top-news-1350×250-leaderboard-1

Wafanyakazi wapya JKCI waonywa kuhusu rushwa

Na Mwandishi Maalum

Wafanyakazi wapya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wametakiwa kutojiingiza katika vitendo vya rushwa vitakavyosababisha kudhorotesha utoaji wa huduma bora katika Taasisi hiyo.

Rai hiyo imetolewa jana Machi 5,2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dk. Peter Kisenge wakati akizungumza na wafanyakazi hao kabla ya kuanza kazi.

Dk.Kisenge amesema kutoa huduma kwa kufuata maadili ya utumishi wa umma pamoja na kuwa na utashi kutawasaidia kurudisha furaha kwa wagonjwa ambao wamekuwa wakiwategemea.

Baadhi ya wafanyakazi wapya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakila kiapo cha kufuata masharti ya utumishi wa umma wakati wa kikao cha kuwapokea kilichofanyika jana katika ukumbi wa Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Picha na: JKCI

“Hatutaki kusikia mmechukua ama mmetoa rushwa kwani hatutafurahia hata kidogo mtu mmoja aje kusambaratisha umoja wetu tulioujenga katika Taasisi yetu”, amesema Dk. Kisenge

Aidha amewataka wafanyakazi hao kutumia fursa zinazopatikana katika Taasisi hiyo vizuri na kupenda kujiendeleza katika fani zao ili kuleta chachu zaidi katika kutoa huduma bingwa bobezi.

Kwa upande wake Dk. Innocent Humay ambaye ni mwajiriwa mpya katika Taasisi hiyo ameahidi kwa niaba ya wenzake kufanya kazi kwa weledi na kuleta mafanikio zaidi ya Taasisi hiyo.

Dk. Innocent amesema waajiriwa hao walipofika JKCI wamepokelewa vizuri na kupata mafunzo ya siku mbili ambayo yatawasaidia kufanya kazi vizuri

“Kwa niaba ya wenzangu tunahaidi kufanya kazi na kufuata miongozo tuliyopewa kuwasaidia wagonjwa wanaotibiwa hapa”, amesema Dk. Innocent

Kwa mwaka wa fedha 2024/2025 JKCI imepewa kibali cha kuajiri wafanyakazi wapya 51 wa kada mbalimbali ambapo kati yao wafanyakazi 24 wamesharipoti kazini.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.