top-news-1350×250-leaderboard-1

Fanyeni haya huenda mvutano wa Chadema, Serikali utamalizika

Jumapili iliyopita, nilihudhuria mkutano kati ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, na Jukwaa la Wahariri. Kama mmoja wa wahariri waliokuwepo, nilipata fursa ya kuuliza maswali na kuchangia hoja.

Licha ya kwamba Tundu Lissu na Chadema walituita ili kutufafanulia kaulimbiu yao ya “No Reforms, No Election” ili sisi wahariri tuwaelezee Watanzania hoja yao kuhusu umuhimu wa mabadiliko, niliona kuwa ingawa madai yao ya reforms ni ya msingi, hoja ya no election haina mashiko.

Uchaguzi ni suala la kikatiba na hakuna mtu au taasisi yoyote inayoweza kuzuia kufanyika kwa uchaguzi mkuu.

Nilipopata fursa ya kuchangia, nilieleza dhana ya siasa za utopia yaani siasa za hadaa, kwamba hakuna mtu anayeweza kusimamisha uchaguzi.

Hata hivyo, kwa kuwa madai yao ya mabadiliko ni ya msingi, niliwashauri badala ya kuendelea kuhubiri siasa za hadaa, watumie siasa za kimkakati na waendeleze mazungumzo.

Nilikumbusha jinsi Rais Samia Suluhu Hassan alivyoonesha nia njema kwa Tanzania, ikiwa ni pamoja na kumtembelea Tundu Lissu alipokuwa hospitalini Nairobi baada ya shambulio alilopata la kupigwa risasi akiwa jijini Dodoma.

Aidha, nilimkumbusha Lissu kuwa Rais Samia alikutana naye alipokuwa Ubelgiji na baadaye aliporejea Tanzania, alifuta kesi ya ugaidi dhidi yake, akaanzisha maridhiano kati ya CCM na Chadema na kuruhusu mikutano ya hadhara.

Sasa, Serikali ya Awamu ya Sita imekuja na sheria mpya ya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kuibadilisha Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuiita Tume Huru ya Uchaguzi.

Hata hivyo, licha ya hatua hizi, bado Chadema hawana imani kuwa watasikilizwa na wanataka kulazimisha mambo ambayo hayawezekani.

Katika mkutano huo, Tundu Lissu alimpa nafasi Katibu Mkuu wake, John Mnyika, kujibu hoja yangu kuhusu maridhiano. Makamu Mwenyekiti, John Heche, aliposimama kuchangia, alieleza kwa uchungu kuhusu damu iliyomwagika kwenye figisu za uchaguzi, akitaja kumpoteza kaka yake wa tumbo moja kwa sababu ya siasa.

Kwa uchungu, Heche alisema kwamba bila mabadiliko, basi wao ama wataishia magerezani au makaburini. Ushuhuda wake ulikuwa wa kugusa hisia.

Pamoja na yote, ni muhimu kutambua kuwa wapinzani ni Watanzania wenzetu na haki inapaswa kutendeka kwa wote. Madai yao ya mabadiliko madogo ya katiba ni ya msingi.

Kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi, baadhi ya mambo muhimu tunayoyataka yafanyike kabla ya uchaguzi wa 2025 tayari yamefanyika, mengine hayajatekelezwa kikamilifu na baadhi hayajafanyika kabisa ikiwa ni pamoja na hitaji kubwa la mabadiliko madogo ya katiba.

Kwa msingi huo, tunapaswa kuendelea kumuomba Rais Samia, kwa heshima na kwa kumchukulia kama Mama wa Taifa, atusikilize. Ingawa kanuni ni kwamba wengi wape, wachache pia wanapaswa kusikilizwa. Katika hili la mabadiliko madogo, naona Chadema wana hoja ya msingi na wasihesabiwe kama wapinzani pekee, bali kama Watanzania wachache wenye hoja zinazopaswa kusikilizwa.

Katika hili, ningependa kushauri, Chadema na wapinzani wengine watumie muda mfupi uliobaki kwa siasa za kimkakati badala ya siasa za kiharakati. Kama ilivyotokea Marekani, wanapaswa kutumia fursa iliyopo kufanya siasa za ukweli na si kupoteza muda na siasa za utopia.

Lakini pia mabadiliko madogo ya katiba yanaweza kufanyika kwa hati ya dharura. Muhimu ni utashi wa kisiasa kutoka kwa Rais Samia na sheria mpya ya uchaguzi inapaswa kurekebishwa.

Vifungu batili viondolewe ili kila Mtanzania awe huru kupiga kura kumchagua kiongozi anayemtaka kwa mujibu wa Ibara ya 5 ya Katiba. Kwa sasa, Mtanzania analazimika kuchagua mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.

Ibara ya 21 ya Katiba irekebishwe kusudi kila Mtanzania awe na haki ya kugombea uongozi bila kulazimika kwanza kujiunga na chama cha siasa. Kwa sasa, mfumo huu unakwamisha watu makini kuingia kwenye uongozi wa umma.

Na Tume Huru ya Uchaguzi iwe kweli huru na shirikishi kwa sababu wananchi walitaka tume huru yenye mchakato shirikishi, si kubadili jina kutoka NEC kuwa INEC huku muundo ukiwa ule ule.

Ifike mahali uwanja wa siasa usawazishwe ili uchaguzi wa 2025 uwe wa haki.

Iwapo haya yatafanyika, basi uchaguzi wa 2025 utakuwa huru na wa haki kwa Watanzania wote.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.