Dar es Salaam. Huenda sasa kilio cha foleni kwa wanaotumia vyombo vya moto vya gesi kikapungua kutokana na ongezeko la vituo vya kujazia gesi, wachambuzi wanasema manufaa si tu kwa kundi hilo.
Matumizi ya gesi asilia kwenye magari kawaida huokoa gharama kwa zaidi ya asilimia 50 ikilinganishwa na dizeli na petroli. Kwanza, gesi huuzwa bei ya chini, lakini unywaji wake sio mkubwa kama ilivyo kwa mafuta. Pia matengenezo ya gari (Sevisi) huchukua muda mrefu kwa kuwa gesi huzalisha moshi kidogo.
Leo, Machi 3, 2025, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limesema katika kukabiliana na uhaba wa vituo vya kujaza gesi kwenye magari, vituo saba vinaendelea kujengwa na vipo katika hatua mbalimbali za ujenzi jijini Dar es Salaam.
Vituo hivyo ni TAQA Dalbit Tanzania kando ya barabara ya Bagamoyo, Energo Tanzania Limited barabara ya Coca-cola, Puma Energy Tegeta IPTL Dar es Salaam, Puma Energy Mbezi Beach – Tangi bovu, Puma Energy Mabibo External, BQ Constructors barabara ya Goba, pamoja na Tanhealth Jangwani Beach Mbezi.

Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa TPDC, Derick Moshi, katika ziara ya bodi ya wakurugenzi wa TPDC waliofanya ziara ya kukagua ujenzi wa kituo cha kujaza gesi barabara ya Sam Nujoma, kando ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam amesema kuna habari njema.
“Vituo hivyo saba vinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa 2025. Kwa sasa tuna vituo sita vinavyotoa huduma ya gesi kwenye magari nchi nzima, vituo vinne vinatoa huduma ya gesi kwa magari na bajaji, vituo viwili vinahudumia magari ya Dangote,” amesema.
Moshi amesema kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kutakuwa na vituo viwili vya kujaza gesi kwenye magari vitakavyoongezeka vikimilikiwa na Kampuni ya TAQA Dalbit pamoja na TPDC.
Akizungumzia kituo cha kujaza gesi barabara ya Sam Nujoma, Moshi amesema kimekamilika na sasa kinachofanyika ni ufuatiliaji wa mifumo ya gesi kwenye kituo hicho kubaini usalama wa mifumo yake.
“Kituo kimeshakamilika kwa kiwango kikubwa, na gesi tayari ipo. Tunachosubiri kwa sasa ni majaribio kwa magari,” amesema.
Mradi wa kituo mama cha ujazaji gesi cha Mlimani ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kukuza matumizi ya nishati mbadala na kupunguza gharama za uendeshaji kwa watumiaji wa magari yanayotumia gesi badala ya petroli au dizeli.
Mwakilishi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Paul Makanza amesema bodi ya TPDC imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya gesi.
“Tumeridhika kama bodi kwa maendeleo ya mradi huu. Unapokuwa mkubwa, faida zake zitakuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa kwa kupunguza utegemezi wa mafuta ya petroli,” amesema Makanza.
Kwa mujibu wa TPDC, ujenzi wa kituo cha kujaza gesi Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam unagharimu Sh14.55 bilioni, na kituo kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kushindilia gesi kwenye magari matatu ya kusafirisha gesi kupeleka mahali pengine na kujaza magari 1000 kwa siku.

