Washington. Rais Donald Trump amelishangaza Bunge la Marekani baada ya kutangaza kuwa amemteua mtoto, Devarjaye Daniel “DJ Daniel” (13) kuwa Ofisa wa hiari wa Idara ya Usalama wa Taifa (Secret Service) nchini humo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la WION, Trump amechukua uamuzi wa kumteua mtoto huyo kutokana na matamanio yake ya kulitumia jeshi la polisi nchini humo.
Hata hivyo, ndoto ya mtoto ilionekana kutotimia baada ya vipimo vya madaktari kubaini kuwa DJ Daniel anasumbuliwa na maradhi ya saratani kwa miaka mingi na hitilafu kwenye uti wa mgongo wake.
DJ alipokuwa ameketi kwenye jukwaa la wageni, Trump alisimulia hadithi yake, akifichua kuwa aligunduliwa kuwa na aina adimu ya saratani mwaka 2018 na alipewa miezi mitano pekee ya kuishi.
Licha ya kila changamoto anayopitia, DJ aliendelea kupambana bila kukata tamaa ya kutimiza ndoto yake ya kuwa ofisa wa polisi nchini humo.
“Madaktari walimpa muda wa miezi mitano tu ya kuishi. Hilo lilikuwa zaidi ya miaka sita iliyopita. Tangu wakati huo, DJ na baba yake wamekuwa katika safari ya kuhakikisha ndoto yake inatimia.”
“Usiku wa leo, DJ, tutakupa heshima kubwa zaidi ya zote,” Trump alitangaza.
“Ninamwomba Mkurugenzi wetu mpya wa Idara ya Usalama wa Taifa, Sean Curran, akufanye rasmi kuwa wakala wa Idara ya Usalama wa Taifa wa Marekani,” alisema.
Baada ya kutangaza uamuzi huo, ukumbi ulilipuka kwa shangwe na zaidi huku wabunge wa Domecrats zaidi ya 12 wakiungana na wabunge wa Republican kuunga mkono hoja hiyo, jambo ambalo ni nadra kufanywa na pande hizo.
Baba yake DJ Daniel akiwa amejawa na hisia, alimwinua DJ juu huku hadhira ikipiga kelele kwa sauti moja: “DJ! DJ!”
Kisha, Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Marekani, Curran alimkaribia DJ na kumpa beji rasmi ya Idara ya Usalama wa Taifa huku shangwe likiendelea.
DJ, akiwa na tabasamu mwanana, alimkumbatia Curran huku akimshukuru Trump na mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, hali ya mshikamano wa kisiasa kati ya vyama hivyo haikudumu kwa muda mrefu. Trump alipoanza kuzungumzia sera za afya za serikali yake, makofi kutoka upande wa wabunge wa Democrats yalianza kupungua.
Mbunge wa Democrats, Rashida Tlaib huku akiwa kimya kibao cheupe kilichoandikwa: “Umepunguza ufadhili wa utafiti wa saratani,” akipinga maamuzi ya bajeti ya rais Trump.
Katika kitendo kingine cha hisia kali, Trump aliipa heshima familia ya Laken Riley, mwanafunzi wa miaka 22 kutoka Georgia aliyeuawa mwaka jana alipokuwa akifanya mazoezi ya kukimbia.
Katika tukio hilo, mhamiaji asiye na vibali kutoka nchini Venezuela alikutwa na hatia ya mauaji hayo kisha kuhukumiwa kifungo cha maisha bila jela.
“Laken alinyang’anywa uhai wake kutoka kwetu na mshiriki wa genge la wahamiaji haramu ambaye alikamatwa kwa kuvuka mpaka wa kusini ulio wazi wa (rais wa zamani Joe Biden) na kisha kuachiwa huru ndani ya Marekani chini ya sera za kikatili za utawala huo ulioshindwa,” Trump alisema.
“Marekani haitamsahau kamwe Laken wetu mrembo,” aliongeza, akiapa kuhakikisha hakuna familia nyingine itakayopitia janga kama hilo.
Pia aliangazia Sheria ya Laken Riley, iliyowasilishwa muda mfupi baada ya yeye kurejea madarakani, ambayo inahitaji wahamiaji wasio halali waliokabiliwa na mashtaka kuzuiliwa.
Akiita sheria hiyo kitendo thabiti na chenye nguvu, Trump aliwasilisha sheria hiyo kama nguzo muhimu ya msimamo wake mkali kuhusu uhamiaji.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.
Crédito: Link de origem