top-news-1350×250-leaderboard-1

‘Wajasiramali tumieni maabara ya mkemia mkuu kupima sampuli za bidhaa’

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wajasiriamali nchini wameshauriwa kutumia Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kupima bidhaa zao kabla ya kuzipeleka nje ya nchi kuepuka kurudishwa kwa kushindwa kutimiza vigezo.

Maabara hizo zimepata ithibati hivyo mfanyabiashara au mjasiriamali atakayezitumia atapata matokeo ambayo yanakubalika kitaifa na kimataifa.

Ushauri huo umetolewa Machi 3,2025 na Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uchunguzi wa Bidhaa za Mazingira kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Dk. Shimo Peter, wakati akizungumza katika mahojiano na waandishi wa habari kwenye maonesho ya wanawake na vijana wajasiriamali yaliyoandaliwa na Chama cha Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC) ambapo mamlaka hiyo inashiriki.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, akisaini kitabu cha wageni wakati alipotembelea banda la Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) kwenye Maonesho ya Wajasiriamali Wanawake na Vijana Mlimani City Dar es Salaam. Kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Uchunguzi wa Bidhaa za Mazingira, Dk. Shimo Peter.

“Tuna kurugenzi maalumu kwa ajili ya uchunguzi wa bidhaa ambazo zinazalishwa hapa nchini, tuna uwezo wa kuwapa taarifa ya uchunguzi ambayo imeainisha viwango, imeainisha viambata, ubora na usalama wa bidhaa. Lengo ni kuhakikisha wanazalisha bidhaa ambayo itamlinda mlaji, wanazalisha bidhaa ambazo zinakidhi soko la ndani na soko la nje.

“Katika shughuli za uchunguzi wa kimaabara, maabara yoyote ile ili iweze kutambulika duniani au nchini lazima iwe imepata ithibati, ithibati ni moja ya kigezo ambacho kinawezesha bidhaa yoyote kuuzwa nchi za nje. Sisi maabara zetu zimepata ithibati hivyo, mfanyabiashara au mjasiriamali atakayetumia Maabara za Mkemia Mkuu wa Serikali atakuwa na uwezo wa kupata matokeo ambayo yanakubalika kitaifa na kimataifa,” amesema Dk. Peter.

Aidha amesema wanatumia maonesho hayo kutoa elimu kuhusu shughuli za Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kuhakikisha wajasiriamali wanazalisha bidhaa ambazo zinakidhi viwango vya ubora vya kitaifa na kimataifa.

“Kama utakuwa umepima sampuli zako kwa kutumia maabara ambayo ina ithibati itakuwezesha kukupa matokeo ambayo ni sahihi na ambayo yanakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa na utakuwa na uhakika wa bidhaa ambayo umeuza.

“Watumiaji nao wawe na uelewa wa bidhaa na kuhoji kama bidhaa wanazonunua zimepimwa katika maabara ambazo zinatambulika kitaifa na kimataifa ili walaji wawe na afya bora na kuwa na bidhaa ambazo zinakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa,” amesema.

Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, ambaye alitembelea banda la GCLA kwenye manonesho hayo ameipongeza kwa kazi nzuri wanazofanya hasa za uchunguzi wa sampuli mbalimbali na kuitaka kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli zinazofanywa na mamlaka hiyo.

Crédito: Link de origem

Leave A Reply

Your email address will not be published.