TPDC inaeleza kiwango cha gesi kinachoweza kushindiliwa kwa siku na mitambo ya kituo hicho ni futi za ujazo milioni tatu kikihudumia magari na viwanda, kikiwemo kiwanda cha dawa Kairuki kilichopo Kibaha mkoani Pwani. Kituo hicho kitakuwa na pampu nne za kujaza gesi zenye uwezo wa kuhudumia magari manane kwa wakati mmoja.
Mchambuzi wa masuala ya maendeleo na siasa, Dk Onesmo Kyauke amesema ongezeko la vituo vya kujaza gesi kwenye magari ni hatua nzuri kwani kutapunguza uagizaji wa mafuta nje ya nchi.
“Uagizaji wa mafuta ukipungua, matumizi ya fedha za kigeni nayo yatapungua. Hivyo, shilingi yetu itaimarika. Pia, ongezeko hili litachangia ajira nyingi kwa vijana hasa kujiajiri kwenye bajaji na gari mtandao,” amesema.
Dk Kyauke amesema jambo ambalo Serikali ianze kulitazama ni kuanzisha vituo vya kujaza gesi katika mikoa ambayo bado haijafikiwa na nishati hiyo pamoja na kupanua wigo wa matumizi ya nishati hiyo majumbani.
“Wajitahidi kutanua matumizi majumbani kwa sababu nishati hii inasaidia kwenye mazingira,” amesema.
Naye dereva wa teksi mtandao, Shaban Mponda amesema ongezeko la vituo vya kujaza gesi ni nafuu kwao akisema uchache wa vituo ndio unawafanya watu kushindwa kubadili mifumo ya magari yao.
“Vituo vingekuwa vingi hakuna mtu ambaye angetumia mafuta kwenye biashara hasa kwa wanaofanya safari za kuzunguka hapa Dar es Salaam. Gesi ni nafuu, changamoto ni upatikanaji. Wakijenga vituo vingi watavutia watu wengi zaidi,” amesema.
Taarifa ya TPDC inaonyesha ujenzi wa kituo kimoja cha kujaza gesi inagharimu kati ya Sh2.1 bilioni hadi Sh2.7 bilioni kulingana na ukubwa na mahitaji ya eneo wakati kituo cha mafuta ni Sh400 milioni.
Kuhusu kiwango cha gesi Kilichopo nchini
Tanzania inakadiriwa kuwa na futi trilioni 230 za ujazo za gesi asilia, ingawa zilizothibitishwa mpaka sasa ni futi trilioni 57.5, hivyo kuiweka kwenye ramani ya dunia ikishika nafasi ya 82.

Gesi hiyo tayari imeanza kuchimbwa katika visiwa vya Songosongo wilayani Kilwa Mkoa wa Pwani na eneo la Msimbati mkoani Mtwara, ikitumika kuzalisha umeme na kuendesha mitambo ya baadhi ya viwanda nchini.
Faida za kutumia gesi ikilinganishwa na mafuta
Taarifa zilizopo zinaonyesha kuwa gesi asilia katika mfumo wa CNG kama nishati katika matumizi kwenye magari ni nishati ya gharama nafuu ikilinganishwa na dizeli na petroli.
Bei ya gesi asilia ni nafuu kuliko bei ya dizeli; kwa mfano, bei rejareja ya gesi asilia katika mfumo wa CNG kwa sasa ni Sh1,550 kwa kilo moja, wakati bei ya petroli ni Sh2,820 kwa lita moja.
Kadhalika, matumizi ya gesi kwenye magari ni nafuu kuliko mafuta kwani kwa gari ambayo inatumia lita moja ya petroli kwa kilometa 12, kwa upande wa gesi kilo moja inaweza kwenda kwa zaidi ya kilometa 20.
Gesi asilia inapatikana/inazalishwa nchini, itasaidia watumiaji wa nishati hii kuwa na uhakika wa upatikanaji wa nishati ya kuendesha magari yao wakati wote (Security and reliability of supply) katika bei inayotabirika zaidi kuliko ilivyo kwa upande wa mafuta ambayo huagizwa toka nje ya nchi, na pia bei za mafuta hubadilika mara kwa mara kutegemea soko la mafuta dunia.
Matumizi ya gesi asilia kwenye magari kwa ujumla yanasaidia nchi kuokoa fedha za kigeni ambazo zingetumika kuagiza mafuta kama dizeli na petroli kutoka nje ya nchi. Mpaka sasa Tanzania imegundua mita za ujazo trilioni 57 za gesi asilia.
Vilevile, gesi asilia ni nishati rafiki kwa mazingira kwa sababu inatoa kiwango kidogo cha gesi ukaa (CO2) ukilinganisha na petroli na dizeli, hivyo matumizi ya gesi kwenye magari hayo itasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira.
Crédito: Link de origem