vibanzi kwenye jicho la mwingine. Itakuwa si sawasawa tunasherehekea siku ya wanawake wakati safu ya uongozi wa juu inatusuta,” amesema Lissu huku akirejea msamaha kwa aliyoyazungumza.
Azungumzi “No reforms, No Election”
Katika maadhimisho hayo, Lissu amefafanua kwamba ajenda ya “No reforms, No Election” ilikubaliwa na wajumbe wa kamati kuu, kisha mkutano mkuu, siyo yeye binafsi na wakati huo yeye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Tanzania bara.
“Tumetoka kwenye kamati kuu na Mwenyekiti Mbowe (Freeman), tukaenda baraza kuu, lililoitikia, tukaenda kwenye mkutano mkuu na mwenyekiti ni Freeman Mbowe,” amesema.

Ameongeza kuwa mkutano mkuu wa Chadema ulisema “No Reform, No election”, akihoji inakuaje msimamo huo ukawa wa Tundu Lissu, na kuitwa dikteta uchwara? Pia, amewashangaa baadhi ya wajumbe wa kamati wanaodaiwa kusema ni msimamo wake binafsi.
Lissu amesisitiza kuwa kaulimbiu hiyo ni msimamo sahihi wa Chadema, huku akihoji kwamba kunahitajika ushahidi gani kujua kwamba chaguzi zilizopo siyo rafiki kwa vyama vya upinzani.
Amewataka wenye haraka na uchaguzi watulie kwanza wakati huu ambao Chadema kinashinikiza ajenda ya No Reform, No Election itakayohakikisha mchakato huo unakuwa huru na haki kwa vyama vyote.
“Kama suala la kuwahi kwenda bungeni, mimi ndiyo ninapaswa kuwa na haraka nina miaka 57, tuache mambo madogo twende kwenye hoja za msingi ya kupigania mabadiliko,” amesema Lissu.
Crédito: Link de origem