Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imezindua mpango wa kuwapatia mikopo vijana wanaotaka kujiajiri na kujipatia kipato kwa kufanya kazi masaa 24, ikiwa ni hatua ya kupambana na changamoto ya ajira na kuhamasisha uzalishaji.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo katika Soko la Kariakoo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema wamejipanga kuhakikisha kuna ulinzi na usalama wa kutosha kwa wafanyabiashara na mali zao.
“Kwa sasa ni mwendo wa ‘Dar Biashara Masaa 24’, na tunahakikisha wafanyabiashara wanapatiwa huduma za msingi kama intaneti ya bure (free Wi-Fi), kamera za CCTV kwa ulinzi, na mazingira bora ya kufanya biashara,” alisema Chalamila.
Aliongeza kuwa serikali inajadiliana na Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa, kuhusu kurekebisha muda wa mwisho wa kuuza pombe, ili watu waweze kunywa kwa utaratibu mzuri.
Mpango huu pia utafika kwenye masoko mengine kama Manzese, Mbagala na maeneo mengine ya jiji, ambapo wafanyabiashara wa Soko la Congo na wengine wanakaribishwa kushiriki.
Mpango huu unalenga kuboresha mazingira ya biashara, kuhamasisha vijana kujiajiri, na kuleta ustawi wa kiuchumi jijini Dar es Salaam.
Crédito: Link de origem